Dar es Salaam. Serikali imeziomba nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kuipa taarifa ya mikutano waliyoifanya bila ya kuishirikisha hivi karibuni.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akizungumzia na waandishi wa habari ofisini kwake jana alisema wameziomba nchi hizo kuitaarifu kile walichokijadili.
Alisema kwakuwa nchi hizo ni miongoni mwa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zilitakiwa kutoa maelezo kwa Umoja huo ili kila nchi wanachama ziweze kutambua lengo lao.
Membe alisema pia Serikali ya Tanzania, imeziomba nchi hizo kuwapa maelezo ya kile walichokuwa wakikijadili katika mkutano wao wa hivi karibuni uliofanyika Kenya.
“Tumewaomba wenzetu hawa, kutueleza mkutano wao ulikuwa unahusu nini, kwani tulipaswa kujua kutokana na kuwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hata kama hawakutaka kutushirikisha,” alisema Membe na kuongeza: “Nawaomba Watanzania wenzangu wasiwe na wasiwasi juu ya mkutano huo, kwani tuna kila kitu hapa nchini. Hatuna haja ya kuanza kufikiri mambo ambayo hayana msingi wowote.”
Alisema uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda umeanza kuimarika baada ya marais wa nchi hizo, Jakaya Kikwete na Paul Kagame, kukubaliana kuanza mazungumzo yatakayokuwa yakifanyika katika nchi hizo.
Membe alisema Rais Kikwete na Rais Kagame, walikutana peke yao, wakiwa na lengo la kuelezana na kuelimishana mambo mbalimbali na walikubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
“Rais Kikwete amesema mkutano ulikuwa mzuri, wamezungumza mambo mengi na wamekubaliana kuanza kufanya mazungumzo yatakayokuwa yakifanyika Tanzania na Rwanda, hii itakuwa ni kuimarisha uhusiano wetu na wao,” alisema Membe.
“Hali hii inakata majungu, uongo na fitna zilizokuwa zikienezwa na watu, ambavyo vingeweza kusababisha kutokuelewana baina yetu na wenzetu wa Rwanda.”
Alisema katika mkutano huo, marais hao walielezana, kuchambua na kujadili ukweli, lengo likiwa ni kurudisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment