Umoja wa Mataifa, UN umewataka waasi wa kundi la M23 kuweka silaha chini ili kumaliza mapambano yanayofanyika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuleta athari mbaya kwa wananchi.
Umoja huo umesema kumalizwa mapambano kati ya majeshi ya umoja huo na waasi wa M23 kutasaidia kupatikana kwa njia za kuleta suluhu baina ya pande hizo mbili.
Wito huo umetolewa na mjumbe maalum wa kanda ya Maziwa Makuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Mary Robinson ambaye ametoa wito huo wakati wa ziara yake mashariki mwa DRC eneo ambalo linakabiliwa na vita.
Hatua hiyo imekuja huku majeshi serikali ya Kongo yakishirikiana na majeshi ya Umoja wa Mataifa yakiwa yamefanikiwa kuidhibiti ngome muhimu ya waasi wa M23.
Bi Robinson akiwa mjini Goma baada ya kuzungumza na viongozi wa serikali za mitaa na wakazi wa mji huo amesema kuwa waasi wa M23 lazima wakomeshe mapambano na kusalimisha silaha kama ilivyopendekezwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Bi. Robinson aliwasli nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku majeshi ya DRC yakisaidiwa na JWTZ na MONUSCO yakijipanga kuikomboa ngome ya Kibumba inayoshikiliwa na waasi wa M23 iliyoko kilomita 30 kaskazini mwa Mji wa Goma.
Ijumaa iliyopita wapiganaji wa M23 walirudi nyuma kutoka katika maeneo waliyokua wakiyashikilia kuzunguka Mji wa Goma.
Waasi hao waliikimbia ngome yao baada ya kupewa kichapo kitakatifu na mjeshi ya MONUSCO yanayoongozwa na jeshi imara la JWTZ.
Chanzo:- Mpekuzi
No comments:
Post a Comment