WITO uliotolewa na viongozi wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu wa kuitaka Serikali ya Kongo ikae meza moja na waasi wa M23 kwa ajili ya kutatua mgogoro wao, umepokewa kwa mikono mwili na waasi hao, ingawa wametoa angalizo la kurudi tena kwenye uwanja wa mapambano iwapo watachokozwa.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu, kiongozi wa kundi hilo la waasi wa M23, Betrand Bisiimwa, alipongeza uamuzi huo wa kuwataka wakutane na Serikali ya Kongo kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wao ambao umedumu kwa muda mrefu.
Bisiimwa akizungumzia uamuzi huo uliofikiwa hivi karibuni katika kikao kilichoketi Uganda, kilichowashirikisha Rais Jakaya Kikwete, Paul Kagame wa Rwanda, Joseph Kabila wa Kongo, Yoweri Museveni wa Kongo na wengine, alisema kikundi chake kilifanya juhudi kama hizo kwa zaidi ya miezi kumi iliyopita, lakini serikali ya Kongo iliwapuuza, hivyo kusisitiza kwamba wapo tayari kwa mazungumzo au kuendelea na mapigano.
“Naupongeza wito wa viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu kwa sababu wameona umuhimu wa kuyaokoa maisha ya Wakongomani wa hapa mjini Goma, siku zote amani inatafutwa kwa makubaliano ya kukaa meza moja, lakini ukiamua vita hauwezi kushinda,” alisema Bisiimwa.
Wakati Bisiimwa akitoa kauli hiyo, siku chache zilizopita alikaririwa na gazeti dada la MTANZANIA Jumatano akikiri kuwa majeshi ya Umoja wa Mataifa ni hatari na yanaweza kuwamaliza.
Hivi karibuni viongozi wa nchi zinazounda Ukanda wa Maziwa Makuu ulitoa wito wa siku tatu kwa Serikali ya Kongo kukutana na waasi wa M23, ili kujadili njia zitakazoleta amani katika eneo la Mashariki mwa Kongo.
Rais wa Uganda, Museveni, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo, ameelezea uwepo wa nafasi kubwa ya kufikia makubaliano ya kumaliza mapigano kati ya pande zote mbili.
Mbali na hilo, MTANZANIA Jumapili ilipomtaka athibitishe kama wapiganaji wake wapo tayari kusalimisha silaha, alikataa na kusema wapo tayari kwa vita.
“Jeshi langu limerudi nyuma tena kwa kilomita mbili kutoka mji mdogo wa Kanyaruchinya kwa lengo la kurejesha amani katika mji wa Goma na pia kupisha uchunguzi wa makombora yaliyotokea katika mji huu na nchi ya jirani ya Rwanda, sasa kama wakitufuata huku kwa ajili ya vita tutapambana nao, na kama ni mazungumzo ya amani basi ninaunga mkono hilo,” alisema.
Wakati kiongozi huyo wa M23 akisema hayo, zipo taarifa zinazodai uamuzi wa waasi hao kurudisha nyuma vikosi vyake unatokana na kipigo kikali walichokipata katika mapigano yaliyotokea katikati ya wiki iliyopita, kutoka kwa kikosi cha FIB ambacho kipo chini ya jeshi la kulinda amani la MONUSCO, kikiongozwa na askari wa JWTZ.
Habari ambazo zimenaswa na gazeti hili zinasema kuwa jeshi la MONUSCO imefanikiwa kuchukua umiliki wa mji wa Goma kwa asilimia 95, huku kikosi cha askari wa Serikali ya Kongo wanaoshirikiana na FIB wakitangaza nia ya kuendeleza mapigano dhidi ya waasi wa M23, kwa lengo la kuwapokonya silaha.
Chanzo:- Mtanzania.
No comments:
Post a Comment