Social Icons

Friday, 6 September 2013

WABUNGE WAZICHAPA BUNGENI NA POLISI.....

L*Sugu, Kasulumbayi wazichapa kavukavu na polisi...
*Ajeruhiwa, polisi watangaza kumsaka kila kona...
*Mbowe achafua hali ya hewa...








UKUMBI wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, jana uligeuka ulingo wa masumbwi, baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kupigana hadharani na askari wa Bunge.

Wabunge hao walichapana ndani na nje ya ukumbi, hali iliyosababisha tafrani kubwa, huku maofisa usalama na askari polisi kutoka kituo kikuu mjini Dodoma, wakilazimika kuitwa kwenda kuongeza nguvu ili kukabiliana na hali hiyo.

Hatua ya vurugu hizo, ilikuja baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kunyanyuka ili kutaka kutoa hoja, ambapo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtaka kukaa chini hali iliyowafanya wabunge wote wa upinzani kunyanyuka wakiashiria kumuunga mkono.

Mbowe, alisimama bungeni baada ya kutangazwa matokeo ya kutaka kuendelea na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mkoani, Ali Khamis Seif (CUF), kuomba mwongozo wa Spika wa kutaka Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uahirishwe hadi pale yatakapopatikana maoni ya wadau kwa upande wa Zanzibar.

Hoja hiyo, ilionekana kuwa mwiba mkali, baada ya Seif pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu kutoa taarifa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, Pindi Chana (CCM), kuwa amelidanganya Bunge kwa kutoa taarifa ya uongo.

Baada ya hoja hizo, Naibu Spika Ndugai, aliamuru kupigwa kura za kutaka kuendelea na mjadala huo ambapo wabunge 157 wakitaka kuendelea na mjadala huo, huku 59 wa kambi ya upinzani wakitaka usiendelee.

“Baada ya kutangazwa kwa matokeo haya ya kuamua kuendelea na mjadala ama laa kama alivyowasilisha mheshimiwa Ali, sitataka kupokea taarifa yoyote.

“Ninachotaka kuwahakikishia kiti changu kinatenda haki kwa kila upande wa vyama humu ndani, ila ninachotaka kusema hakilali kitu hapa,” alisema Ndugai.

Wakati Ndugai, akiwa amemtaka mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), ili aweze kuendelea na hoja hiyo ndipo aliposimama Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akitaka kutoa taarifa huku Naibu Spika akimzuia kwa kumtaka akae chini hali iliyowafanya wabunge wote wa upinzani kunyanyuka ndani ya Bunge kama njia ya kupinga hali hiyo.

Wabunge hao waliosimama ni wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, hali iliyomfanya Naibu Spika Ndugai kutoa amri kwa askari wa Bunge kumtoa nje Mbowe.

Agizo hilo la Ndugai liliibua hisia kutoka kwa wabunge wa vyama hivyo na kwenda karibu na kiti cha Mbowe kama njia ya kumlinda ili asiweze kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge na askari hao kama ilivyoamuriwa.

Mvutano huo, ulioanza saa 6:35 mchana hadi saa 7 mchana, ilimlazimu Ndugai kutoa agizo tena mara ya pili kwakumtaka kiongozi wa askari hao kutekeleza agizo hilo kwa kumtoa nje Mbowe.

Chanzo:- Mtanzania.

No comments:

 
 
Blogger Templates