MAMIA ya wakulima wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, wamefunga barabara kwa saa nane kwa kile walichodai wamechoshwa na vitendo vya wafugaji kupeleka mifugo katika mashamba yao. Wananchi hao walifunga barabara eneo la Doma lililopo mpakani mwa Wilaya ya Mvomero na Kilosa, huku wakiwa na silaha za kijadi kama mapanga, marungu, mawe pamoja na maji na pertoli.
Kufungwa kwa barabara hiyo kulisababisha watumiaji wa barabara hiyo waliokuwa wanakwenda Kongo, Zambia, Afrika Kusini na mikoa mingine kushindwa kuendelea na safari, jambo lililoleta usumbufu mkubwa.
Kutokana na hali kuwa tete eneo hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alifika eneo hilo akiambatana na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa na mabomu na silaha za moto.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alimtuma Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Elia Ntandu, kwa lengo la kutafuta suluhisho la wakulima na wafugaji hao.
Wananchi hao walionekana kuwa na hasira waliwaeleza viongozi hao kwamba wamechoshwa na vitendo vya wafugaji kuharibu mazao yao kwa kulisha mifugo nyakati za mchana na usiku.
Walisema mbali ya kuharibu mazao yao yaliyopo eneo la Msongori, wamekuwa na mapigano ya mara kwa mara kati yao na wafugaji huku wanawake wakibakwa na wafugaji.
Walisema vitendo vya ubakaji kwa wanawake vinaleta hofu ya usalama wao wa maisha kiafya na kijamii.
Hata hivyo, baada ya kutoa malalamiko yao, Shilogile, aliwaomba wananchi hao kufungua barabara magari yaweze kuendelea na safari zao, lakini waligoma na kudai wapate suluhisho la kero zao.
Wananchi hao waliwataka viongozi hao kwenda maeneo ya mashamba kushuhudia uharibifu uliofanywa na wafugaji hao kitendo kilichokubaliwa na pande zote.
Wananchi hao waligawanyika makundi mawili huko moja likibaki barabarani na wengine kuambatana na viongozi hao kwa ajili ya kuwaonyesha mashamba yao yalivyoharibiwa.
Wakati wakishuhudia uharibifu huo, ghafla vijana waliokuwa wamepakizana katika pikipiki walifika eneo hilo kitendo kilichozua mvutano tena kwa kuwa walitaka kupewa jibu hapo hapo shambani.
Kutokana na mvutano huo, viongozi hao pamoja na wananchi waliamua kurejea Doma kusuluhisha mgogoro lakini hali ilibadilika ghafla baada ya polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya barabarani.
Polisi walilazimika kutumia mabomu kutokana na wananchi hao kuzidi kukaidi amri ya kufungua barabara, ili mazungumzo yaweze kufanyika pembeni.
Licha ya wananchi kujiandaa na maji, petroli na silaha nyingine hazikufua dafu kwa polisi na badala yake kila mmoja alikimbia kuokoa maisha yake.
Hata hivyo, taarifa ambazo zililifikia MTANZANIA Jumatatu zilieleza kwamba, kutokana na kufungwa kwa barabara hiyo, watumiaji wa njia hiyo walilazimika kuuziwa chakula kwa bei ghali.
Ilidaiwa kwamba, wali kuku au nyama uliuzwa kati ya Sh 4,000 hadi Sh 5,000 badala ya Sh 3,000 za kila siku.
Chanzo:- Mtanzania
No comments:
Post a Comment