Social Icons

Tuesday, 8 October 2013

KIKWETE: MAENDELEO HAYATALETWA NA MIJADALA ISIYOISHA.


Rais Jakaya Kikwete, amesema Tanzania haiwezi kuendelea kwa mijadala isiyoisha na vikao vya kulipana posho bali kwa viongozi kufanya maamuzi na kuyatekeleza haraka.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inachelewa kupata maendeleo ya haraka kwa sababu kila mtu anayepewa kazi anataka kwanza kujadili badala ya kuchukua maamuzi na kuyatekeleza.

Alitoa tahadhari hiyo alipozindua Kambi ya Vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na wananchi kabla ya kuzindua kambi hiyo na kukagua shughuli zinazofanywa na vijana 50 kutoka vijiji vya Wilaya ya Rufiji ambao wanajifunza mbinu na maarifa ya kilimo bora katika kambi hiyo, alitaka kujua kama makampuni mawili yaliyoomba ardhi ya kulima kisasa katika bonde la Mto Rufiji, yamepewa ardhi ya kuanza kulima. 

Awali katika maelezo yaliyosomwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la Rufiji (RUBADA), Aloyce Masanja yaliashiria kuonyesha kuwa makampuni hayo, Frontline Development Partners na Lukurilo Holdings Company Limited yalikuwa yamepewa ardhi na Mamlaka hiyo kama yalivyokuwa yameomba.

Lakini Rais Kikwete alipotaka maelezo ya ziada kutaka ukweli kama makampuni hayo yamepewa ardhi na ni kiasi gani, Masanja alithibitisha kuwa Frontline Development Partners walioomba hekta 20,000 walikuwa hawajapewa hata hekta moja na kuwa Lukurilo Holdings walioomba hekta 12,000 walikuwa wamepewa 4,000 tu.

Rais Kikwete alishangazwa na hali hiyo na kusema: “Kwa miaka minne sasa tumekuwa tunazungumza jambo hili bila kufikia uamuzi wake. Tumewahi kujadili suala hili pale Ikulu, Dar Es Salaam, na kukubaliana. Imetokea nini? Tulikubaliana kutekeleza jambo hilo sasa tunaendelea kujadili nini?”

Alisema: “Nchi yetu itachelewa sana kupata maendeleo kwa sababu kila mtu anayepewa kazi anataka kuanza kujadili. Tanzania haiwezi kuendelea kwa mijadala na kwa vikao vya kulipana posho visivyoisha. Hatuwezi kuendeleza nchi kwa mwenendo huu-Frontline Company imeanza kuomba ardhi ya kulima kiasi cha miaka mitano iliyopita.”

Rais Kikwete ambaye aliwaamuru viongozi wote wanaohusika na suala hilo kukutana wiki ijayo alisema: “Nchi inakwamishwa na watu wa namna hii, kila siku kuzungumza na kujadiliana…hadithi haiishi. Maendeleo yetu yanachelewa kwa sababu mizunguko-kila siku mnazunguka, hammalizi.”
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 
 
Blogger Templates