Mtoto wa kiume wa dikteta wa Libya aliyeuwawa Moamer Gaddafi Alhamisi (19.09.2013) amefikishwa mahakamani katika mji wa Zintan kwa mashtaka ya kuvuruga usalama na kesi yake imeahirishwa hadi tarehe 12 mwezi wa Disemba.
Seif al-Islam pia alikuwa anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya Tripoli kwa ajili ya kutajwa kwa kesi yake ya mashtaka ya usalama kuhusiana na uasi wa mwaka 2011 uliompinduwa baba yake lakini kuna wasi wasi iwapo waasi wa zamani waliomteka na kumshikilia huko Zintan watakubali kumpeleka Tripoli.
Mwendesha mashtaka wa Libya Abdulqader Radwan hapo Jumatano aliamuru Seif al -Islam ahamishiwe katika mahakama ya Tripoli kutoka ya Zintan ilioko kilomita 180 kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Mrithi huyo wa zamani wa uongozi wa Gaddafi na washtakiwa wengine zaidi ya 30 akiwemo kiongozi wa zamani wa ujasusi Abdullah al Senussi wanashtakiwa kwa madai ya uhalifu waliofanya wakati wa uasi wa mwaka 2011 uliomn'gowa madarakani Gaddafi.
Kesi muhimu katika historia ya Libya
Baghdadi al -Mahmudi waziri mkuu wa mwisho katika kipindi cha Gaddafi na Mansur Daw ambaye alikuwa akiiongoza Kikosi cha Ulinzi cha Wananchi pia ni miongoni mwa washtakiwa katika mojawapo ya kesi muhimu kabisa ya kisheria katika histroria ya Libya.
Mwendesha mashtaka wa Libya Radwan ameuambia mkutano wa wandishi wa habari kwamba wametuma agizo la kuhamisha kesi hiyo katika mahakama ya Tripoli kwa mamlaka zinazoshugulikia watu wanaohusishwa na kesi nambari 630 akiwemo Sef al-Islam.Inaripotiwa kwamba mazungumzo yalifanyika hadi usiku wa manane hapo jana kwa ajili ya kumhamisha Seif mjini Tripoli kwa masaa kadhaa.Duru zilizo karibu na kesi hiyo zimesema suala hilo litategemea zaidi hali ya usalama.
Mashtaka makuu yanayowakabili watuhumiwa ni pamoja na mauaji yaliofanyika wakati serikali ilipokuwa ikipambana na uasi ambao ulizuka katika mji wa mashariki wa Benghazi hapo mwezi wa Februari mwaka 2011.
Seif al-Islam yuko mikononi mwa serikali
Gaddafi alitekwa na kuuwawa na waasi katika mji alikozaliwa wa Sirte mwezi wa Oktoba mwaka huo.
Mtoto wake huyo wa kiume alitekwa mwezi uliofuatia na kundi la waasi wa zamani kutoka eneo la milimani la Zintan na amekuwa akishikiliwa huko tokea wakati huo.Serikali ya sasa ya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini ilijaribu mara kadhaa kutaka kuhamishiwa Tripoli kwa mtoto huyo wa Gaddafi bila ya mafanikio.
Hata hivyo serikali hiyo imekuwa ikisisitiza kwamba Seif al-Islam anashikiliwa na serikali.
Wakati huo huo shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu Amnesty International limetaka kukabidhiwa haraka kwa Seif al Islam na Senussi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Shirika hilo limesema mfumo wa mahakama nchini Libya unatakiwa kufanyiwa mageuzi makubwa na kuna wasi wasi mkubwa juu ya uwezo wa serikali kuhakikisha kesi zinafanyika kwa haki kutokana na kuwepo kwa hali mbaya ya usalama nchini humo.
Jumla ya nyaraka 40,000 na kurasa 4,000 za maelezo ya usaili zitazingatiwa na mahakama ambayo itasikiliza kesi hiyo katika eneo la siri katika mji mkuu wa Libya.
Iwapo watuhumiwa watapatikana na hatia wanaweza kuhukumiwa adhabu ya kifo.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Josephat Charo
Chanzo:- dw.de
No comments:
Post a Comment