OKTOBA 5 -9 mwaka huu tumeshuhudia msuguano mkubwa kati ya wafanyabiashara ya usafirishaji na Wizara ya Ujenzi chini ya Waziri Dk. John Magufuli.
Msuguano huu ulisababisha adha kubwa kwa abiria toka mikoani na hata kulala kwenye mabasi Kibaha baada ya kushindwa kufika Ubungo.
Malori yaliegeshwa barabarani kwa kisingizio kwamba wanadaiwa tozo ya asilimia 5 wakizidisha uzito.
Kwa barabara na madaraja kuna kiwango chake cha kubeba mizigo. Kila nchi ina viwango vyake kutokana na barabara ilivyotengenezwa. Kwa mfano nchi zote zilizo chini ya Umoja wa Ulaya uzito wa mwisho ni tani 44, zaidi ya hapo gari halipaswi kupita. Uingereza ni tani 44, Ujerumani na Ufaransa (40). Marekani na Urusi (36), Uganda na Kenya (54) wakati Tanzania ni tani 56. Zaidi ya hapa msafirishaji anapaswa kupata kibali.
Barabara hizi pia zinaishi kama binadamu (Life Span), zina makadirio ya miaka, mfano barabara za Uingereza, ‘Life Span’ yake ni miaka 60 wakati za Tanzania ni miaka 20. Hii inatokana na teknolojia iliyotumika kujenga barabara hizo.
Ili kudhibiti na kulinda uhai wa barabara hizi kila nchi imeweka mizani ili kudhibiti uzito kwa lengo la kulinda uhai wa barabara.
Marekani kila baada ya kilometa moja kuna mizani, kwetu sisi ni baada ya kilomita 10 au zaidi ndiyo unakutana na mizani nyingine.
Mvutano wa sasa unatokana na sheria zilizopitishwa na Bunge kuanzia mwaka 1970, sheria 30; na sheria mpya ya usalama barabarani ya 2002. Umeanza wakati Waziri Magufuli anapotaka sheria mpya ifanye kazi. Msafirishaji anaona inamdhibiti asibebe mizigo kuzidi uzito uliokubaliwa kisheria.
Mfanyabiashara atajitahidi akwepe ushuru bandarini na atataka aachiwe abeba tani zozote pasipo kuzuiliwa. Ni yeye anayepata faida na si serikali.
Tukiangalia kwa umbali wa mita moja, tunaona serikali kwa muda huu inakosa mapato, lakini kama tutakuwa na uwezo wa kufanya akili zetu zione zaidi ya kilometa 100 na miaka 50 ijayo tusingelalamika kwa kukosa mapato kutokana na kuzidisha uzito kwa wasafirishaji.
Madai ya wasafirishaji ni kwamba wanapima katika mizani moja na wakifika kwenye nyingine uzito unabadilika, kwa madai ya kwamba mizigo inahama, ni sawa.
Lakini kwa upande mwingine tusisahau katikati ya mizani moja hadi nyingine, mfanyabiashara huyu anaweza akabeba mizigo mingine, hivyo ni wazi uzito utakuwa umeongezeka. Hili hatulioni na tunang’ang’ania tu kuwa mizigo inahama.
Kuna wasafirishaji wengine kama Tanzania Breweries, Coca Cola, Abood Bus Service, Dar Express, mbona inaonyesha usafirishaji wao hauvuki kiwango cha uzito kilichowekwa? Mbona wao ni waelewa!
Wasafirishaji wanaokiuka utaratibu huu na waliozoea kutoa chochote kwa watu wa mizani ndio wanaopata shida kwani Wizara ya Ujenzi kwa sasa imebadilisha wafanyakazi wake wa kwenye mizani.
Wasafirishaji wanapofika kwenye mizani hizo kama baadhi yao walivyozoea kutoa ‘kitu kidogo’, mpimaji anapokataa kupokea kitu kidogo, hapa ndipo mgogoro unapoanza.
Mimi ni padre, naishi katika jamii na nina jamaa zangu ambao wamefukuzwa kazi Wizara ya Ujenzi, walikuwa kwenye mizani.
Katika kusukuma gurudumu la maendeleo, serikali ina namna nyingi ya kufanya kazi; kwanza, ni serikali yenyewe, pili, sekta binafsi, ambayo mwishoni mwa mwaka 1980 na mwanzoni mwa 1990 - ilipigiwa debe sana na Margaret Thatcher (apumzike kwa amani) na Regan – Thatcherism na Reganism – kwamba serikali pekee haipaswi kuwa mtoaji na mhimili wa huduma za jamii. Hivyo, sekta binafsi zihusike katika kuisaidia serikali katika kutoa huduma za jamii, serikali hata hivyo inabaki mkono wa kuume katika kutoa huduma za kijamii.
Kwa kifupi falsafa hii ya akina Thatcher na Regan iliaminika kama ndiyo mkombozi kwa matatizo ya kimaendeleo na kiuchumi kwa nchi za dunia ya tatu.
Kwa bahati mbaya huku kwetu falsafa hii ni butu kwani ufisadi umefungamanishwa kapu moja na utawala bora.
Sekta binafsi zimepewa kipaumbele, zama za soko huria zikashika kasi, milango ya wawekezaji wa nje na ndani ikafunguliwa kwa fujo.
Katika kutekeleza mawazo ya akina Thatcher – tukaja na sera za ‘Ruksa’ – “kila kitu ruksa” – kwa kuitafasiri kwa lugha ya kiuchumi ni ‘Ruksagonomics’ – msome Nkwazi Mihango katika makala yake; ‘Ours is egomaniacs instead of Economics’ ( THISDAY, October, 7-13, 2013, uk.7).
Kwa falsafa hii ya akina Thatcher, ni kwamba serikali ihusike zaidi katika kutunga na kusimamia sera.
Tatu, muungano wa sekta binafsi na serikali katika kutoa huduma; muungano huu huitwa PPP (Public Private Partnership) ni ubia wa serikali na sekta binafsi katika kutoa huduma za jamii. Mgawanyo wote huu ni kwa ajili ya faida kwa umma.
Kuna aina nyingine ya nne ya ubia usio rasmi, ambao ni ule wa wakubwa kuungana na wafanyabiashara katika kufanya biashara zao si kwa faida ya umma bali kwa kiongozi na mfanyabiashara; faida ya ubia huu haiendi serikalini au kwa umma.
Ubia huu kati ya kigogo na mfanyabiashara ambao naweza kuuita, ‘Kigogo –Businessman Partnership’. Ndio unaouua nchi hii.
Kupitia ubia huu, mfanyabiashara ndio mnufaika zaidi. Kwanza anajua siri zote za serikali mapema zaidi hata kama zabuni haijawekwa hadharani.
Pili, kigogo huyo kupitia ubia huu wa ‘Kigogo –Businessman Partnership’ atafundishwa hata namna ya kukwepa kodi.
Tatu, kigogo atamuunganisha mfanyabiashara huyo na vigogo wengine wa serikali kuhakikisha zabuni anashinda na kazi atafanya hata si katika ufanisi.
Mahatima Gandhi alizoea kusema kuwa; kwenye dunia hii tunavyo vya kutosha kukidhi mahitaji yetu. Lakini hakitoshi kukidhi ulafi wetu.”
Tajudeen Abdul–Raheem (aliyefariki 2009 jijini Nairobi, Kenya) – aliyekuwa mwanamapinduzi mwenye kupigania Mwafrika na Uafrika – Panafricanism; aliona viongozi hawa wasioridhika – wala rushwa - ni kama wauuaji wa umma.
Mwanamapinduzi huyu aliendelea kusema kwa tafsiri isiyo rasmi; “Ni wazi ni wauuaji wa umma, wanaua mamilioni ya watu…fedha zinazotolewa kwa ajili ya dawa, hospitali, shule zinanyonywa, walioduni kufa mapema na kufanya jamii zetu kuwa sizizo na usalama.” (Tajudeen Abudul-Raheen; kwenye kitabu chache kiitwacho, Speaking Truth to Power -2010).
Ni mioyo milafi inayofanya viongozi waingie katika ‘Kigogo –Businessman Partnership’ na matokeo yake tumeshindwa hata kuifufua reli ya kati. Wanajua wazi kuwa reli ya kati ikifanya kazi wengi watakwama kibiashara.
Sipingi juhudi zinazofanywa na Waziri Mwakyembe katika kuboresha reli na bandari. Lakini mabadiliko yanapokelewa katika mitizamo yote miwili, yaani hasi na chanya. Mfano mzuri ni ule wa kubadilisha Bodi ya Bandari uliozua miguno mingi! Wenyeji wanahoji, hawa wapya wataboresha au ni mfumo tu umewaleta? Wenyeji wamesahau kuwa ni ‘divai mpya katika kiliba kipya’.
Nakumbuka mwandishi mmoja, Robert Chambers katika vitabu vyake vya maendeleo; kimoja kinasema ‘Whose Change?’ -Mabadiliko ni kwa Nani?/Mabadiliko ni kwa Manufaa ya Nani?
Hivyo basi, Mwakyembe kama wafanyakazi wa bandari na reli wanavyomwita; ni ‘Good Fighter’, anampigania nani? Ni kwa ajili ya kundi dogo au umma? Vita yake ni kweli inalenga kuleta mageuzi ya kweli, akienda vizuri ni mpiganaji wa umma akikosea stepu watu wa bandarini wataendelea kumwita ‘Trumpet Brower’ - yaani mpiga filimbi tu.
Dk. Mwakyembe haya ni maneno tu ya watu wa bandarini, ni watu ambao wamepokea mabadiliko katika mrengo hasi.
Usafiri wa reli ukiimarika utakuwa na faida kubwa kwa serikali na kwa wananchi pia, bei ya bidhaa inayosafirishwa kwa treni ina nafuu kwa mlaji.
Tatizo la msongamano wa malori ya mizigo katika barabara halitaisha hadi reli ya kati ifanye kazi kwa ufanisi.
Rais Chiluba wa Zambia (1991-2001), alipoingia madarakani alimwandama sana mtangulizi wake Keneth Kaunda, lakini na yeye katika utawala wake aligubikwa na kashfa nyingi zikiwemo za matumizi mabaya ya rasilimali ya Wazambia, kashfa kubwa ni kujiingiza katika biashara ya kuwa ‘transpota’.
Si rahisi kwa raia kusini mwa Jangwa la Sahara kumwambia rais wao kuwa ni mwizi; lakini Wazambia walidiriki kumwambia na vyombo vya habari hasa magazeti yakaandika kabisa kuwa ‘Chiluba ni jambazi/jangiri, Chiluba ni mwizi’.
Viongozi wakae pamoja wafufue reli. Reli ikifanya kazi vizuri malori ya mizigo yatapungua barabarani.
Maendeleo hayaletwi na wizara moja bali ni mjumuisho wa wizara mbalimbali katika utofauti ambao unalenga ufanisi mmoja. Viongozi wetu waisome vizuri Dira ya Maendeleo 2025.
Chanzo:- Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment