Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema nchi yake na Marekani zinakubaliana juu ya namna ya kuharibu silaha za kemikali za Syria, na kuusifia utawala wa rais Assad kwa kutoa ushirikiano.
Rais Putin aliyasema hayo siku ya Jumanne, baada ya kukutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry nchini Indonesia, na kuongeza kuwa Urusi inaweza kukaribisha wazo la Indonesia kushiriki mazungumzo ya amani ya Syria, yaliyopangwa kufanyika mjini Geneva baadae mwaka huu.
Rais huyo wa Urusi aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa mkutano wa ushirikiano wa kiuchumi wa mataifa ya Asia na Pacific uliofanyika katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia, kuwa Urusi na Marekani zina uelewa sawa juu ya nini kinahitaji kufanyika na vipi, na kusema kuwa anafurahi kuwa rais Barack Obama alichukua msimamo huo kuhusu silaha za kemikali.
Putin alisema kuwa serikali ya Syria ilikuwa inatoa ushirikiano kamili kwa wakaguzi wa Umoja wa Mataifa, na kupendekeza Indonesia ijiunge na mazungumzo ya amani juu ya mgogoro wa nchi hiyo. Alisema kuwa wanaamini inawezekana kuongeza idadi ya washiriki wa mazungumzo hayo ya amani kwa kuyaongeza mataifa yenye idadi kubwa ya Waislamu kama vile Indonesia.
Zoezi kudumu mwaka moja
Wataalamu wa kimataifa walio na jukumu la kuanza mchakato wa kuhakiki na kuharibu silaha za kemikali waliwasili nchini Syria mapema mwezi huu, na Urusi, amabyo ni mshirika wa muda mrefu na muuzaji wa silaha kwa utawala mjini Damascus, iliahidi kusaidia katika mchakato wa kuharibu silaha hizo. Putin alisema anaamini wataalamu kutoka shirika la kuzuiwa matumizi ya silaha za kemikali OPCW, wataweza kufikia lengo lao la kuharibu silaha za kemikali za Syria ndani ya mwaka mmoja.
Timu hiyo ya wataalamu, ikisaidiwa na Umoja wa Mataifa, inalenga kusimamia zoezi la kuharibu mitambo ya kutengeneza silaha za kemikali nchini Syria ifikapo Novemba Mosi, na kuanza kushughulikia silaha za kemikali hadi kufikia Juni 2014. Putin aliisifu Syria kwa ushirikiano wake juu ya mpango huo, ambao ulifikiwa kati ya Marekani na Urusi mwezi uliyopita, baada ya Marekani kutishia kuishambulia Syria.
Awamu tatu
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha mpango huo mwezi uliyopita, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alipendekeza kwa baraza hilo jana Jumatatu, kuundwa kwa timu ya wataalamu 100 kusimamia zoezi hilo, na kuongeza kuwa wataalamu hao watahitaji msaada kutoka kwa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Katika barua aliyoituma kwa baraza hilo lenye wanachama 15, Ban alisema zoezi la kuharibu silaha hizo litafanyika kwa awamu tatu -ya kwanza ambayo tayari imekwishaanza, ya pili ambayo itahusisha kuharibu silaha za kemikali na mitambo ya kuchanganya, na awamu ya tatu ambamo ufutaji wa programu hiyo utahakikiwa na kufuatiliwa.
Chanzo;- dw.de
No comments:
Post a Comment