Social Icons

Thursday, 10 October 2013

VYOMBO VYA HABARI TANZANIA KUTOWAANDIKA DR. MUKANGARA NA MWAMBENE.


Dar es Salaam. Wadau wa habari nchini wametangaza msimamo wa kutotangaza wala kuandika habari zinazomhusu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo), Assah Mwambene kama sehemu ya kupinga mwenendo wa serikali wa kuvifungia vyombo vya habari.

Wadau hao kutoka taasisi mbalimbali za habari wamesema kuwa pamoja na kilio cha muda mrefu cha kuitaka serikali kufuta Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, lakini hakuna jambo lolote lililofanyika mbali ya kuendelea kuviandama vyombo hivyo.

Katika taarifa yao, wadau hao wamesema pia wamesikitishwa na tabia iliyoonyeshwa na Dk Mukangara na Mwambene kuchukua uamuzi wa kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania bila kuyasikiliza na kupotosha umma juu ya jambo hilo.

“Kwa msingi huo, wadau tumeamua kwamba tutasitisha kuandika, kutangaza na kupiga picha shughuli zozote zitakazowahusisha au kuratibiwa na Dk Mukangara na Mwambene hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo. Adhabu hiyo inaanza mara moja kuanzia leo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha taarifa ya wadau hao imesema kuwa wataendelea kupinga Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo kuongeza nguvu ya kisheria mahakamani kwenye kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd, mwaka 2009 inayopinga sheria hiyo.

Taasisi zilizoshiriki kwenye uamuzi huo ni pamoja na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat), Jukwaa la Wahariri (TEF), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika-tawi la Tanzania (Misa-Tan) na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Nyingine ni Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Klabu ya Waandishi wa Habari ya Dar es Salaam (DCPC) na Tanzania Human Rights Defenders (THRDC).

Chanzo:- Mwananchi.

 


No comments:

 
 
Blogger Templates