ALIYEKUWA Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, marehemu Dk. Sengondo Mvungi anadaiwa aliajiri mtu aliyekuwa akishiriki matukio mengi ya ujambazi kuwa mlinzi wa nyumbani kwake bila mwenyewe kutambua. Siri hiyo ilibainika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wakati wanaotuhumiwa wa wanaodaiwa kumuua Dk. Mvungi walipopandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji ya kukusudia.
“Huyu masai, Longishu Losingo (29) ni jambazi wa siku nyingi alikuwa na kesi ya wizi wa gari katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, akahukumiwa kwenda jela miaka saba.
“Wewe si ulifungwa miaka saba wewe, mimi mwenyewe nilikuwa nakutoa mahabusu kukupeleka mahakamani, umekwenda kwa Dk. Mvungi ukajifanya unaomba kazi ya ulinzi, mkamuua bure baba wa watu, mwangalie kwanza … sasa hivi umejitambulisha kwa jina gani,”alidai polisi PC Christopher.
Masai akijibu alisema: “nimejitambulisha kwa jina la Longishu”.
“Hawa wote majambazi, wewe Ngosha mzoefu, Makenza ulikuwa jela kwa ujambazi… katika hawa hakuna hata jambazi mgeni wote wakazi wa Gerezani, wanatoka wanarudia kufanya matukio.
“Huyu Makenza alikuwa na kesi katika Mahakama ya Samora, ukiwaona hapa wapole kama siyo wao, wameiba wakakimbilia kununua raba mpya,”hayo yote yalikuwa maneno ya polisi na askari Magereza waliokuwa wamewazunguka watuhumiwa hao nje ya mahakama.
Washtakiwa hao, walifikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye silaha na rungu kubwa lililokuwa na maandishi ‘Mama mkanye mwanao,’ huku juu ya gari walimokuwamo kukiwa na machela ya kubebea wagonjwa.
Wakili wa Serikali, Aida Kisumo aliwasomea washtakiwa hao mashtaka ya mauaji ya kukusudia mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo.
Aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Chibago Magozi maarufu Chiligati (32), mkazi wa Vingunguti, John Mayunga maarufu Ngosha (56) mkazi wa Kiwalani aliyekutwa na bastola ya Dk. Mvungi.
Wengine ni Juma Kangungu (29) mkazi wa Vingunguti, Longishu Losingo (29), aliyekuwa mlinzi wa marehemu na mkazi wa Kariakoo, Masunga Makenza (40), mkazi wa Kitunda, Paulo Mdonondo (30) mkazi wa Tabata Darajani, Mianda Mlewa maarufu White (40), mkazi wa Vingunguti Shule ya Tapa, Zacharia Msese (33) mkazi wa Buguruni Ghana kwa Hawa Masudi, Msigwa Matonya (30) kazi wa Vingunguti Machinjioni na Ahmad Kitabu (30) Mkazi wa Kinondoni, Mwananyamala.
Chanzo:- Mtanzania
No comments:
Post a Comment