Social Icons

Tuesday, 12 November 2013

DR. MWAKYEMBE APIMWA UBAVU

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameingia katika mzani wa kupimwa ubavu na uongozi wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) ambao unasuasua kutekeleza agizo lake la kumtaka Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Ronald Phiri, kutoendelea kuishi hotelini na badala yake apewe nyumba ya kuishi ili kukwepa gharama.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Ronald Phiri, kwa takriban miezi 6 sasa anatajwa kuishi katika Hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam kwa gharama ya shirika hilo na hivyo kuteketeza mamilioni ya shilingi.

New Africa HotelHabari zilizopatikana kutoka Ofisi za Makao Makuu ya TAZARA, Dar es Salaam, zinadai kwamba Khiri amekuwa akilipia chumba anachokitumia kulala katika hoteli hiyo dola za Marekani 200 (takriban Sh 320,000) kwa siku, sawa na takriban Sh. 9,600,000 kwa mwezi. Kwa hesabu hiyo, kwa miezi hiyo sita ambayo Khiri ameishi hotelini hapo, TAZARA italipa Sh. 57,600,000.

Hasara yote hiyo kwa shirika la TAZARA inaingiwa wakati Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amemwagiza Kaimu Mkurugenzi huyo kuhamia katika nyumba ya TAZARA iliyoko Masaki, ambayo ilikuwa ikitumiwa na mtangulizi wake, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Akashambatwa Lewanika.

Lewanika alistaafu ajira yake mwanzoni mwa mwaka huu na kurejea nchini kwao Zambia, kabla ya Bodi ya TAZARA kumteua Khiri kukaimu nafasi hiyo.

Akizungumza na wafanyakazi wa TAZARA Oktoba 21, mwaka huu, Dk Mwakyembe alimpa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo, Khiri, muda wa wiki mbili kuondoka hotelini hapo na kuhamia katika nyumba ya shirika.

Mmoja wa wafanyakazi wa TAZARA ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia gazeti hili akisema: “Unajua mpango wa kumweka hotelini (Phiri) ulikuwa ni wa muda wa miezi mitatu tu, lakini kama ujuavyo gharama za kuishi hotelini pale ni dola za Marekani 200 kwa siku.

Kwa hiyo, miezi mitatu imepita na sasa ni miezi zaidi ya sita.”

Akizungumzia hali hiyo ya kuendelea kuishi hotelini hapo kinyume cha maelekezo ya Waziri Mwakyembe, Kaimu Mkurugenzi huyo wa TAZARA anasema hata yeye hajisikii raha kuishi hoteli hiyo ya New Africa, akisema hali hiyo inamsababishia kuishi mbali na familia yake.


Chanzo:- Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates