Social Icons

Thursday, 7 November 2013

FAHAMU RISASI KATIKA RANGI NA ATHARI ZAKE

RISASI ni madini ya chuma yenye rangi ya kijivu, ambayo hupatikana ardhini kwenye tabaka la dunia.

Awali kabla ya kuelewa athari za afya zitokanazo na madini ya risasi, madini haya yalitumika kwa wingi kwenye bidhaa mbalimbali kama vile petroli, betri, bidhaa za chuma, mawe ya vioo, makopo au vyombo vya kuhifadhia chakula, ndoana na risasi za bunduki au bastola.

Kwanini risasi katika rangi?

Katibu Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Agenda, Silvani Mng’anya, anasema kuwa rangi zinazokuwa na risasi ni zile ambazo risasi imeongezwa na kuchanganywa kwa ajili ya kuifanya ikauke mapema baada ya kupaka, pia kuleta ung’avu mzuri wa rangi husika.

Anasema risasi hulinda ubora wa rangi kwa muda mrefu na kuzuia unyevunyevu unaosababisha kumomonyoka kwa kifaa kilichopakwa rangi.

Wakati mwingine kiasi kidogo cha risasi chaweza kuwepo katika malighafi iliyotumika kutengenezea rangi.

Mng’anya anasema nchi zinazoongeza risasi katika rangi ni zile zinazoendelea kiuchumi kama Tanzania, Afrika Kusini, Nigeria, Senegal, India na nyingine nyingi.

Mwaka 2009 utafiti wa rangi zenye risasi duniani ulifanywa na asasi ya Wanachama wa Mtandao wa Kuondoa Kemikali Zisizooza Duniani (IPEN), zikiongozwa na asasi ya Toxics Link ya India na asasi zisizo za serikali katika nchi husika.

Asasi ya Agenda ni miongoni mwa asasi zilizoshiriki katika utafiti  huo ambapo kati ya sampuli 20 za rangi za mafuta  zilizokusanywa kutoka kwenye rangi zinazouzwa Tanzania, rangi 19 zilikutwa na risasi zaidi ya kiwango,  450.

Sheria za Tanzania zinasemaje?

Katika tafiti za mwaka 2009 na 2012 zilizingatia kuwapo kwa  kiwango cha hiari kilichowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambacho kinataka kiwango cha risasi katika rangi kisizidi 450 ppm au 0.045.

Sheria ya Kemikali za Viwandani namba 3 ya mwaka 2003 kifungu cha 30 (1) inaunga mkono ukatazaji, uzuiaji na uondoaji wa kemikali zote zilizothibitika kuwa hatarishi na ni sumu kwa afya ya binadamu na  mazingira.

Ukiacha sheria tajwa hapo juu, hakuna sheria rasmi ya matumizi ya risasi katika rangi nchini Tanzania.  

Kuna sheria ya rangi zenye risasi nchi nyingine?        

Nchi nyingi zinazoendelea na nchi zenye uchumi unaokua hazina sheria na kanuni za viwango vya risasi kwenye rangi.

Baadhi ya nchi zina viwango vya hiari tu juu ya kiasi cha risasi kwenye rangi.

Risasi ni sumu, huingia mwilini kwa binadamu kwa kiasi kikubwa kupitia  mfumo wa uvutaji hewa, kwa njia ya mdomo au kiasi kupitia njia ya ngozi.

Risasi kama yalivyo madini mengine kama chuma, zinki na kalisi zina tabia ya kuunganika na mfumo wa kibailojia ndani ya mwili wa binadamu.

Risasi husababisha athari inapojikusanya sehemu yoyote katika mwili.  Kwa mfano katika mishipa ya damu risasi inaathiri chembe hai nyekundu za damu na kuzuia uwezo wake wa kusafirisha oksijeni kwenda sehemu mbalimbali za mwili.

Risasi huishia kwenye mifupa ambapo huingilia uzalishaji wa chembe hai za damu na kuzuia ufyonzwaji wa  madini ya kalisi yanayosaidia ukuaji mzuri wa mifupa.

Watu gani wanaathiriwa zaidi na risasi? 

Watoto wadogo ambao miili yao inakua inanyonya risasi kirahisi zaidi kulinganisha na watu wazima. Kiwango kidogo tu cha risasi kinaathiri ukuaji wao wa akili, uelewa wa mambo, ukuaji wa mwili na tabia.

Katika kipindi cha ujauzito, hususan katika kipindi cha mwisho, risasi inaweza kupenya kwenye mji wa uzazi na kumwathiri mtoto aliyeko tumboni.

Wanawake wafanyao kazi katika mazingira hatarishi yenye risasi wapo katika hatari ya kuharibika kwa mimba na watoto kuzaliwa kabla ya  wakati wake.

Wapakaji rangi, wanaokarabati nyumba au vifaa vyenye risasi, viwanda vya kutakatisha metali (chuma) na wahunzi wapo katika hatari kubwa ya kuathiriwa na risasi.

Dalili ya aliyeathiriwa na risasi

Mng’anya anasema kwa kawaida hakuna dalili za moja kwa moja za mtu aliyeathiriwa na risasi. Watoto wenye kiwango kikubwa cha risasi kwenye miili yao wanaweza kusikia maumivu ya tumbo au kupoteza hamu ya kula, kuhangaika, kutokulala au kuwa na hasira.

Mara nyingi athari za kiafya zitokanazo na sumu ya risasi huchanganywa na dalili za magonjwa mengine kama kifua cha baridi na mafua. Dalili nyingine zinaweza zikaanza kama kutapika, wazimu na hatimaye kusababisha kifo.

Anasema kiwango cha sumu ya risasi mwilini huchunguzwa tu kwa kupima damu. Daktari anachukua sampuli ya damu ya mtoto.

Sampuli hiyo hupelekwa kwenye maabara na kufanyiwa uchunguzi kubaini kiwango cha risasi kilichopo kwenye damu na kutoa ushauri juu ya nini kifanyike kama kuna ulazima.

Uelewa kuhusu rangi zenye risasi

Taasisi nyingi za serikali kama vile wizara, idara, wakala za serikali na viongozi wataalamu wa viwanda wana ufahamu kuwa baadhi ya rangi zina risasi.

Hata hivyo, wasambazaji, wauzaji na wapaka rangi hawana ufahamu wa kutosha juu ya rangi zenye risasi na athari zake kwa afya.

Juhudi za kupunguza madhara ya risasi

Matumizi ya risasi katika rangi na katika uzalishaji mwingine yalizuiwa Amerika ya Kaskazini, Ulaya Magharibi, Asia na Afrika takriban miaka 70 iliyopita.

Akitolea mfano Mng’anya anasema risasi imeondolewa kutumika katika mafuta ya petroli nchi nyingi, uondoaji huo ulifanyika taratibu kwa kipindi kirefu.

Katika mkutano wa pili wa kimataifa wa usimamizi wa kemikali (ICCM2) uliofanyika Geneva kuanzia  Mei 11 hadi 15, 2009 uliidhinisha mapendekezo ya asasi ya Toxics Link na mwanachama IPEN India, kuanzisha ushirikiano wa kimataifa wa wadau wa kuondoa matumizi ya risasi katika rangi kama mchango muhimu katika kutekeleza aya ya 57 ya Mpango wa Utekelezaji wa Mkutano wa Dunia wa Maendeleo Endelevu (WSSD) na Mkakati wa Kimataifa wa Usimamizi wa Kemikali (SAICM).

Lengo kuu la ushirikiano huo unaoitwa Ushirika wa kidunia katika kuondoa rangi zenye risasi (GAELP) ni kuwalinda watoto kutokana na athari za rangi zenye risasi na kupunguza athari za risasi kwa wafanyakazi walio katika mazingira hatarishi.

Lengo jingine ni kuondoa kabisa uzalishaji, uuzaji na matumizi ya rangi zenye risasi na hatimaye kuondokana na athari za rangi hizo.

Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kutumia mamlaka na rasilimali zake zinaunda Sekretarieti ya Ushirika wa GAELP.

Tutapunguzaje athari za risasi katika rangi?

Mng’anya anasema ni vema kusafisha vumbi na vipande vya rangi vinavyodondoka na kuchakaa kwa kutumia maji.

Pia inapaswa kuwalisha watoto chakula chenye virutubisho vikiwamo vya madini ya chuma, kalisi, vitamini C na vyenye kiwango kidogo cha mafuta.

Anasema watoto wapewe chakula chenye virutubisho kama matunda ili waepuke kutia vitu vingine tofauti na chakula kwenye vinywa vyao.

Ni vema kuhakikisha watoto na wajawazito hawaingii eneo la kazi lenye mazingira hatarishi ya uwepo wa risasi hadi ukarabati utakapomalizika na kusafishwa vizuri.

Kingine ni kusafisha mikono ya mtoto, mdomo na uso pamoja na vitu vya kuchezea (midoli) mara kwa mara.

Kutibu sumu itokanayo na risasi mwilini

Mng’anya anasema hakuna njia sahihi ya kutibu athari zitokanazo na sumu ya risasi ingawa katika hali ya hatari kwenye matabibu wanatumia dawa ya ‘chelaton’ kutibu watoto au watu wazima wenye kiwango kikubwa cha risasi kwenye damu.

Kwa kawaida dawa hii hutolewa hospitali kwa kuchoma sindano kwenye mishipa au kwa kumeza. Dawa hii inaungana na risasi kwenye damu na muunganiko huu hutolewa nje kwa njia ya mkojo.

Kama kiwango cha risasi ni kikubwa sana, tiba hutolewa kwa awamu mbili ili kupunguza kiwango cha risasi katika damu.

Pamoja na matibabu haya, risasi huchukua muda mrefu sana kutoka katika mwili na athari nyingine zinaweza kuwa za kudumu.

Chanzo:- Tanzania Daima


No comments:

 
 
Blogger Templates