Geita.Rais Jakaya Kikwete jana aligoma kupokea zawadi ya dhahabu kutoka Kampuni ya Nyamigogo Grand Vezir Holdings ya mkoani Geita.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema viongozi wa kampuni hiyo walitaka kumkabidhi Rais Kikwete gramu 227 za dhahabu safi wakati alipotembelea mgodi huo.
Rais Kikwete badala yake aliwaelekeza waiuze dhahabu na fedha zitakazopatikana zitumike kuwasaidia watoto yatima.
Alikabidhiwa zawadi hiyo wakati wa sherehe ya kuzindua mgodi wa uchenjuaji dhahabu wa kampuni hiyo nje kidogo ya mji mdogo wa Kharuma ambao ni makao makuu ya wilaya mpya ya Nyang’hwale, Geita.
Gramu hizo 227 zina thamani ya Sh16 milioni kwa bei ya sasa ya soko la dhahabu duniani.
Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Rais Kikwete aliuliza: “Sasa nifanye nini na zawadi hii? Nawarudishieni hii dhahabu, iuzeni popote mnakotaka na fedha itakayopatikana tutawapa watoto yatima.”
Akizungumza na wananchi katika mgodi huo, Rais Kikwete aliupongeza uongozi wa mgodi huo akisema umeongeza thamani ya dhahabu na maisha ya wananchi katika eneo hilo... “Mmefanya vizuri na mgodi huu, ni mradi wa maana kwa kuongeza thamani ya dhahabu na kuboresha maisha ya wananchi katika eneo hili. Ubunifu huu unastahili pongezi,” alisema Rais Kikwete.
Mgodi wa Nyamigogo ni wa marudio kwani unazalisha dhahabu kutokana na mchanga ambao awali ulishafuliwa na kutoa dhahabu. Ulianzishwa mwaka 2011 na mpaka sasa kiasi cha Sh 1.6 bilioni kimewekezwa kuuendeleza.
Uongozi wa mgodi huo ulisema mgodi huo unaozalisha kiasi cha gramu kati ya 500 na 600 kwa mwezi, na unaajiri watu 45 kati yao wanawake 10.
Rais Kikwete alizindua mgodi huo ikiwa sehemu ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika ziara yake Geita ambao ni moja ya mikoa minne aliyoianzisha mwaka jana. Mikoa mingine ni Simiyu, Njombe na Katavi.
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment