Social Icons

Sunday, 17 November 2013

KENYA YALAANI UAMUZI ULIOTOLEWA NA UN

Nairobi. Serikali ya Kenya imelaani uamuzi uliotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) wa kutupilia mbali ombi la Umoja wa Afrika (AU) kutaka kesi zinazowakabili viongozi wakuu wa nchi hiyo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) zisitishwe.

Katika kujadiliwa kwa suala hilo, nchi nane wanachama wa Baraza la Usalama la UN zikiwemo Uingereza, Ufaransa, Marekani, pia nchi wanachama wote wa ICC za Guatemala, Argentina, Australia, Luxembourg na Korea Kusini, zote zilijitoa na kukataa kushiriki kupiga kura hiyo zikidai kwamba siyo mahala pake.

Angalau kura takriban tisa zilihitajika ili kupita kwa azimio hilo lililotolewa na AU, lakini mkakati wa kura uliosimamiwa na kutekelezwa na Rwanda, Togo, Morocco, China, Urusi, Pakistan na Azerbaijan ndizo nchi zilizounga mkono azimio hilo lakini zilishindwa kulipitisha baada ya kutofikia kura tisa zilizohitajika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, muda mfupi baada ya kura za kuunga mkono ombi hilo juzi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imewatuhumu wanachama wa baraza hilo kwa kile ilichodai “kutokuwa makini katika masuala muhimu ya kidunia”.

Taarifa hiyo ya Kenya ilielekeza wazi lawama zake kwa Marekani na Uingereza kwa kutothamini nafasi ya Afrika na kutojali umuhimu wa amani na usalama.

Lawama hizo zilielekezwa kwa mataifa hayo, huku Kenya ikizisifu China na Azerbaijan (inayoshikilia uenyekiti kwa sasa) pamoja na Rwanda, Togo na Morocco- mataifa matatu ya Afrika katika baraza hilo la UN kwa kuonyesha uongozi bora.

Kwa uamuzi huo, ina maana kuwa hatima ya Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake, William Ruto iko mikononi mwa mkataba wa Roma unaoiunda ICC.

Marekani na Ufaransa zazungumza:

Katika msimamo wao, Marekani na Ufaransa zilieleza wazi kwamba ombi hilo la Afrika linatakiwa kufikishwa kwenye Mkutano Maalumu wa ICC unaowakutanisha nchi wanachama unaotarajiwa kufanyika mjini The Hague Jumatano ijayo.

Ilieleza kuwa, mkutano huo unatakiwa kuzingatia ubadilishaji wa taratibu zake ikiwemo kuwaruhusu watuhumiwa kusikiliza kesi zao kwa njia ya video, suala ambalo litarahishisha kesi hiyo dhidi ya viongozi hao wakuu wa Kenya.

Huku kesi ya Rais Kenyatta ikitarajiwa kuanza rasmi Februari mwakani, majaji wa Mahakama ya ICC wameamua rais huyo atahudhuria kikao cha kwanza na kile cha mwisho katika kesi hiyo na mashahidi ndiyo watakaohitajika kuwepo wakati mwingi.

Azimio hilo lililowasilishwa kwa Baraza la Usalama la UN, lilitaka kesi hiyo iahirishwe kwa mwaka mmoja ili kuzuia hofu ya kutokea ghasia nchini Kenya na hata vitisho vya ugaidi.

Chanzo:- Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates