Zanzibar.Vikosi vya Ulinzi na Usalama Zanzibar, vimekamata kontena la futi 40 likiwa limepakia meno ya tembo yaliyohifadhiwa kwenye mifuko ya nailoni yenye ujazo wa kilo 50, yakisafirishwa nje ya nchi.
Meno hayo yalikamatwa Bandari ya Malindi majira ya alasiri jana na polisi, Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Maofisa wa Usalama wa Taifa na raia wema waliotoa taarifa kuhusiana na mpango huo.
Akizungumza mjini hapa jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema uchunguzi wa tukio hilo umeanza ikiwamo kuwasaka wamiliki wa mzigo huo kupitia Kampuni ya Wakala wa Kusafirisha Mzigo, iliyopewa kazi hiyo.
Kamishna Mussa alisema kazi ya kupakua mzigo na kuchana gunia moja baada ya jingine tayari imeanza chini ya ulinzi mkali wa askari ili kujua idadi ya meno na thamani yake. Alisema mzigo huo ulikamatwa kupitia taarifa za siri zilizofanikisha kugundua kontena hilo lililokuwa na meno hayo yaliyochanganywa na kuwekwa katikati ya makombe (sea shells).
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alisema wakati umefika kwa Watanzania kushiriki na kuvikabili vitendo vya ujangili vyenye lengo la kuangamiza wanyamapori hasa Tembo na Faru.
Balozi Kagasheki alisema kazi inayofanywa na askari ni sehemu ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, huku akiwapongeza askari kwa kufanikisha jukumu lao.
Naye Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais (Idara Maalumu na Vikosi vya SMZ) Haji Omar Kheir alisema hakuna sheria za nyara za Serikali kutokana na visiwa hivyo kutokuwa na wanyamapori wa aina hiyo, lakini wahusika wanaweza kushtakiwa kwa kuhujumu uchumi ya Zanzibar iliopitishwa mwaka huu.
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment