BAADA ya kuilalamikia kwa muda mrefu Serikali ya Awamu ya Nne akidai viongozi wake wameshindwa kuchukua uamuzi mgumu, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amegeuka na kumsifu Rais Jakaya Kikwete, kuwa ndiye kiongozi ambaye ametekeleza Ilani ya CCM kwa kiwango kikubwa kuliko awamu nyingine.
Lowassa ambaye amekuwa akiandamwa na mahasimu wake kisiasa kutokana na kauli hizo za kubeza utendaji wa serikali, alitoa sifa hizo kwa Rais Kikwete jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara baada ya kuweka jike la msingi la ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Wilaya ya Monduli.
Alisema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa Ilani hiyo ya Uchaguzi ya CCM.
“Ndugu zangu Wana Monduli, huu ni uthibitisho wa utekelezaji wa hali ya juu wa Ilani ya Uchaguzi ya chama chetu, na ni lazima niseme wazi, hakuna kipindi ambacho ilani ya uchaguzi imetekelezwa kwa kiwango kikubwa kama awamu hii chini ya Rais Kikwete,” alisema.
Hospitali hiyo ambayo majengo yake yatakamilika Februari mwakani, itagharimu zaidi ya sh bilioni mbili na itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 72 katika wodi nne.
“Nilipotoa ahadi ya hospitali hii nilikuwa natoa ahadi ya Ilani ya CCM, kwa hiyo ipongezwe na Rais Kikwete kwa kusimamia kidete ilani yetu ya uchaguzi,” alisema Lowassa ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo.
Aliongeza kuwa hospitali hiyo itakuwa na vifaa vya kisasa na kuifanya kuwa moja ya hospitali bora nchini.
Lowassa alitoboa siri kwamba alimfuata Rais Kikwete kumuomba fedha kwa ajili ya mradi wa maji, ambapo alimwagiwa sh bilioni tatu.
“Jingine mlijue, Rais Kikwete nilimuomba fedha za mradi wa maji, akanipa bilioni tatu ziko tayari benki, hii yote ni kutimiza ilani ya chama, ndiyo maana nasema hakuna awamu ambayo imetekeleza ilani ya uchaguzi kwa asilimia kubwa kama hii yake,” alisema.
Lowassa pia alisema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kujenga nyumba takriban mia moja, ambapo kati ya hizo 50 ni za kupangisha na nyingine ni za kuuzwa.
Hivi karibuni Lowassa alirejea kauli yake bungeni akisema nchi inakosa viongozi jasiri wenye kusimamia utekelezaji wa mambo waliyoamua katika sekta mbalimbali.
Alisema nchi ina tatizo kubwa la uswahili mwingi wa kukaa kutekeleza kile kinachotakiwa kufanyika kiasi cha kusababisha kila mtu kuanza kulalamika.
“Hapa mnaamua bila kutekeleza, watu hawana ujasiri wa kufanya maamuzi magumu, ni lazima awepo mtu mmoja wa kuamua, si wote kulalamika lalamika.
“Tukishakubaliana mambo ni lazima yafanyike. Ni lazima tuondokane na kuwa nchi ya kulalamika kuanzia kiongozi wa juu mpaka mwananchi,” alisema.
Aliongeza kuwa kama angekuwa kiongozi wa serikali angejikita kwenye vipaumbele vitatu, ambavyo ni ajira, Reli ya Kati na elimu, kuliko kuwa na vipaumbele vingi visivyotekelezeka.
Chanzo:- Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment