Polisi wakikagua gari walilokuwa wakisafiria watu wanne kabla ya kupigwa risasi na mtu aliyejulikana kwa jina la Gabriel Munis na kuua watu wawili na kujeruhi wengine na baadaye kujiua,
Maeneo ya Bungoni na Amana, Ilala, jijini Dar es Salaam, jana yalikumbwa na mtikisiko mkubwa, baada ya mfanyabiashara wa mkoani Mwanza, Gabriel Munishi (30-35), kuwashambulia kwa risasi watu wanne, akiwamo mama na mabinti zake wawili, ambao mmoja aliuawa, kabla ya muuaji naye kujiua kwa risasi kutokana na kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.
Aliyeuawa amefahamika kuwa ni mfanyakazi wa Makao Makuu ya Benki ya Barclays, jijini Dar es Salaam, Alfa Alfred (34), ambaye ni mkazi wa Ilala.
Alfa anadaiwa kuwa ni mdogo wa mpenzi wa muuaji, Christina Alfred (35), ambaye alijeruhiwa kwa risasi kwenye paja la mguu wake wa kulia.Aidha, mama mzazi wa mabinti hao, Hellen Elieza (60-63), amejeruhiwa bega la kulia.
Pia Francis Mshumbira (41), ambaye ni raia wa Kenya, amejeruhiwa kichwani na kifuani.
Wote wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) isipokuwa Christina, ambaye alitibiwa katika Hospitali ya Amana na kuruhusiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Marietha Minangi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa lilitokana na wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 1:30 asubuhi wakati Hellen, Alfa na Francis, wakiwa kwenye gari dogo, wakitokea kwenye nyumba, iliyoko pembeni ya hoteli mpya ya M.M. Ltd iliyo jirani na baa maarufu kama “Klabu ya Wazee” eneo la Bungoni.
Gari hilo aina ya Toyota Surf, lilikuwa likiendeshwa na Francis, ambaye yeye pamoja na muuaji inadaiwa walikufa papo hapo katika eneo la tukio.
Taarifa kutoka eneo hilo zinaendelea kudai kuwa watu hao walikuwa wakienda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya kuwasindikiza baadhi yao waliokuwa wakisafiri kwenda nchini Cyprus.
Baadhi mashuhuda waliliambia NIPASHE kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio jana kuwa kabla ya Hellen, Alfa na Francis kutoka kwenye nyumba hiyo, muuaji alifika eneo hilo na kuwasubiri kwenye viti vya baa hiyo.
Mashuhuda hao ni pamoja na madereva teksi, waosha magari, wahudumu wa hoteli na baa hiyo, wafanyabiashara wa duka, majirani na wapita njia.
Tukio hilo lilizua taharuki kubwa miongoni mwa watu waliokuwa katika maeneo hayo wakati huo wakihofu kuvamiwa na majambazi baada ya milio kadhaa ya risasi kusikika kwa nyakati tofauti katika eneo hilo.
Hali hiyo ilisababisha shughuli mbalimbali zilizokuwa zimefunguliwa muda huo katika maeneo hayo, zikiwamo za duka na ofisi kusimama kwa muda.
Pia watu waliokuwa karibu na eneo hilo walikimbia hovyo na wengine waliokuwa kwenye magari, wakiwamo abiria wa daladala, kushuka na kuanza kutimua mbio.Baada ya hali kutulia, watu kutoka maeneo mbalimbali, walifurika katika eneo la tukio lililokuwa limetapakaa damu.
Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya wasamaria wema na madaktari wa Hospitali ya Amana, waliichukua miili ya marehemu na kuipakiza kwenye gari na kisha kuipeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.
Pia waliwachukua majeruhi, ambao baadhi walibebwa kwenye mkokoteni na kuwakimbiza katika hospitali hiyo kabla ya baadaye kuwapeleka MNH.
Dereva teksi wa kituo cha Bungoni, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini ndiye alikuwa shuhuda wa kwanza kushuhudia tukio hilo.
Alisema kabla ya tukio hilo, jana asubuhi alipata mteja (muuaji), ambaye alihitaji kupelekwa sehemu.
Lakini akasema kabla hawajafika alikokuwa akihitaji kupelekwa, jamaa huyo alimuomba akatishe safari na kumtaka ampeleke sehemu nyingine.Kwa mujibu wa dereva huyo, alimpeleka jamaa mpaka eneo la tukio.
“Mara baada ya kumfikisha hapo, jamaa alitoa Sh. 5,000 na kunikabidhi. Lakini cha kushangaza, ni kitendo cha jamaa huyo kutoa bastola wakati akiwa anaelekea kwenye geti la nyumba,” alisema dereva huyo.
Alisema wakati jamaa anaelekea getini, mlango ulifunguliwa na gari aina ya Toyota Surf lilitoka likiwa na watu wanne ndani, akiwamo mwanaume mmoja, ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha gari na mama mmoja na kina dada wawili.
“Jamaa akiwa na bastola alianza kuwashambulia watu waliokuwa ndani ya gari hilo na kumpiga risasi dereva na dada mmoja,” alisema dereva huyo na kuongeza kuwa mara baada ya kuona hivyo ilibidi akimbie.
Pia mmoja wa waosha magari katika baa hiyo, Juma Salum, ambaye alishuhudia tukio hilo, alisema alishuhudia jamaa akimpiga risasi ya mgongoni mama wa mfanyakazi wa benki aliyeuawa.
Alisema pia alishuhudia msichana mwingine akipigwa risasi ya mguuni baada ya kufungua geti na kutoka nje kisha jamaa akajipiga risasi chini ya kidevu na kujimaliza.
“Jamaa na dereva aliyekuwa akiendesha gari walifariki palepale,” alisema.
Hadi tunakwenda mitamboni, taarifa kutoka kwa Kamanda Minangi zilikuwa zinaeleza kuwa waliokufa katika tukio hilo ni watu wawili, ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Amana na kwamba, waliojeruhiwa ni watatu.
Alisema katika eneo la tukio, iliokotwa bastola moja na maganda 14 ya risasi, magazine mbili na risasi mbili.
Afisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Algaesha, jana alipotafutwa kuzungumzia hali za majeruhi, alisema alikuwa katika kikao.
Baadaye jioni Algaesha alielekeza atafutwe afisa mwingine aliyemtaja kwa jina la Jacqueline, ambaye hata hivyo, alipopigiwa simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa hadi tunakwenda mitamboni.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment