MWENYEKITI wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, amewataka Watanzania wasidanganywe na kauli za baadhi ya viongozi kuwa hawana mitaji ya kuwekeza wakati mtaji wao mkubwa ni rasilimali zao.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa shindano la ‘Twitte na Mengi’ linalofanyika kila mwisho wa mwezi, Mengi alisema mtaji mkubwa wa biashara yoyote si fedha mifukoni kama inavyofikiriwa bali ni maarifa na ubunifu wa wazo bora la biashara kichwani.
Bila kutaja majina, Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini, alisema wapo baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakiwabeza Watanzania kwamba hawana uwezo wa kujishughulisha na baishara kubwa na kwamba viongozi wa aina hiyo ni sawa na mwenye macho asiye na uwezo wa kuona na ana masikio lakini hasikii.
Ingawa hakutaja jina la kiongozi, lakini ni dhahiri kwamba Mengi alikuwa akimlenga Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospiter Muhongo, ambaye amekuwa akiwabeza Watanzania kuwa hawana uwezo wa kuwekeza kwenye sekta ya gesi.
Mengi alisema mawazo ya aina hiyo yanatokana na umaskini wa fikra na kusisitiza kuwa mtaji mkubwa wa Watanzania ni rasilimali zao.
Mengi alisema viongozi hao hawapaswi kuaminiwa kwa kuwa hawana nia njema na Watanzania na kueleza kuwa kila Mtanzania ana nafasi ya kuwa tajiri iwapo rasilimali zilizopo zitatumiwa kwa usawa na kuwajali Watanzania pia.
“Watanzania wasidanganyike eti hawana mtaji, mtaji mkubwa wa rasimali upo, na ni mtaji mkubwa sana wenye thamani kwa Watanzania, niwaambie Watanzania kuwa wasiwaamini viongozi wanaowaambia hawana uwezo wa kuwa matajiri ama kutajirika ama kunufaika na rasilimali, hilo linawezekana,” alisema Mengi.
Alisema inashangaza kuona kazi anayoweza kufanya mwenyeji, anapewa mgeni na kinachowaumiza Watanzania ni kutofahamu nini maana ya biashara na maana ya mtaji wa biashara, na kuongeza kuwa mawazo ya kiubunifu yanaweza kuwa mtaji tosha katika kufanikisha biashara.
Washindi wa shindano hilo na kiasi cha fedha walichozawadiwa kwenye mabano ni Suzana Senga (sh milioni moja), Pili Grace Mmasi (sh 500,000) na Victor Byemelwa (sh 300,000).
Katika shindano la mwezi huu, washiriki wanatakiwa kutwiti kwenye akaunti ya Mengi kujibu swali; “Ni kwa vipi Watanzania wanaweza kushiriki kuwekeza katika sekta ya gesi.”
Chanzo:- Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment