MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, amemsuta Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, akisema hana sifa za kuchukia rushwa ndani ya chama kwani wakati wa kipindi chake ilishamiri sana.
Mgeja ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, alisema kuwa mbali na kipindi cha Sumaye kushamiri mianya ya rushwa, lakini pia wakati huo ndio Tanzania ilifunga mikataba mingi mibovu yenye harufu ya rushwa inayopigiwa kelele na Watanzania wengi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kijijini kwake Nyanhembe, Kata ya Kilago wilayani Kahama, Mgeja alisema kuwa ameshangazwa na kauli ya Sumaye juzi ya kulalamikia kukithiri kwa rushwa sasa, akisema si kweli kwamba mwanasiasa huyo anaichukia rushwa bali anachokifanya kina lengo la kutaka kuwadanganya Watanzania.
Mgeja aliongeza kuwa wakati wa Sumaye, nchi ilifunga mikataba mingi mibovu katika sekta ya madini, viwanda, mashamba na ranchi za taifa ikiwemo uuzwaji wa Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) iliyouzwa kwa bei ya kutupa huku naye akijitwalia eneo kubwa la ardhi kule Kibaigwa mkoani Dodoma.
“Binafsi napingana na Sumaye katika hili, si kweli kwamba anachukizwa na tatizo la rushwa hapa nchini. Angekuwa na sifa hiyo basi wakati wa kipindi cha uongozi wake asingeruhusu nchi yetu kufunga mikataba mibovu, leo hii Watanzania wanalia kwa mikataba hiyo.
Mgeja alisema ni vizuri badala ya kuhangaika Sumaye angekaa chini na kutulia badala ya kuwakumbusha machungu aliyowasababishia wananchi wakati akiwa kiongozi mkuu wa shughuli za serikali.
Alisema badala ya kulalamika angesaidiana na serikali juu ya mbinu gani zitumike katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili Watanzania ili waweze kupata maisha bora wanayoyatarajia.
“Kwa kweli Sumaye hawezi kujigamba kwamba anachukia rushwa, kama kweli ana sifa hiyo, basi katika kipindi chake asingeruhusu mikataba mibovu ikiwemo ile ya Songas, IPTL, Meremeta, Mwananchi na wizi wa fedha za EPA, yote haya angezuia, aache kuwadanyanga Watanzania,” alisema Mgeja.
Alimuomba aache kuwanyooshea vidole wenzake na kwamba nguvu hiyo anaipata wapi au ana lengo la kufunika madhambi yake aliyoyafanya wakati akiwa waziri mkuu, na kwamba suala la rushwa hakuna Mtanzania anayeliunga mkono maana wote wanakerwa na vitendo hivyo.
Pia Mgeja alitoa mfano wa uamuzi mbaya uliofanyika kipindi cha uongozi wa Sumaye kwa kuamua kuuza nyumba za umma zilizojengwa kwa nguvu ya Watanzania wote wakiwemo wafugaji, wavuvi na wakulima ambao hawakushirikishwa katika kufikia uamuzi huo.
Alisema uingiaji wa mikataba mibovu inayoiumiza nchi hivi sasa ni rushwa kubwa kushinda rushwa ndogo ndogo anazozipigia kelele Sumaye zinazojitokeza mara nyingi nyakati za uchaguzi, na kwamba huenda bado ana machungu ya kushindwa katika uchaguzi wa ujumbe wa NEC wilayani kwake na Dk. Mary Nagu.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari iwapo hivi sasa yupo katika harakati za kumfanyia kampeni mmoja wa watu wanaotaka kuwania urais nchini, Mgeja alisema yeye binafsi haamini kama ni wakati muafaka wa Watanzania kuanza kulumbana juu ya mtu gani awe rais mwaka 2015.
“Mimi nafikiri suala nani awe rais mwaka 2015 si wakati huu, na halipaswi kupewa nafasi ya kusababisha Watanzania tugawanyike, tujengeane uhasama, chuki na fitina, na kusababisha kupoteza umoja na mshikamano wetu tulionao,” alisema Mgeja.
Chanzo:- Tanzania Daima


No comments:
Post a Comment