Social Icons

Wednesday, 6 November 2013

WINNIE MANDELA NA MAUAJI YA KUTISHA


WAKATI utawala wa kibaguzi wa makaburu wa nchini Afrika Kusini ulipofikia tamati, mwaka 1994, rais aliyeingia madarakani kwa kufuata demokrasia, Mzee Nelson Mandela, aliona ni vyema wananchi wa nchi hiyo waukabili ukweli wa yale yaliyotokea wakati wa utawala huo wa kibaguzi na kuridhiana ili kuponya vidonda na kupoza mioyo ya wale walioathirika na vitendo hivyo.

Ili kupata ukweli, wakati huo akiwa ndiye rais wa kwanza mweusi nchini humo aliyechaguliwa kidemokrasia, Mzee Nelson Mandela aliunda Tume ya kuukabili Ukweli na Maridhiano (The Truth and Reconciliation).

Rais Mandela alijua kwamba, matukio yaliyopita wakati wa serikali ya kibaguzi ya makaburu nchini humo hayawezi kuzikwa na kusahaulika hivi hivi, ni lazima wayakabili.

“Sisi kama kama taifa ni lazima tuukabili ukweli ili tuweze kujiponya wenyewe..” alinukuliwa akisema Rais Mandela, kwa wakati huo.

Rais Mandela aliunda timu ya majaji 17 wanasheria na wachungaji,  wakiwemo weupe na weusi na wadau wengine kutoka katika kada mbalimbali za kisiasa na kijamii.

Ikiwa chini ya mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Askofu Desmond Tutu, tume hiyo ilipewa jukumu la kutafuta ukweli wa yale yaliyotokea nchini humo wakati wa serikali ya kibaguzi.

Wale wananchi wa kawaida walioshiriki katika uhalifu mbalimbali wakati serikali ya kibaguzi ikiwa madarakani, lakini pia wale waliokuwa katika serikali hiyo ya kibaguzi nao walialikwa kwenda mbele ya tume hiyo ili kueleza kuhusu vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu walivyovifanya chini ya mwamvuli wa serikali ya kibaguzi na waliahidiwa na tume hiyo, kwamba kama wataeleza ukweli basi watawekewa kinga ya kutoshitakiwa.

Hata wananchi wa kawaida waliohusika kwa njia moja ama nyingine na uhalifu wa kibinadamu wakati wa utawala huo dhalimu wa kibaguzi nao walipewa fursa hiyo, kwamba, wakisema ukweli watawekewa kinga ya kutofunguliwa mashitaka dhidi ya makosa yao.

Tangu kuundwa kwa tume hiyo Aprili mwaka 1996, tume hiyo ilifanya vikao katika kumbi mbalimbali na katika makanisa kwenye miji mbalimbali nchini humo.

Wakati wa vikao hivyo tume hiyo ilishuhudia baadhi ya watu mbalimbali wakiwemo weusi na weupe wakielezea kuhusu vitendo vya kikatili walivyofanya au kushuhudia vikifanyika dhidi ya binadamu.

Baadhi ya simulizi hizo zilikuwa ni za kutisha kiasi cha kuwaacha wasikilizaji wakilia. Wazazi walisikia jinsi watoto wao walivyouawa, watu walioathirika na vitendo vya serikali ya kibaguzi walieleza kuhusu madhila yao jinsi walivyoteswa.

Kutokana na simulizi hizo za kutisha, kiongozi wa tume hiyo, Askofu Desmond Tutu alilazimika kutenga chumba maalumu ambacho alikuwa akikitumia kulia nje ya chumba cha mkutano.

Ilikuwa kila mahali alipokwenda, lazima chumba hicho kiandaliwe. “Kulikuwa na chumba ambacho machozi ya watu yalikuwa yakisafisha majeraha yaliyotokana na serikali ya kibaguzi iliyopita,” alinukuliwa akisema Askofu Desmond Tutu.

Ndani ya mwaka mmoja tume hiyo ilikuwa imekwishahoji zaidi ya watu 7,000 na kila aliyejieleza katika tume hiyo, simulizi yake ilikuwa ni ya kutisha na kuogofya.

Kutokana na hali ya kutoaminiana tangu kuondolewa kwa serikali ya kibaguzi, shughuli za tume hiyo zilikuwa haziripotiwi na hazikuwa zikifuatiliwa sana.

Hata hivyo ilikuwa bado kitambo kidogo tu, yale yanayojiri ndani ya tume hiyo yaanze kuvuta hisia za watu wengi nchini humo, lakini pia vyombo vya habari havikubaki nyuma katika kufuatilia jambo hilo kwa ukaribu.

Winnie MandelaHiyo ilikuwa ni baada ya aliyekuwa Mke wa Rais Mandela, Winnie Madikizela-Mandela ambaye walitalikiana kutokana na rais huyo kumtuhumu mkewe kuwa ni mzinzi, kutakiwa aripoti katika tume hiyo Desemba 1997.

Kitendo cha Winnie Mandela kuitwa katika tume hiyo kilimfedhehesha mno Rais Mandela, kwani kitendo cha kushuhudia mwanamke aliyemwoa na kudumu naye kwa miaka zaidi ya 30, kabla hawajaachana, anasimamishwa katika tume hiyo akituhumiwa kwa mauaji, unyanyasaji na ukatili dhidi ya watu wake mwenyewe, kilimweka katika wakati mgumu.

Awali Askofu Desmond Tutu, rafiki wa karibu wa familia ya Mandela kwa miongo kadhaa, alimuomba Winnie Mandela kujitokeza mbele ya tume hiyo kwa hiyari yake mwenyewe, lakini baada ya kukataa, hakuwa na jinsi nyingine, isipokuwa kutoa amri kwa mamlaka ya tume hiyo ajitokeze. Hata hivyo ulikuwa ni uamuzi ambao hata yeye (Askofu Desmond Tutu) ulimuumiza.

Alipojitokeza kwa mara ya kwanza katika tume hiyo hapo Desemba 9, 1997, Askofu Tutu huku akionekana kulengwa machozi alimuomba Winnie Mandela awajibike kwa matukio ya kihalifu dhidi ya binadamu, yaliyofanyika na kuhusishwa na jina lake.

 “Nakupenda sana Winnie, nakuomba, nakuomba, nakuomba….., wewe ni mtu mkubwa na hujui ni kiasi gani utaheshimika iwapo utasema: samahani sikufanya vyema, naomba mnisamehe,” alieleza Askofu Tutu.

Hata hivyo pamoja na Askofu Tutu kumuomba aseme ukweli na kuomba radhi kuhusu yale yaliyotokea na kuhusishwa na jina lake, lakini Winnie Madikizela-Mandela huku akionekana kutokuwa na hisia za kujutia vitendo alivyotuhumiwa kuvitenda, alisema tu kwa kifupi, “mambo yalikuwa ni ya kutisha na kusikitisha.” Kisha akaendelea, “...kwa hiyo naomba mniwie radhi kwa yote yaliyotokea.”

Lakini alikanusha kuhusika vitendo vya utekaji nyara, utesaji na mauaji vilivyokuwa vikifanyika katika viunga vya Soweto na kundi lake lililokuwa likimtumikia.

Chanzo:- Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates