Social Icons

Sunday, 22 December 2013

KUNG'OLEWA MAWAZIRI: Wasomi wapongeza, watahadharisha


WASOMI nchini wamepongeza, huku pia wakitahadharisha hatua iliyotumiwa na wabunge kuungana hadi kuwang’oa mawaziri wane, ambao majina yao yalitajwa kwa namna moja ama nyingine katika sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili. Akizungumzia hatua hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dk. Prosper Ngowi, alisema kwa suala lililotokea bungeni juzi, wabunge wameonyesha jukumu lao la kuisimamia serikali.

“Angalau kwa jambo lililotokea juzi Bunge limeonyesha wajibu wao wa kuisimamia serikali, kwa jambo hili limejipa hekima na heshima inayostahili, lakini kwa kitendo cha Rais Kikwete kukubali kutengua nyadhifa za wale mawaziri ni kitendo cha busara,” alisema Dk. Ngowi.

Dk. Ngowi pia alitoa angalizo kwa Rais Kikwete anapokwenda kubadilisha safu ya Baraza la Mawaziri kuwa makini kwa kuweka mawaziri wepesi ambao hawahitaji kujifunza kwa muda mrefu.

“Tayari serikali hii imebakisha miaka miwili ya utendaji, Rais awe makini katika kuteua mawaziri, achague watu wepesi na si watu wa kujifunza, akichagua mtu wa kujifunza atapoteza muda na fedha za Watanzania,” alisema Dk. Ngowi.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kikao cha Bunge kimefanya uamuzi mzuri, huku akitoa rai ya kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuhusika kwenye matukio yaliyotajwa kwenye taarifa za kamati.

“Nitoe rai kwamba wale wote ambao wamehusika katika hili wasiachwe, lakini nitoe angalizo langu kwamba isije ikawa ile taarifa imetiwa chumvi sana, niungane na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, kutaka kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kuchunguza taarifa zote zilizowasilishwa.

“Kwa mtazamo wangu, naona hata ile taarifa ya kamati inatakiwa kufanyiwa uchungizi na ikibanika kuna sehemu imetiwa chumvi, basi na wale walioiandaa wachukuliwe hatua,” alisema Dk. Bana.

Akizunguzia hatua ya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki kutangaza kujiudhulu mwenyewe, alisema kitendo hicho kitaendelea kukumbukwa katika historia ya siasa.

Dk. Bana alisema suala la kuwawajibisha mawaziri liende sambamba na kurekebisha mifumo ya uendeshaji serikali.

“Leo hii wakati kina Kagasheki wanang’atuka, wale watu wanaojihusisha na biashara haramu wanasherehekea ushindi, wakati umefika mifumo ya utendaji irekebishwe, hususan katika wizara na kazi ianze katika wizara hii ya Maliasili na Utalii,” alisema Dk Bana.

Dk. Bana pia alisema kuwa kitendo cha mawaziri wanne kuondolewa kwenye Baraza la Maziri kimempa nafasi Rais Kikwete kuwaondoa mawaziri waliotajwa kama mizigo.

“Nitashangaa kama wale mawaziri mizigo wataachwa, hii ni fursa tosha kwa Rais kuwaondoa wote waliotajwa na kuweka watendaji, lakini Rais asiishie hapo tu, bali akaondoe na wale makamanda waliosimamia ile operesheni yote ya kutokomeza majangili,” alisema Dk. Bana.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Bashir Ally, alitilia shaka kitendo cha mawaziri kuwajibishwa kwa kelele za wabunge.

“Yapo mambo kama manne hivi ya kuangalia, tuangalie kwamba Bunge litaendelea na mtindo wa kuwawajibisha mawaziri hadi lini, nitoe mfano mdogo kwamba mambo haya yameanza kutokea toka mabunge yaliyopita, likiwemo lile lililoibua tuhuma za Richmond, ripoti ilisomwa kwa mbwembwe, lakini tujiulize hadi leo hii ile ripoti imefanya nini.

“Bunge lazima lijiangalie kwamba litafanya kazi ya kuwahimiza watu kujiuzulu hadi lini, kuna ile tume iliitwa ya Jairo, ripoti yake ilivuma, hebu tujiulize kuwa hadi leo hii ripoti ile imefanya kazi kwa kiasi gani? Lakini kuna tume iliundwa ikaenda Mtwara kuchunguza namna ambavyo wananchi waliteswa wakati ule wa vurugu za gesi, je, ripoti hii imefanya nini?

“Spika atueleze ripoti hizi zimefanya nini, mimi natoa angalizo kuwa isije kuwa watu wanaweka mijadala bungeni kwa ajili ya kujipatia umaarufu, nafikiri wabunge wanapaswa kujiangalia,” alisema Bashir.

Alisema kwa upande mwingine, Rais Kikwete anapaswa kujichunguza njia anayoitumia katika kuweka mambo sawa, baada ya kupata shinikizo la wabunge.

“Rais naye ajichunguze kuwa je, njia anayoitumia ni sahihi, aangalie kuna tatizo gani katika kuendesha hizo wizara, aangalie toka ameanza tayari ameshakuwa na mawaziri wakuu wawili, mawaziri wizara ya maliasili na utalii wanne, achunguze kuwa je, tatizo lililopo Maliasili ni watu, je, kwanini wizara hiyo haitawaliki,” alisema Profesa Bashiru.

Alisema baadhi ya wabunge wametamka wazi na kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aondoke na mawaziri waliobainishwa na tume ya uchunguzi, jambo analosema linaweza lisilete suluhu.

“Nisema wazi hakuna muujiza utakaotokea hata mawaziri wote wakifukuzwa kazi, nasema tena hii nchi haijarogwa, tatizo lake kubwa ni woga wa kujitawala, uchumi wetu ni kilema, unategemea zaidi mitaji kutoka nje, wanaochimba mafuta wanatoka nje, wanaomiliki migodi mikubwa ya dhahabu na vitalu wanatoka nje. 

Chanzo:- Mtanzania

No comments:

 
 
Blogger Templates