ALIYEKUWA Waziri Mkuu wa Tanzania, John Malecela ndiye Mtanzania pekee aliyepata nafasi ya kumtembelea Nelson Mandela wakati akitumikia kifungo cha maisha kwenye gereza la kisiwa cha Robben, nchini Afrika Kusini. Akizungumza na Rai Jumatano jana, Malecela alisema kuwa alifurahia kuipata fursa hiyo na kwamba kifo cha Mandela kimemsikitisha kwani alipata nafsi ya kumjua kiongozi huyo wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini.
Malecela alisema kuwa alifanikiwa kupata nafasi ya kumtembelea Mandela gerezani baada ya kuteuliwa na Jumuiya ya Madola kuunda kamati ya kutafuta maridhiano kati ya serikali ya Makaburu na chama cha ANC.
“Kamati yetu ilikuwa na watu saba, mimi jina langu lilipendekezwa na Rais Kaunda na kupewa sapoti na Rais Mugabe, nikiwa kwenye kamati ile, ambayo nashukuru ripoti yetu kwa namna moja au nyingine ilisaidia kuachiwa huru kwa Mandela, kwani sisi tulikwenda mwaka 1985 mwishoni na safari yetu ya mwisho ilikuwa mwaka 1986 , baada ya miaka minne aliachiwa huru,”alisema Malecela.
Aidha aliwataja baadhi ya watu waliounda kamati yao kuwa ni aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo ambaye wakati huo alikuwa Waziri Mkuu, Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Australia Marcolm Fraser, aliyekuwa Waziri wa Fedha wa India, Mchungaji wa Canada na mwanamama Nitha Baro.
Hata hivyo Malecela alisema kuwa walipokutana na Mandela kwa mara ya kwanza ili kumueleza dhamira yao, hakukubaliana nao kwani alitaka akutane na wafuasi wa chama chake kwanza ndipo afikie maamuzi ya kuzungumza nao.
Kwa mahojiano zaidi na kujua alichokisema Malecela juu ya uhusiano wake na Mandela, usikose kusoma gazeti la Rai la Jumapili.
Chanzo:- Rai

No comments:
Post a Comment