WABUNGE wa Bunge la Tanzania wameingia katika kashfa baada ya kubainika kuchukua posho za safari za kwenda nje ya nchi lakini wakabaki nchini pasipo kurejesha fedha hizo, Raia Mwema limebaini.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alichukua hatua za makusudi kuhakikisha karibu kamati zote za wabunge zinasafiri ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza masuala ya kibunge; lakini uamuzi huo sasa umeanza kutumiwa vibaya na baadhi ya wabunge.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili wakati huu wa mkutano wa sasa wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, umebaini kwamba karibu wabunge wote wamesafiri.
Wanachofanya baadhi ya wabunge kwa sasa ni kukusanya posho zao za safari kana kwamba watasafiri lakini huishia kubaki nchini, huku wengine wakikaa kwa siku chache safarini na kurejea ingawa wanakuwa wamelipwa posho ya siku nyingine.
Mmoja wa wabunge waliokumbwa na tuhuma hizi ni Mbunge wa Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari, ambaye alidaiwa kuchukua posho ya shilingi milioni nane kwa ajili ya safari ya kwenda nchini Malaysia, lakini hakwenda ingawa alipokea fedha hizo.
Raia Mwema limeambiwa kwamba Nassari ambaye ndiye mbunge mwenye umri mdogo kuliko wabunge wote wa Bunge hilo, akiwa amezaliwa mwaka 1985, alisema ataungana na wenzake wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii baada ya siku chache wakiwa Malaysia lakini hakwenda.
Siku chache baadaye, Nassari aliingia kambini na timu ya Bunge iliyokwenda nchini Uganda kushiriki mashindano ya mpira wa miguu, ambako nako alilipwa posho na Bunge hilo.
Akizungumza na gazeti hili katika viwanja vya Bunge wiki hii, Nassari alikiri kuchukua posho hiyo bila ya kwenda Malaysia, ingawa alisema suala lake linafahamika bungeni.
“Nilikuwa na dharura. Kulikuwa na harambee muhimu sana kule jimboni kwangu ambayo nilikuwa nihudhurie na hivyo nikatoa taarifa kwa viongozi wangu wa Bunge.
“Kama Bunge wakiniambia nirudishe hizo fedha nitarudisha bila ya matatizo. Kwa bahati nzuri nilijua kwamba kuchukua hela bila ya kufanya kazi ni makosa na ndiyo maana nikatoa taarifa kwa wahusika,” alisema.
Gazeti hili limefanikiwa kuona barua pepe (email) iliyoandikwa Novemba 28, mwaka huu na Nassari kwenda kwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, ikimueleza kuhusu suala hilo.
“Nilitakiwa kwenda nchini Malaysia na Kamati ya Maendeleo ya Jamii lakini sikwenda kwa sababu ya kutingwa na shughuli ya harambee jimboni kwangu.
“Tayari nilikuwa nimechukua posho ya safari. Kwa barua hii, naomba maelekezo ya ofisi yako ili yale yaliyo ya Kaisari nimpe Kaisari na yale yaliyo ya Mungu nimpe Mungu,” aliandika Nassari katika barua hiyo ambayo pia nakala yake ilitumwa kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa.
Mbunge mwingine aliyeingia katika mkumbo huu ni Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, ambaye inadaiwa alichukua posho ya safari ya kamati yake iliyokwenda Dubai na Uingereza lakini hakwenda kwenye safari hiyo.
Raia Mwema limeambiwa kwamba karibu wajumbe wote wa kamati hiyo walilipwa kiasi cha shilingi milioni tano kila mmoja kama posho ya safari, lakini mbunge huyu mwenye umri wa miaka 51 hakwenda kwenye safari hiyo.
Alipohojiwa na gazeti hili, Zambi alisema; “Ni kweli kwamba nilichukua hiyo posho lakini sikwenda kwenye hiyo safari. Kwanza nilikuwa na ugeni mkoani kwangu ambako Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alikuwa akitembelea.
“Lakini, siku moja baada ya Kinana kumaliza ziara yake, nilipata msiba wa mdogo wangu. Sasa, ningewezaje kuacha msiba kama huu kwa sababu ya hizo milioni tano?
“Mimi ni Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mbeya na Katibu Mkuu wa chama taifa alikuwa anatembelea mkoa wangu, sasa ningewezaje kumuacha peke yake?
“Kwanza kama Bunge likizihitaji hizo fedha ni suala la kuniambia tu kwa sababu nitazirejesha. Kama wewe ungekuwa umefiwa na mdogo wako ungeweza kuendelea na safari ili uhalalishe matumizi ya shilingi milioni tano?” alihoji mbunge huyo.
Gazeti hili limepata pia taarifa kuhusiana na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Pindi Chana, ambaye ingawa inadaiwa alilipwa posho kwa ajili ya safari ya kwenda Kenya na Ghana lakini akaenda Kenya ambako alikaa kwa siku mbili na kisha akaenda zake India kwa matibabu.
Chana ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria ambayo ilikuwa na ziara ya wiki mbili katika nchi hizo; na Raia Mwema limeambiwa kwamba kutokana na kutokuwepo kwa mwenyekiti huyo, kamati hiyo ilirejea nchini siku mbili kabla ya siku ambazo walikuwa wamelipiwa na Bunge.
“Mwenyekiti alikuja Kenya akakaa kwa siku mbili tu na baada ya hapo akatuaga kwamba anakwenda India kwa ajili ya matibabu. Ninafahamu alikuwa amelipwa posho yake kwa sababu wengine wote tulikuwa tumelipwa wakati huo,” mmoja wa wajumbe mashuhuri wa kamati hiyo aliliambia gazeti hili.
Kwa kawaida, endapo mbunge atakuwa amekwenda nchi za nje kwa matibabu baada ya kupitishwa na Wizara ya Afya, Bunge humlipa posho ya dola 420 (Sh 672,000) kwa siku.
Hata hivyo, Pinda hakutaka kuzungumzia suala hilo wakati alipohojiwa na mwandishi wa gazeti hili jana zaidi ya kusema kwamba; “hakuna ukweli wowote kwenye hilo.”
Mbunge mwingine ambaye gazeti hili limepata taarifa zake ni Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Joyce Mukya, ambaye inaelezwa alikatiza safari yake ya kibunge nchini Dominica kabla ya kumaliza muda wake.
Gazeti hili limeambiwa na vyanzo vyake kutoka duru za Bunge kwamba Joyce alikatisha ziara yake hiyo kutokana na shinikizo la mmoja wa viongozi wakuu wa kambi ya upinzani bungeni.
Hata hivyo, Mukya jana alikanusha kutomaliza ziara yake hiyo na kusema alikwenda na kudai hawezi kutoa taarifa zaidi.
Gazeti hili limeambiwa na mmoja wa wabunge kwamba tabia hii sasa imekithiri kwa sababu uongozi wa Bunge haufuatilii sana endapo mbunge alilipwa na hatimaye akasafiri.
“Kuna njia rahisi sana ya kujua iwapo mbunge alisafiri au hakusafiri. Katibu wa Bunge angetangaza tu hapa kwamba kila anayesafiri safari ya nje, anatakiwa awasilishe boarding pass yake (tiketi ya kuingia ndani ya ndege) bungeni. Kwa hali ilivyo sasa, mtu anaweza kuchukua posho yake na akabaki hapa bila ya kufanywa lolote.
“Yaani uwajibikaji hakuna kabisa. Kama sisi wenyewe tunashindwa kusimamiana, tunawezaje kupata ujasiri wa kutaka kuisimamia serikali?” alihoji mbunge huyo alyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina.
Suala hili limeonekana kuuletea uongozi wa Bunge changamoto ya aina yake na jana Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, hakutaka kuzungumzia kuzungumzia suala hili na akashauri gazeti limsubiri Spika au Katibu wa Bunge ambao wako safarini kwa sasa.
Chanzo:- Raia Mwema



No comments:
Post a Comment