“Hebu kwanza elezeni vizuri kuna nini?” Hailat dada yake Nargis aliuliza.
“Tulikuwa ndani tumepumzika, baba Zumza alirudi mapema na siyo kawaida yake na kusema amechoka na kwenda chumbani kwake kupumzika.
Ghafla walikuja kina Sunu walisema umewatuma pete ya mumeo. Baada ya kuichukua waliondoka na kutuacha
tukimuandalia kinywaji. Alisema mmoja wao.
SASA ENDELEA...“
Lakini ghafla tulianza kusikia mtikisiko mkubwa nje ya nyumba na baadaye nyumba ikaanza kutikisika ghafla tukaanza kuona moto kila kona kitu kilichotufanya tutoke mbio kuokoa maisha yetu.”
“Mmh! Wakati nyumba inaungua mume wangu alikuwa wapi?” Nargis aliuliza kwa hofu.
“Ndani amelala.”
“Mungu wangu mume wangu atakufa, mama watume wakamuokoe.”
Watwana waliokuwa bado wamelala kifudifudi walitumwa kwenda kumuokoa Thabit, baada ya amri ile walitoweka mara moja na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Thabit.
Walipofika eneo la nyumba walishangaa kukuta bahari, hali ile iliwashtua sana na kujikuta
wakijiuliza labda wamekosea kila waliporudia ramani yao eneo lilikuwa lilelile.
Walijikuta wakiulizana wenyewe:
“Jamani tumekosea wapi?”
“Hatujakosea hapo kwenye bahari ndipo kwenye hiyo nyumba kwani nyumba tuliyofikia kabla ya kuingia ndani si hiyo hapo pembeni
ya bahari?” mmoja alisema.
“Sasa tutafanyaje kama hakuna nyumba tuliyotumwa na mume wa mwana wa mfalme tutamuona wapi?”
“Jamani ile si bahari basi tuingie ndani ya maji ili tujue ndani kuna nini.”
“Poa.”
Walikubaliana na kuteremka ndani ya ile bahari, walipoyagusa maji wote walitoka haraka kila mmoja akipiga kelele za maumivu ya kuungua na moto.
“Motooo!”
Bahari ilikuwa inaunguza walisimama huku kila mmoja akionesha majeraha ya moto.
“Jamani hii ngoma nzito turudishe taarifa.”
“Hatuna jinsi.”
Walikubaliana kurudi chini ya bahari kurudisha taarifa ya hali halisi waliyokutana nayo sehemu yenye nyumba ya Thabit.
Walirudi chini ya bahari kurudisha taarifa, walipofika walimkuta Nargis akiwasubiri kwa hamu kutaka kujua wamefikia wapi
badala ya kurudi bila mumewe.
“Vipi?”
“Hali ni mbaya.”
“Kuna nini?”
“Nyumba haionekani zaidi ya bahari.”
“Bahari imefanya nini?”
“Sehemu yenye nyumba kuna bahari kubwa sana.”
“Sasa kwa nini msiingie ndani?”
“Yaani hali inatisha tumeingia tumeungua vibaya, bahari ina maji ya moto ajabu,” walionesha majeraha.
“Mmh! Sasa nimeelewa,” malkia Zabeda alisema.
“Nini mama?” Nargis aliuliza huku machozi yakimtoka.
“Wametuwahi.”
“Kivipi mama?”
“Inaonesha jinsi gani aliyepanga mpango wa kumchukua mumeo amefanikiwa. Tulitakiwa tumchukue badala ya kuichukua pete tu lakini tumechelewa.”
“Mama sikubali... sikubali nitakufa na mtu.”
“Lazima tujipange la sivyo safari hii tutapotea kabisa.”
“Sasa nitafanyaje?” Nargis aliuliza huku machozi yakimtoka.
“Labda dada yako akusaidie kwa vile wewe huwezi kwenda huko kwa sasa.”
“Mama mimi siendi kokote nilimueleza toka zamani akawa mbishi juu ya wanadamu, mimi nawafahamu vizuri kuliko yeye anayekurupukia mambo.
Wanadamu tunawapenda tu lakini ni viumbe wabaya kuliko hata nyoka mwenye sumu kali. Kama walishindwa kuishi katika bustani ya edeni waliyopendelewa na Mungu wataweza vipi kukaa na viumbe wengine.
“Ningekuwa mimi ningemuulia mbali tena mdogo wangu una bahati umepata watoto ulikuwa ukiwatafuta. Muulie mbali uachane na
maisha ya mashaka, wapo majini wazuri kuliko Thabit wanaokupenda Zahal au Mehoob wapo tayari kukuoa hata leo.”
“Dada bado hujanishawishi yule ni mume wangu hivyo siwezi kumuua kwa ajili ya yaliyotokea, vilevile hakuna mwanaume wa kijini atakayemshinda uzuri mume wangu Thabit.
Najua aliyefanya vile ni mwanamke, kwani siku zote wanawake tumekuwa ndiyo chanzo cha
matatizo.
Hao wanadamu wasingetoka katika bustani ya edeni bila sisi wanawake ambao ndiyo chanzo cha kufukuzwa kwao.
“Hata kama hamtanisaidia nitapigana peke yangu hata nikifa kwa ajili ya kupigania haki yangu siogopi kitu.”
“Ukifa nani atakulelea wanao?” dada yake alimuuliza.
“Mtavyowafanya mtajua nina imani nao wakikua watalipa kisasi kwa atakayeniua mama yao.”
“Nargis mwanangu, inavyonekana watu tutakaopambana nao wamejizatiti. Kama wameweza kuua nguvu ya pete na kuingia kwenye nyumba tuliyoitengeneza, basi kazi ipo tunatakiwa kuongeza nguvu.”
“Ninyi piganeni mimi simo, siwezi kuumia kwa kitu kisicho na faida, atajua mwenyewe atakavyofanya. Kwa nini kila siku tuwe tunapambana na wanadamu hamuoni nao wana akili pengine wameshatujulia, ndiyo maana wanafanya wanavyotaka,” dada yake Hailat alisema kwa uchungu.
“Mama naomba mnisikilize kwa makini, nina miaka minne ya kuwa huku, naomba mniachie kila kitu, sihitaji msaada wenu muda wangu ukifika nitapambana mwenyewe.
Tusije tukakosana bure kwa jambo linalonihusu mwenyewe,” Nargis alisema.
“Hilo ndilo neno hata mimi nakuunga mkono,” dada yake aliunga mkono kauli ya mdogo wake.
“Dawa iliyopo ni kuiharibu mali yake ili kumtia umaskini,” mama yao alitoa wazo.
“Mama hiyo siyo dawa, Thabit hana kosa lolote zaidi ya huyo aliyefanya mchezo ule,” Nargis alimtetea mumewe.
“Sawa lakini tukimtia umaskini, lazima yule mwanamke atamkimbia na wewe utapata nafasi ya kumpata mume wako.”
“Una uhakika gani kama huyo mwanamke atamkimbia, sitaki kuharibu chochote kwenye mali ya Thabit. Sitaki apate tatizo lolote ila nitahakikisha anarudi mikononi mwangu.”
Itaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment