Social Icons

Monday, 8 September 2014

HADITHI: Nilioa jini nikamsaliti -4


 “Amekwambia au umekiona kwa macho yako?”
“Yaani nimeona mwenyewe kwa macho yangu.”
“Kimepasuka kabisa?”
“Tena kimelia kama bomu.”

“Mmh! Hukukosea kitu?”
“Sijakosea nimefuata kila hatua toka jana usiku.”
“Sasa itakuwa nini, mbona mara zote haikutokea kitu kama hicho?”
“Nikuulize wewe.”
SASA ENDELEA…

“Basi turudi kwa mzee Mukti.”
“Kwa lililotokea,  leoleo twende jioni.”
“Hakuna tatizo.”
                                                              ***
Baada ya muda Thabit alirudi akiwa amebadili nguo, Subira alishtuka na kujiuliza ataambiwa nini.
“Vipi bosi?” aliuliza kwa unyenyekevu.
“Nipo sawa.”

“Vipi umeenda hospitali?”
“Sijaenda kwa vile sijaumia chochote.”
“Pole sana.”
“Asante, nipo ofisini.”
“Sawa.”

Subira aliendelea na kazi zake huku akihofia kumuwekea dawa kwenye juisi kwa kuhofia tukio lile kutokea tena. Muda wote alifanya kazi bila amani moyoni, akili yake iliwaza kwenda kuonana na mzee Mukti ili ajue tatizo nini.

Muda wa kutoka kazini Subira alikodi teksi na kumpitia shoga yake na kwenda Mji Mwema kwa mganga Mukti Buguju. Kutokana na foleni walifika saa kumi na mbili na nusu jioni. Walikuta kuna wateja wengi ilibidi wasubiri kuonana naye mpaka saa mbili na nusu usiku ndipo walipokutana.
Baada ya kuingia kwenye chumba cha uganga walikaa kwenye mkeka na kumsalimia mzee Mukti.
“Marahaba warembo, kama sikosei mlikuja jana?”

“Ndiyo mzee.”
“Vipi mbona ghafla?”
“Kuna tatizo mzee wangu,” Sofi alisema kwa niaba ya Subira aliyekuwa amenyamaza kimya.
“Tatizo gani?”
“Subira mueleze,” Sofi alimgeukia Subira na kumwambia.
“Ndiyo binti,” mzee Mukti alimsemesha Subira aliyekuwa ameinama.

“Kumetokea tatizo ofisini.”
“Tatizo gani?”
“Kuhusiana na ile dawa ya chai.”
“Imefanya nini?”

Subira alielezea yote yaliyotokea baada ya kufuata maelekezo ya kutumia dawa kuanzia usiku na asubuhi alipomtengenezea chai na maajabu yalitokea.
“Hicho kikombe kimemdondoka wakati anakunywa chai au vipi? Hebu nifafanulie.”
“Kimepasuka kabla hajainywa, kikombe kilipokaribia mdomoni kilipasuka kama bomu.”
“Eti?” mzee Mkuti alishtuka.

“Hakikumponyoka bali kimepasuka kama bomu kabla hakijagusa mdomo,” Subira alirudia.
“Chai haikumuunguza?”
“Kidogo lakini hakwenda hospitali.”

“Mmh! Kazi ipo,” mzee Mukti alisema huku akichukua unga kwenye kichupa kidogo kilichokuwa kwenye chupa nyingi za dawa na kumwaga kwa kuusambaza na kutulia kuutaza sehemu alizotupa  kwa muda akiwa ameshika tama kisha aligeuka na kusema.

“Mmh! Kazi hii niliidharau kumbe ni nzito sana, bosi wako ni mume wa jini lililopo chini ya bahari na utajiri ule jini yule ndiye aliyempa. Kwa sasa yupo ujinini amekwenda kujifungua na atarudi baada ya miaka kumi. Kwa hiyo ametegesha mawasiliano yake na kuona kila kinachotendeka duniani ili kumlinda mumewe.

“Jini yule ni mpole sana ila ni mkorofi anapotaka kuingiliwa katika maisha yake hasa kumchukua kipenzi mume wake. Ile pete anayovaa bosi wako ndiyo mawasiliano makuu kati yake na mkewe jini Nargis. Kila kitu kinachofanyika lazima ajue na kutumia nguvu zake za kijini kupitia pete ile kuzuia Thabit asipatwe na tatizo lolote, ndiyo maana nikasema kazi ile sikuiangalia mapema kumbe nzito sana.”

“Kwa hiyo tutafanyaje maana kama ni hivyo rafiki yangu yupo hatarini?” Sofi aliuliza kwa niaba ya shoga yake.
“Kama mna nia ya dhati, itabidi muingie gharama za kuweza kuvunja mawasiliano kati ya Thabit na mkewe jini, kisha nikutengeneze wewe hata miaka kumi ikiisha akirudi asikufanye kitu kwa vile tutakuwa tumemdhibiti.”

“Kama kiasi gani?”
“Laki tatu.”
“Mzee wangu mbona nyingi sana?” Sofi aliuliza.
“Ni kweli ni nyingi lakini ni ndogo kulingana na kazi yenyewe, kumbuka nikikosea hata mimi naweza kufa kwa vile vita hiyo lazima itageukia kwangu. Pia baada ya zoezi letu utakuwa na maisha mazuri sana.”
“Sawa nitalipa,” Subira alikubali.

“Kazi hii inatakiwa ifanyike haraka sana kwa vile tayari tumeichokoza.”
“Sawa mzee wangu, lini?”
“Kwa vile mwezi bado haujamezwa na mawingu, kazi yako itafanyika kesho usiku saa sita baharini. Unatakiwa uje kulala huku na ukitoka hapa unafikia moja kwa moja kazini.”
“Sawa hakuna tatizo.”

“Nina imani lile ni tatizo ambalo halina madhara kwako, endelea kutumia dawa kujifusha kuoga ya chai na juisi achana nayo kwa muda.”
“Sawa mzee wangu, naweza kukutumia leo kutoka katika simu?” Subira aliuliza.
“Hakuna tatizo.”
Mganga alimtajia namba za simu, Subira alimtumia fedha yote kisha waliagana na kuondoka kuwahi nyumbani kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana.
                                                             ***
Siku ya pili majira ya jioni Subira alielekea Mji Mwema kwa mzee Mukti Buguju peke yake kwa vile siku ile alitakiwa kulala kule. Alifika saa moja usiku na kwenda moja kwa moja kwa mzee Mukti alipomuona alimkaribisha na kumuomba atulie kwa vile kazi yake ilitakiwa kufanyika saa sita usiku mwezi ukiwa katikati.

Majira ya saa tano usiku alifuatwa na kijana wa mzee Mukti na kumwambia ajiandae kuna safari ya kwenda baharini. Alipewa shuka nyekundu na kilemba chekundu na kuambiwa avue nguo zote ajifunge zile kisha asuburi. Baadaye aliitwa nje, alipofika alikuta watu wanne na mzee Mukti na kuelezwa;
“Sasa mama kazi ndiyo inakwenda kuanza kwa vile hali ya hewa inaruhusu.”

Inaendelea.

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates