Social Icons

Tuesday, 9 September 2014

Maalim Seif ni Popo






















MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), amemshambulia kwa maneno Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Maalim Seif Sharif Hamad, huku akimfananisha na popo.

Mbunge huyo alisema hayo baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, akisema lengo ni kujibu mashambulizi yaliyoelezwa kwake na Maalim Seif kupitia kituo kimoja cha televisheni.

Baada ya kupewa fursa hiyo, Hamad alisema Maalim Seif hafai kuwa kiongozi kwa kuwa hana msimamo kisiasa jambo ambalo linamfanya awe kama popo ambaye hajulikani kama ni ndege au mnyama.

Hamad aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akizungumzia tuhuma dhidi yake, alizodai zilitolewa juzi na Maalim Seif wakati aliposhiriki kipindi maalumu katika televisheni moja ya hapa nchini.

Alisema juzi, Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alizungumzia mambo yanayohusu kamati yake namba tano.

“Kwanza, alisema kuwapo kwangu ndani ya Bunge ni kubebwa na Spika wa Bunge la Muungano kwani kesi niliyofungua ilishakwisha mahakamani na mimi siyo mbunge tena.

“Naomba nitoe taarifa, kwamba shauri nililofungua bado linaendelea na kesi ipo tarehe 26 mwezi huu na siku hiyo haitakuwa hukumu ila ni siku ya kuendelea kusikilizwa.

“Hivyo basi, ni vizuri Maalim Seif kama mtu mzima na kwa nafasi aliyonayo, asitake kuwadanganya Watanzania kwani hategemewi kutoa taarifa isiyo sahihi kwa nafasi yake ya kumshauri Rais wa Zanzibar.

“Katika hili, naomba nitamke kwamba, Spika yuko makini na hana mamlaka ya kuingilia mahakama, kwahiyo, hoja ya kumpandikiza Spika siyo sahihi na namuomba amuombe radhi,” alisema Hamad.

Pamoja na hayo, alizungumzia mwenendo wa kamati yake na kusema imekuwa ikifanya kazi kwa kufuata kanuni kama zilivyo kamati nyingine.

“Kwa mujibu wa ibara ya 52 ya kanuni za Bunge hili, tuliunda kamati 12 na mimi naongoza kamati namba tano.

“Katika kamati yangu, tuliunda kamati ndogo iliyo chini ya Mwenyekiti Dk. Aley (Dk. Nassor Aley) ambaye ni mhadhiri pale SUA Zanzibar, na huyu ndiye aliyesoma maoni ya wengi.

“Hili nalo Maalim Seif limemuudhi kwani katika mahojiano yake alimsema vibaya Dk. Aley na kitendo hicho kimemdhalilisha Dk. Aley ambaye ni msomi wa chuo kikuu na ni mtu mwenye mawazo yasiyoshurutishwa na mtu.

“Nimesikitika sana kwa wadhifa wa Maalim kumdhalilisha Dk. Aley ambaye anatoa mchango wake vizuri, hajayumba katika msimamo wake na si busara hata kidogo kumdhalilisha, namwomba amwombe radhi,” alisema.

Kwa mujibu wa Hamad, kitendo cha kumsema vibaya Dk. Aley kinamjengea chuki kwa Wazanzibari, na kwamba kiongozi mzuri ni yule anayewaunganisha watu badala ya kuwatenganisha.

Kuhusu msimamo wake juu ya kauli alizodai ni za udhalilishaji, alisema atafikisha suala hilo mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

“Maalim alidai mimi ni dalali wa CCM, hili nimemwachia mwanasheria wangu alifanyie kazi kwa ajili ya kulifikisha mahakamani ili akathibitishe udalali wangu ulivyo.

“Maalim Seif ni mtu wa kuropokaropoka tu kwani hata mwaka 1995 alimsingizia Dk. Salmin, kwamba anataka kumuua na alifanya hivyo kupitia BBC, lakini alipotakiwa kutoa ushahidi, akashindwa kuutoa.

“Kuna viongozi wengine wako kama popo, yaani popo hajulikani kama ni ndege au mnyama, mtu anasema anataka Serikali ya mkataba na wakati huo huo anasema anataka Serikali tatu, haiwezekani.

“Kwa hiyo, nasema Katiba hii itapita na kwa kuwa sijawahi kusema nitagombea urais, sasa natangaza nitagombea urais wa Zanzibar.

“Nilitaka kugombea ukatibu mkuu ukanitimua, sasa nitagombea urais Zanzibar wala usiingie kiwewe. Najua unasema nina uchu wa madaraka, lakini ujue mimi sijawahi kugombea urais mara nne,” alisema Hamad na kupigiwa makofi.

Katika mazungumzo yake, Hamad alisema aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini na hakuwahi kukumbwa na kashfa yoyote na kwamba uadilifu huo ameendelea nao hata kwenye kamati za Bunge Maalumu la Katiba.

Pamoja na hayo, mwanasiasa huyo alizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Bunge na kuwaambia kuwa atagombea urais kupitia Chama cha ADC.

“Maalim ananitafuta sana, kwahiyo, mimi kama mwanasiasa baada ya kupata ile ‘pratform’ bungeni, nikaona ni busara niitumie kusema.

“Nimetumia fursa hiyo kusema yote hayo na wala sijamkosea Maalim Seif ila yeye ndiye amenikosea adabu.

“Kisiasa kuna njia mbili za kugombea, naweza kugombea kama mgombea binafsi, lakini kwa kuwa kuna kile chama cha ADC ambacho mimi ni mlezi wake, nitagombea kupitia huko,” alisema.

Chamzo Mtanzania


No comments:

 
 
Blogger Templates