Dar es Salaam. Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi amepongeza jinsi mchakato mzima wa Katiba Mpya ulivyoenda na kupongeza uamuzi uliofanywa wa kusitisha mchakato huo hadi baada ya Uchaguzi Mkuu.
Sebregondi alisema hayo jana alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Ltd inayochapicha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen.
“Kwa mtazamo wangu tangu kuanza kwa mchakato huu nimeshuhudia mambo mengi mazuri yaliyofanywa katika ngazi mbalimbali.
Moja likiwamo lile la ukusanyaji wa maoni kupitia Tume ya Jaji Warioba iliyokuwa imeundwa kwa ajili ya kukusanya maoni kwa wananchi nchi nzima. Hilo lilikuwa jambo jema kwa sababu limeonyesha umuhimu wa wananchi kwa kuwapa nafasi ya kutoa maoni yao kwa ajili ya Katiba Mpya,” alisema.
“Kazi iliyofanyika ni kubwa na nzuri. Pia, kuundwa kwa Bunge Maalumu la Katiba ambalo ndilo lilikuwa likijadili rasimu hiyo ya Katiba kutokana na maoni yaliyokuwa yamekusanywa kutoka kwa wananchi.”
Jana, Bunge la Katiba lilihitimisha kazi yake baada ya kutangaza matokeo ya kura za kupitisha Rasimu. Kwa mujibu wa makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na TCD, mchakato huo utaendelea baada ya uchaguzi mkuu mwakani.
Licha ya pongezi hizo, balozi huyo alisema, mchakato huo umeleta matabaka baina ya wajumbe wa Bunge hilo hasa lilipokuja suala la muundo wa Serikali. Hali hiyo ilisababisha wajumbe wanaounda Umoja wa Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge Aprili mwaka huu.
Akizungumzia suala la Muungano, Sebregongi alisema haoni haja ya kuvunja Muungano kwani watu wakifanya mambo kwa umoja wanaweza kupiga hatua zaidi katika mambo muhimu ya maendeleo.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment