MIAKA kadhaa iliyopita Chama cha Wananchi (CUF) kilikuwa na sera au kaulimbiu za ‘ngangari’ na ‘jino kwa jino’.
Nakumbuka Uchaguzi Mkuu wa 2000 hadi 2005 sera hiyo ilikuwa katika kilele chake. Ukienda katika mikutano viongozi waliwasalimu wanachama kwa: ‘CUF’ ngangariii’ ‘vijana ngangariiii’, ‘akina mama ngangariii’. Wafuasi nao walijibu: ‘ngangariiii’.
Ukiacha salamu hizo, kulikuwa na nyimbo na vidokezo vilivyobeba ujumbe wa jino kwa jino uliotumika kuhamasisha wanachama, wafuasi na wapenzi wa chama hicho katika mikutano, maandamano na shughuli nyingine za kichama.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa CUF, Abdul Kambaya, ngangari neno ambalo maana yake ni ukakamavu au kwa lugha ya vijana ‘kukomaa katika jambo fulani’; na ‘jino kwa jino’ msemo ambao unahimiza kulipa ubaya kwa ubaya (kisasi); ni kaulimbiu zilizoanzishwa kwa nia nzuri.
Akielezea maana ya kaulimbiu hizo, Kambaya anasema ‘ngangari’ na ‘jino kwa jino’ zilikuwa ni kaulimbiu zilizohimiza ukakamavu katika kudai haki, na kwamba ni wapinzani wao CCM na vyombo vya habari vilivyopotosha tafsiri ya kaulimbiu hizo.
Tafsiri mbaya anayoizungumzia Kambaya ni ile taswira iliyojengeka katika jamii juu ya CUF ya miaka ile ambapo baadhi ya wananchi walikichukulia (baadhi hadi sasa) kuwa ni chama cha kigaidi kinachoendeleza siasa za visasi, fujo, vurugu, matusi, ubabe na uvunjifu wa amani.
CCM ilitumia vema kaulimbiu hizo tata za CUF zilijojenga taswira mbaya mbele ya jamii kujinufaisha kisiasa kwa kukishambulia chama hicho kila walipopata nafasi. CCM walihakikisha wanaaminisha na kuimarisha taswira ya CUF kama chama cha kigaidi kwa kutumia kila aina ya hoja. Hata rangi nyekundu katika bendera ya CUF ilitajwa kuwa ni ushahidi kuwa ni chama kinachokusudia kumwaga damu.
Januari 27, 2001 taswira ya CUF kama chama cha kigaidi iliimarika zaidi baada ya kuendesha maandamano yaliyopigwa marufuku na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30 (kwa mujibu wa takwimu za CUF), hususan kule Pemba huku wengine kadhaa wakikamatwa na kushitakiwa.
Lengo la maandamano yale ilikuwa ni kuelezea kutoridhika kwa chama hicho na mchakato wa uchaguzi wa 2000 na baada ya hapo walichodai kuwa ni unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za biandamu.
Mabalaa yaliendelea kuiandama CUF pale ambapo siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Omar Mahita, alikutana na waandishi wa habari na kukituhumu CUF kwamba kimeingiza makontena ya visu na majambia kwa ajili ya kuchafua amani.
CUF, wakati huo kikiwa chama chenye nguvu zaidi miongoni mwa vyama vya upinzani, hakikupata hata nafasi wa kukanusha habari zile. Kulipokucha wananchi wote walikuwa wakizungumzia tukio hilo huku wakisubiri kupiga kura. Hata wana CUF wenyewe walichanganyikiwa wasijue kama habari zile ni za kweli ama la. Inasemekana wengi hawakujitokeza hata kupiga kura.
Hujuma hizi za CCM zisingefanikiwa bila CUF wenyewe kujenga msingi mbaya kwa kuanzisha na kutumia kaulimbiu hizi ambazo si tu zinaweza kutafsiriwa kama za kuchochea fujo lakini pia zinaenda kinyume kabisa cha falsafa ya moja ya dini kuu za Watanzania, ukristu, unaohubiri ukichapwa kofi shavu moja, geuza shavu la pili.
Kwa mujibu wa Kambaya, pamoja na CUF kuamini kuwa vyombo vya habari vimepotosha kaulimbiu hizo za ngangari na jino kwa jino, viongozi waliona umuhimu wa kujitathmini na kujiuliza kama kaulimbiu hizo zinakisaidia chama. Wakaamua kuachana nazo. Wakaamua wapunguze siasa za mapambano.
Pamoja na kutumia kaulimbiu hizo, si kwamba CUF haikuwa na wafuasi. Walikuwapo wengi ingawa si idadi ya kutosha kushinda uchaguzi mkuu.
Tatizo lililoikumba CUF ni kuwa haikuweza kuvutia wafuasi wapya, nje ya kundi la kijamii ambalo CUF kiasili ina ufuasi. Na hata kundi hilo ambalo CUF kiasili ina ufuasi si lote liliunga mkono chama hicho. Kwa mfano, inaaminika CUF imetaga mayai kusini mwa nchi na maeneo ya pwani, lakini mbona haijafanikiwa kupata wabunge wa kutosha maeneo hayo?
Kwa maoni yangu kulikuwa na tatizo katika taswira ambayo chama hicho kilijijengea kwa umma, taswira ya chama cha kigaidi na fujo. Taswira hii iliogofya makundi fulani ya kijamii. CUF imejaribu kubadilisha taswira hiyo iliyoogofya watu, ingawa ilishawagharimu huko nyuma.
Bahati mbaya ni kuwa CUF walichelewa kung’amua tatizo la taswira lililotokana na si tu kaulimbiu lakini hata baadhi ya vitendo vyao. CUF walichelewa kuona tatizo kwa sababu waliamini tayari wanaungwa mkono na Watanzania wengi.
CUF hawakujua kuwa katika siasa, kelele na kujitokeza kwa watu katika mikutano si kipimo cha ushindi. Unaweza kuwa na wafuasi wachache wenye mwamko mkubwa ambao wapo tayari kusafiri kila penye mkutano wa chama kupeleka hamasa. Unaweza kudhani unafanya kampeni kumbe unaimarisha tu imani ya wanachama wako.
Kutokana na matukio ya karibuni ni wazi kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nacho kinaelekea kupita njia ile ambayo CUF walishaijaribu, wakaiona haiwafai na kuamua kuiasi.
Sisemi kwamba lazima mkakati ulioshindwa kuisaidia CUF lazima ushindwe pia kwa CHADEMA, hasa ukizingatia tunalinganisha nyakati tofauti, vyama tofauti, viongozi tofauti, na hata uwezo tofauti wa kukabiliana na propaganda. Hata hivyo, ni vema CHADEMA wawe waangalifu.
Katika miaka ya karibuni, mikusanyiko ya CHADEMA imewahi kukumbwa na vurugu zilizosababisha mauaji katika maeneo kadhaa ikiwemo Arusha, Iringa na Morogoro, ingawa mara nyingi ni matendo ya polisi ya kuzuia mikusanyiko ndio ilikuwa chanzo cha fujo. Kadhalika, kumekuwa na jitihada za CCM za kuihusisha CHADEMA na matukio kadhaa ya kigaidi ikiwemo kutesa na kupanga mipango ya kuumiza watu (rejea video ya Lwakatare) na kadhalika.
Lakini, pamoja na jitihada za CCM za kukihusisha chama hicho na fujo, CHADEMA imeendelea kukua na kupata uhai kutokana na kazi yake ya kuhimiza maendeleo na kupambana na ufisadi na kwa hivyo imekubalika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, pamoja na Watanzania kuunga mkono CHADEMA na kukifanya chama kikuu cha upinzani kwa Tanzania Bara, ni muhimu chama hicho kitathmini mwelekeo wake na kuhakikisha hakipotezi umaarufu wake, kinakua zaidi na kuvutia makundi ya wafuasi nje ya makundi ya wafuasi wake wa sasa.
Je, mwelekeo wa kimapambano kinaouchukua sasa wa kuhimiza maandamano yasiyo na kikomo utakisaidia chama hicho kukua kisiasa ama la? Msimamo huo una faida? Hilo ni swali la msingi CHADEMA wanapaswa kujiuliza.
CUF ambao wamo katika muungano wa UKAWA si wajinga kunyamaza na kuwaachia CHADEMA waongoze maandamano.
Kwa CUF huu ni mkakati wa kisiasa unaotokana na miaka ya uzoefu wa siasa za mapambano. Walijifunza kuwa siasa za mapambano hazilipi.
Watanzania wengi wanapenda maendeleo sana lakini wanapenda amani zaidi. Hawa ndugu zangu Waswahili ninaoishi nao huku Magomeni, Dar es Salaam ukiwaambia maandamano ya kudai kuahirishwa Bunge la Katiba wanakuona chizi tu.
Hata marafiki zangu wa daraja la kati, wanaweza kukuunga mkono katika misimamo yako ya kudai serikali tatu lakini maandamano!? No way. .
Chanzo RaiaMwema
No comments:
Post a Comment