Alijifikisha macho ili apate ukweli kama tukio lililotokea mbele yake lilikuwa la kweli. Baada ya tukio lile Nargis alicheka kisha kwa upole alisema:
“Hongera umejitahidi lakini hapa ndipo mwisho wa matatizo, ila leo sikuja kwa shari nami nimekuja kama wateja wengine hivyo nataka msaada wako.” SASA ENDELEA...
Mzee Mukti akiwa bado mapigo ya moyo yapo juu na kijasho kiliendelea kumtoka, alijiuliza Nargis anataka msaada gani ikiwa tayari ameonesha ana uwezo mkubwa kuliko yeye. Huku akijitahidi kuficha hofu yake alimuuliza.
“U...u...una...taka m...m...saada gani ewe jini mwana wa mfalme wa bahari ya dhahabu?”
“Naomba kwanza suala la ujini liweke pembeni nami nakuja kama Subira alivyokuja, naitwa Nargis mke halali wa Thabit. Kwa hiyo nisaidie kama mwanadamu mwenye matatizo na si jini ndiyo maana nipo mbele yako kama mwanadamu.”
“U...unataka msaada gani?”
“Nataka unirudishie mume wangu mikononi mwangu.”
“Nimrudishe vipi?”
“Kama ulivyomtoa, najua umepewa fedha nyingi baada ya kuninyang’anya mume wangu. Nataka kukuambia ulichopewa na Subira, mimi nitakupa mara mia ili tu unirudishie mume wangu. Mimi kweli ni jini lakini nina haki ya kuishi maisha nitakayo bila kumdhuru kiumbe yeyote.
“Ni kweli mwanzo kabla ya kuwa mzazi nilikuwa sikubali kushindwa, nilipata dhambi nyingi kwa ajili ya kutoa roho za watu na majini kwa ajili ya kumlinda mume wangu. Lakini nimeona si lazima kutumia nguvu au kutoa uhai wa kiumbe kumlinda mume wangu.
“Kipindi hiki cha kumtafuta mume wangu nimekutana na vikwazo vingi toka kwako nina imani uwezo wako ndiyo uliomfanya Subira akupe zawadi nyingi za nyumba na magari. Nilikuwa na uwezo wa kuviteketeza vyote ulivyopewa lakini sikutaka kufanya hivyo kwa vile kwangu mali si muhimu kama mume wangu.
“Mali aliyokupa Subira ni yangu kwa vile hajui imepatikana vipi, mimi ndiye mmiliki wa mali yote aliyonayo Thabit. Kumbuka mali zote ziliteketezwa pamoja na uganga wako hukuweza kuzirudisha lakini nilizirudisha. Hata mume wangu alipopata matatizo usingeweza kumtibu, nilimtibu mwenyewe.
“Huoni jinsi gani ninavyomjali mume wangu pia ni mzazi mwenzangu, kwa hiyo ninacho kuomba kikubwa nirudishie mume wangu. Sema unataka nikupe kitu gani ili unirudishie mume wangu.
Hata wewe kama unasafiri kwenda nyumbani ukirudi ukute mkeo kipenzi kaolewa na mtu mwingine utajisikiaje tena kwa hila za huyo mwanaume? “Nina imani unajua maumivu yake kingine nimeteswa kwa haki yangu hivi hapa jini na mwanadamu nani mbaya?” Nargis aliuliza huku machozi ya uchungu yakimtoka na kuongeza uzuri wake mara kumi.
“Mzee Mukti kwa nini unamlisha chakula asichokipenda mume wangu? Kwa nini unamlisha haramu? Subira yupo na mume wangu kwa nguvu za dawa yupo kama ndondocha. Sitaki nirudi nilipotoka kwani uvumilivu una kikomo, waganga wengi walikufa kwa ubishi hivyo sitegemei na wewe kuwa hivyo.
“Lakini leo nimekuja kistaraabu, hivi mtu aliyedhamiria kukuua unaweza kuzungumza naye hivi?” Nargis alimuuliza mzee Mukti aliyekuwa amepigwa na butwaa macho yamemtoka pima.
“Nakuuliza mzee wangu, mara ngapi mmepanga mipango ya kuniua lakini mmeshindwa. Lakini leo nakuja kwako kistaraabu hivi, kweli?”
“Najua nazungumza maneno mengi bila vitendo,” Nargis alisema huku akinyanyuka kitendo kilichoongeza wasiwasi kwa mganga na kujua kumekucha.
Lakini ilikuwa tofauti kwa Nargis ambaye alishika mkono kichwani kwa muda kisha alipiga kofi. Ghafla walitokea viumbe wawili wamebeba mabegi mawili makubwa na kuyaweza mbele ya mganga. Baada ya kuweka Nargis alipiga kofi jingine lililowafanya viumbe wale kuyeyuka. Baada ya kutoweka Nargis alisema:
“Mzee wangu, huu ni utajiri ambao utautumia mpaka kufa kwako hata kizazi chako kitakufa na kuuacha. Nina imani njaa ndiyo inayowafanya waganga wengi wawadhuru wasio na hatia. Nina imani nimeona jinsi gani ninavyompenda mume wangu.”
Nargis alisema huku akifungua yale mabegi, moja lilikuwa limejaa fedha za mataifa mbalimbali na lingine lilikuwa na mchanganyiko wa madini yote ya thamani.
“Sasa mama unataka msaada gani?” Mzee Mukti alichanganyikiwa na mali iliyokuwa mbele yake.
“Kunirudishia mume wangu.”
“Unataka nimfanye nini Subira?”
“Sitaki umfanye kitu chochote kibaya, ninachotaka liondoe tandaburi ulilomvilingishia mume wangu ili arudi kwenye akili yake ya kawaida anitambue kama mimi ni mkewe wa halali. Najua kwa sasa umeifunga akili yake asinikumbuke na kufanya aamini kabisa mkewe ni Subira.”
“Nitafanya hivyo, nakuahidi kazi hiyo nitaifanya mwenyewe.”
“Sitaki uifanye wewe, nataka aifanye Subira mwenyewe kama alivyofanya mwanzo.”
“Sawa nimekuelewa.”
“Nina imani tutakwenda vizuri kama utafanya ninavyotaka.”
“Nakuahidi kufanya kila ulichonieleza.”
“Nitashukuru, naomba nikuache uendelee na wateja wengine.”
“Hapana leo nitakuwa na kazi yako tu.”
“Kuja kwangu kusiwe chanzo cha wengine kukosa huduma, najua lazima Subira atakuja hivyo utaanza hapo ila sasa hivi wahudumie wagonjwa wengine.”
“Nashukuru kwa huruma yako.”
Kama alivyoingia ndivyo alivyotoka katika umbile la kibinadamu na kuwaaga wagonjwa wengine waliokuwa kwenye foleni. Baada ya kutoka Mukti alishusha pumzi ndefu asiamini kilichotokea.
Itaendelea
Chanzo globalpublishers
No comments:
Post a Comment