“Angalia pale...” akasema akisonza kidole kwenye ukuta ambao kulikuwa na ngozi ya mnyama.
Sikujua ni mnyama gani!
Nikaangalia!
Nilishuhudia mambo ya ajabu ya kushangaza. Hofu kuu ikanijaa, nikazidi kukodoa macho yangu. Mwili mzima ulitetemeka.
SASA ENDELEA...
Ngozi ile ya mnyama ukutani ambayo kwa kuiangalia ilifanana na ya Fisi ingawa sikuwahi kumwona zaidi ya picha zake na wakati mwingine kwenye runinga, ilikuwa ni kama runinga, kila kitu kilionekana kama naangalia filamu fulani ya kutisha.
Ulikuwa ni wakati wa usiku, chini ya mti mkubwa wa Mbuyu, watu wote wakiwa kama walivyozaliwa, wameshikilia vibuyu mikononi mwao. Usoni wakiwa wamepaka dawa nyeusi iliyofanana kabisa na masizi, hakika niliyokuwa nikiitazama kwenye runinga ya ngozi ya Fisi, ilikuwa ni tafrija ya wachawi usiku wa manane.
Maiti za walioonekana ni kama watoto wachanga zilikuwa zikiletwa na kuwekwa juu ya jiko kubwa lililokuwa likiwaka moto kama makaa ya mawe kwa jinsi ulivyokuwa mkali, muda mfupi tu baadaye maiti hizo zilikuwa zikidondosha mafuta mengi zilikauka kisha kushushwa zikiwa bado za moto, bibi vizee wakakamata miguu na kuichana katikati, kisha kuanza kula kwa furaha kama vile walikuwa wakila nyama nyingine yoyote, hawakujali kabisa kwamba ilikuwa ni maiti.
Awali sikuelewa ni kwa nini Mukulungu aliamua kunionyesha tafrija ile, lakini baadaye watu hao walipoanza kunawa nyuso zao ndipo nilielewa, baba yangu mzazi mzee Matima Matimandole alikuwa ni miongoni mwao! Nikashika mikono yangu yote mdomoni kwa mshangao, sikuwahi hata mara moja kuwaza kwamba baba yangu alikuwa mchawi, kwani alikuwa mcha Mungu kupita kiasi.
“Babaaa? Mchawi?” nilijikuta natamka maneno hayo.
“Ndiyo! Baba yako alikuwa mwenzetu, kwenye chama chetu, alishaua watu wengi mno, kama sharti ili mimi nikiachia ngazi yeye aendelee, lakini ghafla alipotakiwa kukutoa wewe kafara, ili achukue cheo akakataa na kuanza kusali kanisani, jambo ambalo sisi halikutufarahisha, tukaamua kumuua! Tunachotaka kufanya ni kusaini mkataba wetu wa uchawi, usipofanya hivyo hata wewe tutakuua!”
“Je, mnaona kufanya hivyo ni sawa?”
“Ndiyo, lazima uwe mchawi, ili siku moja ukikalie kiti hiki ninachokikalia mimi maana baba yako alikistahili, mrithi ni wewe.”
“Siwezi!” nilisema na hapo hapo runinga ya ngozi ukutani ikazima, Mukulungu akatoka kwenye kiti chake na kunisogelea akionekana kabisa kuvimba kwa hasira.
“Umesemaje?”
“Siko tayari kufanya mambo ya aina hii kama ni kufa acha nife, lakini nisiwe mchawi.”
“Yaani pamoja na kuongea muda wote huo bado hujaelewa?”
“Sitaelewa.”
“Sasa sikiliza, nakuachia uende nyumbani ukafikirie, huwezi kutukimbia sisi, himaya yetu ni kubwa mno tutakufikia wakati wowote tukikuhitaji.”
Baada ya kusema maneno hayo Mukulungu aliondoka na kupotelea gizani, hapohapo nikafumbua macho na kujikuta nimelala kando ya mke wangu Rita, akiendelea kugugumia kwa maumivu makali, damu nyingi zikimtoka sehemu za siri na kulowanisha mashuka.
“Darling yaani kweli mimi nateseka na maumivu wewe umelala usingizi?” Rita aliongea.
Hakuwa kabisa na picha ya mahali nilipokuwa, kwenye ulimwengu usioonekana kwa macho ya kawaida, nikipambana na Mukulungu akinishawishi nitie saini mkataba wa kuwa mchawi jambo ambalo sikuwa tayari kulifanya.
Hakika nilikuwa nimejifunza mambo mengi ambayo sikuwahi kuyafahamu, taswira ya baba yangu mzazi akiwa utupu huku akila maiti za watoto bado ilinitisha kila nilipoikumbuka. Ukweli kwamba mimba za mke wangu mpenzi zilizokuwa zikitoka ilikuwa ni adhabu sababu baba alisaliti wachawi wenzake uliniumiza sana lakini sikuwa na uwezo wa kumsimulia Rita, nikaahidi ingebaki kuwa siri yangu.
“Nipeleke hospitali, ona ninavyovuja damu nyingi!”
Nikajikusanya haraka na kuanza kuvaa nguo, nilipomaliza nilitoka nje hadi nyumba ya jirani ambako aliishi mwanaume mmoja mwenye moyo safi, nikagonga kwenye lango kubwa, mlinzi akafungua na nikamweleza shida niliyokuwa nayo, akanyanyua simu na kumpigia bosi wake aliyekuwa amelala, saa iliyokuwa imetundikwa ukutani ndani ya kibanda cha mlinzi ilisomeka saa tisa na nusu.
Muda mfupi baadaye mwanaume huyo mwenye umri kati ya miaka hamsini na sitini alitoka ndani ya nyumba yake akiwa amevalia bukta na shati tu, akanisabahi nami nikampa heshima yake kisha kumsimulia mateso ambayo mke wangu alikuwa akiyapata.
“Yuko wapi?”
“Nyumbani kwangu.”
“Mnaishi nyumba ipi kweli?”
“Pale kwa mzee Mwinyimkuu, tuko banda la uani.”
“Subiri.”
Akarudi ndani ya nyumba yake akikimbia, nikagundua alikuwa amefuata ufunguo wa gari, mawazo yangu yakawa sawa kwani aliporejea muda mfupi baadaye alinitaka niingie garini na kurudi kinyumenyume kisha kuendesha kwa kwenda mbele hadi mbele ya nyumba tuliyoishi, tukashuka naye hadi kwenye banda letu la nyuma ambako tulimsaidia Rita kuvaa kisha kumbeba hadi kwenye gari, nguo zote zikiwa zimelowa damu.
Safari kwenda hospitali ikaanza, kichwa changu kikiwa kimejawa na mawazo mengi ya vitisho vya mzee Mukulungu na serikali yake ya Kichawi, sikujua jinsi ya kujinasua kutoka kwenye mtego huo lakini jambo nililoelewa ni kwamba sikuwa tayari kusaini mkataba wa kichawi na kuanza kuua watu.
inaendelea
No comments:
Post a Comment