Social Icons

Sunday, 12 October 2014

HADITHI: Usilie Nadia -5



BAADA ya cappuccino kutuburudisha vyema na kutupunguzia baridi kwa kiasi fulani, tuliamua kuunganisha na chakula kabisa.
Nadia akaagiza mchemsho wa kuku, mimi nikaagiza ugali na samaki aina ya sato wa kuchoma. Hiki chakula kilikuwa ni kama kaugonjwa kwangu.
Kila mmoja akajikita katika kusosoa kivyake chakula kile. Hakuna alitemsemesha mwenzake, Nadia alikuwa na staha haswaa katika kula, hakuwa akitafuna huku akiacha kinywa wazi. Alijua kuishika uma vyema na nzuri zaidi hakusema sema wakati anakula. Makosa ambayo wasichana wengi hujikuta wakifanya bila kujua kama ni makosa.
Baada ya dakika hamsini tulikuwa tunanawa mikono. Hapakuwa na jipya jingine tukaelekea nje ya hoteli ile kulitazama kidogo jiji la Mwanza. Ilikuwa ni saa tatu usiku, na jiji la Mwanza lilikuwa bado katika heka heka za hapa na pale. Kila tulichokiona na kikafaa kuzungumzwa tulifanya hivyo. Hadi tulipokifikia kijiwe kimoja cha kahawa, Nadia aliomba tuketi kidogo.
Sikumpinga maana maana kidogo alionyesha kuchakaa uso waker ghafla, bila shaka alikuwa amevamiwa na wazo la ghafla.
Nikaiandaa simu yangu katika sehemu ya kurekodia.
“Duniani kuna mengi sana, na huwezi kuijua kesho yako iwapo leo tru kuimaliza hujui itamalizika vipi. Na katika kitu kinachosababisha tusiijue kesho yetu ni wanadamu wabaya wasiokuwa na huruma kwa wenzao. Nimewahi kuumia sana katika maisha yangu, nimeumia sana baada ya kusikia mama yangu amekufa kwa ajili yangu eti kisa tu mwanaume ambaye nilimpenda kwa dhati nikitarajia atakuja kuyafuta maumivu yangu. Lakini siku nyingine ambayo niliumia sana ni pale ambapo niligundua kuwa sijaipoteza familia yangu tu bali hata wale marafiki ambao nilikuwa nawategemea nao walikuwa kinyume na mimi. Sikutarajia kabisa ingekuwa rahisi kiasi hicho mimi kujikuta katika mji huu nikiwa mpweke, yaani wakati mwingine najilaumu mimi mwenyewe kwa tabia yangu ya kutochangamana na wanafunzi wengine kwa ukaribu zaidi ya marafiki zangu wanne tu. Sikujua kuwa siku moja nitawahitaji na hawatakuwa tayari kunisikiliza kabisa.” Alisita kisha akatazama huku na kule akapepesa macho kisha akaendelea.
“Yaani Desmund alikuwa mjanja hakika katika hili, yaani akanitoa Musoma na kunitupa jijini Mwanza kisha akaniacha huku akiwa ameharibu kila kitu. Desmund alikuwa amecheza karata sahihi kabisa, yaani akanitelekeza Mwanza bila msaada wowote, usiku nikalala nje kisha asubuhi nikaenda kuwatafuta marafiki zangu ni huku nilipokutana na kituko cha mwaka…..yaani kweli rafiki zangu niliosoma nao miaka mitatu chuoni wakaaminishwa kuwa mimini mshirikina, nina majini ambayo ni hatari sana katika mwili wangu? Marafiki wakanikataa eti mume wangu amewaonya wasije kumlaumu wakinikaribisha, niliwalilia na kuwasisitiza kuwa sijui hata hayo majini yanafanana vipi nikawaomba wanipe nafasi ya kunisikiliza lakini hilo halikuwezekana, kila mmoja alidai kuwa anaogopa majini na yanaweza kuhamia kwao.
Nikajikuta nikiwa yatima kamili jijini Mwanza, mbaya zaidi baba yangu alinifanyia komesho alipoamua kuteketeza vyeti vyangu vyote kuanzia awali hadi chuo kikuu.
Nikawa naonekana kituko rasmi, Desmund akawaambia rafiki zangu kuwa majini yalinipanda nikachoma vyeti vyangu.
Ama kwa hakika Desmund aliniweza.
Jijini Mwanza ningeishi vipi sasa iwapo hakuna mtu ambaye alihitaji kunisikia? Ningekimbilia wapi mimi Nadia.
Nikisema kuwa ipo siku nililia ni ile siku yangu ya kwanza kugawa penzi ili nipate pesa ya kujikimu, eneo lenyewe ni lile pale mbele, siku ya kwanza sikupata mtu wa kuninunua ni hapa nilipokutana na Jadida, msichana ambaye sikuwahi kuona tabasamu wala cheko lake isipokuwa siku moja tu, siku ambayo sitaisahau kamwe. Jadida akanichukua usiku ule na kunipeleka katika chumba ambacho alikuwa anaishi yeye na machangudoa wengine. Jadida aliniuliza maswali mawili matatu, nikamueleza kijuu juu kuhusu uwepo wangu eneo lile nikalalamika kuwa ni njaa na sina ndugu yeyote wa kunifadhili. Akanitazama vizuri, nikayaogopa macho yake ambayo yalitangaza chuki waziwazi. Kisha akachukua mkate na juisi akanipatia. Nilipomaliza kula akanipatia maji kidogo nikaoga.
Siku iliyofuata akanipamba kidogo na kisha usiku akawa kiongozi wangu nikijipanga katika barabara kwa ajili ya kusubiri wateja, mteja wangu wa kwanza alikuwa mswahili tu. Sikuamini kama yalew yote yanatokea kwa sababu tu nilimkabidhi moyo wqangu Desmund. Usiku ukamalizika nikiwa nimepata watejawanne. Jadida akawa meneja wangu rasmi.
Kama yeye ambavyo alikuwa hatabasamu basi name sikuwahi kuifurahia siku hata moja ya biashara hiyo. Yaani Desmund hakujishughulisha kunitafuta? Desmund huyu huyu ambaye alikuwa na kitambi kutokana na pesa zangu leo hii amenitupa bila msaada wowote, akaniacha niwe changudoa, akanishutumu kuwa nina majini. Siku ambayo niliamua rasmi kuachana na uchangudoa ulikuwa usiku wa saa nne ambapo nilichukuliwa na mwanaume ambaye alikuwa na asili ya kihindi lakini alionekana kuwa mswahili sana. Huyu alilazimisha niende naye gesti jambo ambalo dada Jadida alinikataza kabisa nisikubali, lakini kutokana na pesa aliyoitoa basi Jadida akaniruhusu niende naye tu. Hii ilikuwa baada ya kuhahakikishiwa usalama wangu.
Sikujua kama yangeweza kutokea mambo ya ajabu kama yale yaliyotokea siku ile.
Tulifika vizuri chumbani, nilijiweka sawa kumridhisha kisha biashara iishie hapo, kweli nilifanya yote aliyoyataka, sikuwa nimewahi kulala na mteja gesti huyu alikuwa wa kwanza akataka nimfanyie kila jambo ambalo huwa namfanyia mwanaume ambaye ni mpenzi wangu mimi nikatii yote haya, kila alivyorudia maneno hayo kuwa yeye ni mume wangu kwa siku hiyo basi alinikumbusha sana kuhusu Desmund wangu, nilitamani sana dunia inimeze lakini cha ajabu nilikuwa sijisikii kabisa hata dalili ya kupata wazo la kujiua.
Baada ya kumfanyia kila kitu kinachoitwa mapenzi lilifuata jambo ambalo lilinifanya kwa mara ya kwanza nimchukie Desmund kabisa na kutotamani kumuona tena maishani. Yule mwanaume akanilazimisha kufanya mapezni kinyume na maumbile, nilibishana naye sana nikagoma kabisa nikidhani atanielewa kama alivyoonyesha usoni kuwa ni mpole. Haikuwa hivyo, mara akaiendea suruali yake. Yule bwana alikuwa na bunduki, kwa mara ya kwanza nikatazamana na bunduki!!! Hakika niliishiwa nguvu. Akaniambia nichague moja tu, kufanya atakavyo ama kuniua palepale. Mwandishi kifo ni kitu kingine na hakika hakizoeleki yaani sikuwa tayari kufa.
Akanivamia pale na kuniambia nikifanya kipingamizi chochote tu ananisambaza ubongo wangu….yaani niliumia, nililia mtangazaji nililia na kumlaani Desmund kwa kila neno nililoweza kusema, sijui kama dua zangu zilifika kwake sijui kabisa kama Mungu alikuwa anatega sikiona kunisikiliza walau kidogo tu! Nililalamika sana siku hiyo.
Nadhani nilipoteza fahamu, maana asubuhi nilijikuta peke yangu, maumivu makali nikashindwa kukaa vizuri, nikaanza kulia upya. Mara mlango ukagongwa. Ilikuwa imetimu saa nne asubuhi.
Muda wa kukabidhi chumba, nilipogeuka kutazama mashuka nikakutana na matone ya damu. Nikamuomba yule dada dakika mbili nivae akaniruhusu huku akisisitiza kuwa ziwe dakika mbili kweli. Nilihaha nisijuie nini cha kufanya, mwisho nikaamua kujikabidhi tu kwa muhudumu nikamueleza kuwa nimeingia katika siku zangu ghafla na nimechafua mashuka.
Hakutaka kunielewa mwisho nikaamriwa kuyafua mashuka yale, nikafanya walivyotaka. Huku maumivu makali yakitambaa katika mwili wangu. Jina la Desmund likichemka katika kichwa changu. Nikamlaani tena asubuhi ile, nikamwombea mabalaa yote yamwandame, hadi ninavyozungumza nawe nitaendelea kulalamika kuwa Mungu hakutega sikio kunisikiliza, angenisikiliza kweli yasingenikuta haya. Sijui hata ni wapi mimi Nadia niliwahi kumkosea Mungu wangu!!! Niliondoka nikiwa nachechemea hadi nikafika nyumbani kwa Jadida. Aliponiona klwa mbali tu alijua kuna tatizo akanikimbilia kwa kasi.
“Nadia..amekufanyaje yule mteja..nimekutafuta sana..” aliniuliza huku akiwa amenikamata mabega. Badala ya kumjibu nilianza kulia, nililia sana akanituliza mwisho nikamwambia kilichojiri.
“Ame….amekufanyaje…yaani…” alishindwa kuzungumza akaanza kutetemeka na kwa mara ya kwanza nikaliona chozi la Jadida….
Afadhali alilia tukalia wote nikahisi yupo mtu aliyeutambua uchungu wangu…..si Desmund aliyeniharibia maisha yangu. Katika zungumza yangu na Jadida nilijikuta kwa hasira nikimweleza mambo mengi sana kuhusu mimi, nilimweleza huku ninalia. Na ni katika siku hii nilipoweza kutambua Jadida alikuwa msichana wa aina gani yaani alikuwa zaidi ya changudoa. Na kubwa zaidi alikuwa akinifaa kabisa, alinibadili kiuelekeo akanibadili kifikra akayafuta machozi yangu na kisha akanionyesha njia ambayo sikujua kama ni mbaya ama ni nzuri hadi nilipoamua kuifuata…..” Akasita kidogo kisha akaendelea….
“Waliosema wema hawagandi alikuwa na maana yake, wema huyeyuka upesi. Jadida ambaye alikuwa mwanga wangu naye akapotea katika namna ya ajabu, hivi yawezekana mimi nilikuwa na bahati kuwa walinifanya vile kisha wakaniacha hai. Jadida…aaah Jadida yaani wakakufanyisha mapenzi kinyume na maumbile kisha wakakuua, hivi uliwaamini kwa nini watu wale, kwanini uliwaamini Jadida. Kumbe Jadida nawe hukuwa nma ndugu, serikali ikakufukia kama mzoga tu…ni mkimi pekee niliyesikitika wengine walisema alikufa akifanya uchangudoa….Jadida ambona uliondoka mapema sasa eeh!!” hapa hakuweza tena kuongea, alikuwa ameuma meno yake kwa hasira sana. Na machozi yalikuwa yanamtiririka.
Upesi nikaita taksi, ikatupakia na kuturudisha hotelini.
Nikiwa natazama mbele nilikuwa nawaza na kuwazua. Mkasa huu ulikuwa mtata kweli, ulikuwa mkasa unaozua maswali mengi na majibu machache.

itaendelea

No comments:

 
 
Blogger Templates