Rais Uhuru Kenyatta yuko njiani kuelekea mjini The Hague kuhudhuria kikao maalumu kuhusu kesi inayomkabili ya vurugu zilizosababishwa na mvutano kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2007.
Kenyatta, ambaye ni kiongozi wa kwanza aliyeko madarakani kufikishwa mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa, aliondoka uwanja wa ndege jijini Nairobi siku ya Jumanne (7 Oktoba) kwa ndege ya kawaida ya abiria kuelekea Amsterdam, Uholanzi, akiandamana na ujumbe mdogo unaowajumuisha mkewe na mwanawe wa kike pamoja na wabunge sita na mawaziri watatu.
Kwenye uwanja huo wa ndege, Kenyatta aliagwa na aliagwa na wafuasi wake wachache.
Kinachompeleka Kenyatta katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague ni kwenda kusikiliza hoja na tathmini kuhusu kesi inayomkabili ikimuhisisha na ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, ambazo zilizoendelea hadi mwaka 2008 na kusababisha kiasi cha watu 1,200 kuuwawa na wengine 600,000 kuachwa bila makaazi.
Akabidhi madaraka
Jumatatu (6 Oktoba), rais huyo wa Kenya alikabidhi madaraka kwa muda kwa makamu wake, William Ruto, ambaye naye pia anakabiliwa na kesi kama hiyo huko huko The Hague. Ruto anachukua majukumu ya kuiongoza nchi hiyo yenye uchumi mkubwa katika eneo la Afrika ya Mashariki.
Rais Kenyatta, mwenye umri wa miaka 52, anakabiliwa na mashitaka matano mbele ya mahakama hiyo, yakiwemo ya kupanga ghasia hizo mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katikahHistoria ya uchaguzi nchini mwake. Kenyatta aliwahi kufika mbele ya mahakama hiyo, lakini wakati huo alikuwa bado hajaingia madarakani. Alichaguliwa rais Machi 2013.
Kumbukumbu za baada ya uchaguzi 2007
Baada ya ghasia hizo za mwaka 2007/2008, aliyekuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Moreno Ocampo, alianzisha uchunguzi na baadaye kufungua kesi dhidi ya maafisa wanne wa serikali ya Kenya pamoja na mwandishi mmoja wa habari.
Maafisa hao walikuwa ni aliyekuwa kamishna wa polisi wakati huo, Mohammed Hussein Ali, aliyekuwa waziri wa viwanda, Henry Kosgei, makamu wa rais wa sasa, Ruto, na aliyekuwa waziri wa fedha, Kenyatta. Mwandishi wa habari aliyeunganishwa kwenye kesi hiyo ni Joshua Arap Sang.
Lakini mwaka 2010, kesi dhidi ya Kosgei ambaye pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa chama cha ODM kilichokuwa sehemu ya serikali ya mseto baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, na ile ya Ali, zilitupiliwa mbali baada ya kukosekana mashahidi.
Bensouda ailaumu serikali ya Kenya
Tayari Mwendesha Mashtaka Mkuu wa sasa wa ICC, Fatou Bensouda, ameshasema wazi kwamba hana mashahidi wa kutosha kuunga mkono kesi hiyo dhidi ya Rais Kenyatta, ingawa pia amekuwa akiitupia lawama serikali ya Kenya kwa kushindwa kushirikiana na mahakama hiyo kuifanikisha kesi hii.
Kwa Wakenya bado kumbukumbu ya kilichotokea katika ghasia hizo mbaya kabisa hazijafutika na hasa baada ya kugeuka na kuwa uhasama wa kikabila na kuichafua sura ya taifa hilo la Afrika ya Mashariki lililokuwa likionekana kama mfano mwema katika suala la usalama.
Vurugu ziliibuka baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kumtuhumu aliyekuwa rais wakati huo, Mwai Kibaki, kuiba kura kuingia tena madarakani na matokeo yake kilichoanza kama vurugu za kisiasa zikageuka kuwa mauaji ya kikabila na kulipizana kisasi. Kenya haikuwa imewahi kushuhudia wimbi kubwa la ghasia kama hizo tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1963.
Magazeti ya nchini Kenya yametangaza kuunga mkono hatua ya Kenyatta ya kujipeleka The Hague, yakisema kwamba kukataa kufanya hivyo huenda kungelisababisha athari kwa nchi nzima.
chanzo dw.de
No comments:
Post a Comment