Social Icons

Sunday, 25 January 2015

Hadithi: Familia Tata. 4


huku akigonga kwa nguvu mlango, hakukuwa na majibu.
“Inabidi uvunjwe,” askari alisema. Mzee Komba akatikisa kichwa kukubali. Kazi hiyo ikafanyika, kitasa kikavunjwa na mara mlango ukawa wazi.

Tonny alionekana akiwa amelala sakafuni.
SASA ENDELEA...

ASKARI alimsogelea Tonny, akamwangalia vizuri usoni mwake, mwili ulionekana kuloa maji. Mzee Komba naye akaingia chooni na kumtazama mwanaye. Askari akamgeuza uso ukatazama juu.
Dr Junior, jirani yao ambaye kwa muda wote amekuwa karibu na tukio hili, akawaomba wambebe kijana huyo na kumtoa nje, kwa sababu ya nafasi ndogo ndani ya choo.

Tonny akatolewa na kulazwa kwenye korido. Dr Junior alimtazama, akamshika kifuani kupima mapigo ya moyo wake.
“Amepoteza fahamu, nadhani ataamka baada ya muda mfupi,” aliwaambia watu ambao sasa walishakuwa wengi ndani ya nyumba ya mzee Komba.

“Apepewe,” askari aliamuru na mara moja, ndugu zake Tonny wakaanza kumpepea kwa khanga na vitenge.
Baada ya dakika chache za kupepewa, Tonny alijitingisha, dalili kuwa fahamu zinaanza kumrejea, kisha akafunua macho, akainuka na kukaa. Wote walimtazama kwa hofu.

“Unajua nini kimetokea?” Baba yake alimuuliza mwanaye huku ameingiza mikono kwenye mifukoni ya suruali yake.
“Ndiyo baba,” Tonny alijibu, machozi yakimlengalenga machoni mwake.
“Nini kimetokea?,” mzee Komba alimuuliza tena.
“Kule kwa kina Juddy baba….,” Tonny akashindwa kumalizia, akaanza kulia kwa sauti.

“Mbadilishieni nguo,” askari alisema, akachukuliwa na kuingizwa ndani, akabadilishwa nguo.
“Mzee, poleni kwa matatizo, inauma sana. Hata hivyo, huyu kijana itabidi twende naye kituoni kwa mahojiano zaidi. Mambo mengine nadhani mtayajua huko,” askari alimweleza mzee Komba aliyetingisha kichwa kukubaliana naye!!!

***
Baada ya gari la polisi kuondoka alfajiri ile, huzuni ilirejea upya. Mama yake Tonny alikuwa akilia pamoja na mama Juddy, ni tukio ambalo halikutarajiwa na liliwagusa wote kwa pamoja. 
“Dada hata sijui nikuambie nini, naumia sana yaani..,” mama yake Tonny alimwambia mama Juddy, akimfuta machozi wakati yeye mwenyewe akiwa analia.

“Usijali dada, mipango ya Mungu, ni bahati mbaya, sote nafsi zetu zitaonja mauti,” naye alimjibu mwenzie, kitu ambacho kilimfariji sana.
Siku hiyo ilitumika kusambaza habari kwa ndugu jamaa na marafiki sehemu zote duniani. Msiba huo uliwashtua watu wengi. Aliyeumia zaidi alikuwa ni Asfat, dada yake Tonny aliyekuwa swahiba mkubwa wa Juddy.

Alikuwa Birmingham nchini Uingereza anakosoma, akisubiri kupanda treni kuelekea London kumpokea shosti wake alipopokea simu ya kaka yake, Amani. Ilikuwa ni saa moja na nusu asubuhi kwa saa za huko.
“Usiniambie ameshapanda ndege tayari kaka,” Asfat alimwambia Amani mara tu alipoweka simu yake sikioni.

“Si bora hata angepanda baadaye, hatapanda tena,” Amani aliongea kwa sauti ndogo, yenye majonzi, iliyomshtua sana dada yake.
“Heee, imekuaje tena kaka Amani mbona unanishtua, baba amegoma kwani…,” aliuliza kwa hamaki.
“Dah, dada wee acha tu, Juddy amefariki,”

“Ni...ni...ni...?!!
Amani alimtuliza dada yake, akamwelezea kisa kizima kilivyokuwa, habari ambazo zilimsikitisha na kumliza sana. Aliyekufa ni rafiki yake wa kufa na kuzikana na aliyeua ni mdogo wake wa damu!
Shughuli za msiba zikaendelea, ukapangwa kufanyika siku nne baadaye ili kuweza kuwakusanya ndugu na marafiki waliokuwa mbali.

Kama ilivyo kawaida ya siku zote, licha ya msiba ule kusababishwa na wao, lakini walishiriki kwenye shughuli kama kawaida, wote wakionyesha kuwa na uchungu. Katika hali ya kawaida, hakuna mtu aliyetegemea yaliyokuwa yakitokea.
Mzee Komba na familia yake walishiriki kila hatua ya tukio lile na mzee Linus na familia yake nao hawakuonyesha kinyongo chochote, wote waliamini kilichotokea ilikuwa ni mipango ya Mungu.

Je, nini kilitokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua toleo lijalo.


chanzo globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates