Social Icons

Sunday, 25 January 2015

Hadithi: Familia tata. 5


Mzee Komba na familia yake walishiriki kila hatua ya tukio lile na mzee Linus na familia yake nao hawakuonyesha kinyongo chochote, wote waliamini kilichotokea ilikuwa ni mipango ya Mungu.
SASA ENDELEA...

Juddy alizikwa siku nne baada ya kufariki katika tukio lililokusanya umati mkubwa wa watu, kwenye makaburi ya Nakasangwe!
Watoto wa familia zote mbili walishiriki kikamilifu shughuli ile ya msiba na walikaa nyumbani kwa mzee Linus kwa siku zote, hadi ya saba, wakati walipokaa kikao cha pamoja kujadili kilichotokea na mzee Komba ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao kile.

“Rafiki, kaka yangu, shemeji yangu na wanangu wote wa nyumba hii, kwa niaba ya familia yangu, tunaomba kuwaomba radhi kwa yote yaliyotokea, lakini tunaamini ni kazi ya Mungu ambayo siku zote haina makosa,” Mzee Komba alisema huku akijifuta machozi, kitendo ambacho pia kilifanywa na watu wote, hasa Asfat, aliyesafiri kutoka Ulaya kuja kuhudhuria mazishi ya rafiki yake mkubwa!

“Usijali kaka, rafiki, jirani na wanangu wote. Kama ulivyosema, hili ni tukio ambalo hakuna aliyelitegemea, huu msiba ni wetu wote kama ambavyo tumeshuhudia, wote mmeshiriki kikamilifu tokea mwanzo hadi sasa. Nyinyi ni sisi na sisi ni nyinyi, haya yamepita, sasa tujitahidi kumnusuru Tonny, ni kijana mdogo aliyetaka kuwachekesha wenzake lakini matatizo yakatokea,” Mzee Linus naye alisema, huku watu wote wakiendelea kujifuta machozi!

Walijadili mambo mengi sana kama familia marafiki na hatimaye baadaye wakakubaliana kuondoa aina yoyote ya chuki baina yao. Wakasimama na kushikana mikono. Wakati wa tendo hili, wote waliendelea kutokwa na machozi.
Tonny alikaa polisi kwa siku tatu, baadaye akapelekwa katika mahakama ya watoto Kisutu jijini Dar es Salaam ambako alisomewa shtaka la mauaji ya bila kukusudia. Na baada ya kusomewa mashtaka yake ambapo hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama ile haikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, akapelekwa Segerea.

Wazazi walimtafuta mwanasheria aliyekuwa akitamba sana jijini Dar es Salaam, Bennedict ili aweze kumsimamia Tonny. Kazi hiyo hata hivyo haikuwa ngumu sana kutokana na wazazi wa marehemu nao kupigana kwa nguvu zote kuhakikisha kijana huyo anaachiwa!
Tonny aliachiliwa huru baada ya miezi mitatu tu na alipotoka mahakamani, alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa akina Juddy akiwa analia!

Kilio chake kiliashiria majuto aliyokuwa nayo. Hata hivyo, wote walionyesha moyo wa huruma dhidi yake na akaomba apelekwe kaburini kwa Juddy ili akaweke shada la maua.
Ombi hilo likakubaliwa na familia zote zikapanga kitendo hicho kifanyike kesho yake ambayo ilikuwa ni Jumapili ili wengine pia wahudhurie.

Makaburini, Tonny alipiga magoti katikati ya kaburi la Juddy, akachukua mshumaa na kuuwasha, akalibusu shada lake la maua na kuliweka, kisha machozi yakaanza kumtoka. Wanafamilia wengine waliomsindikiza nao waliweka mashada yao na kupiga magoti. Mwishowe wote kwa pamoja walisali na kuondoka!

Asfat akarejea zake shuleni Ulaya na ndugu wa familia zingine wakaendelea na maisha yao ya kila siku. Hakukuwa na tofauti yoyote kati ya familia hizi kwa kipindi kirefu.
Mwaka mmoja na miezi sita baada ya kifo cha Juddy, maisha yalikuwa katika mtindo wake wa kawaida kabisa kwa familia hizi rafiki.

Baptist, ambaye alimuachia ziwa Juddy, alikuwa akitoka mjini kutengeneza gari lao lililokuwa limeharibika mfumo wake wa umeme eneo moja la Gerezani, jijini Dar es Salaam. Wakati akirejea nyumbani alikuwa na mawazo mengi.
Katika umri wake wa miaka 25, alikuwa mtu wa kujirusha sana katika maeneo ya starehe. Ilikuwa ni lazima aende klabu kila mwisho wa wiki na hii ilimfanya kuwa na marafiki wengi wa kike na kiume.

Lakini sifa yake kubwa ilikuwa ni tabia yake ya kuendesha gari kwa mwendo kasi. Hata kama alikuwa akienda sehemu ya karibu, alipenda kulikimbiza...

Je, kitu gani kilitokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

No comments:

 
 
Blogger Templates