Baptist akamuelezea kuanzia mwanzo hadi mwisho. Askari akatingisha kichwa. Akachukua mkono wa simu ya mezani, akabonyeza namba kadhaa kisha akauweka sikioni.
Sasa endelea...
“Hebu askari watatu waje ofisini mara moja, wanatakiwa kwenda kupima ajali Nakasangwe na halafu kuangalia maendeleo ya majeruhi hospitalini haraka..,” ofisa yule wa polisi aliongea kwenye simu na kisha kurudisha mkonga sehemu yake.
Dakika moja baadaye, askari watatu, akiwemo mwanamke mmoja walikuwa ofisini hapo, wakapewa maelekezo, kisha wakainuka pamoja na Baptist na kuelekea kwenye gari la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser, maarufu kama Difenda. Wakakanyaga moto hadi eneo la tukio. Wakachukua vipimo pamoja na kupata vidokezo kutoka kwa majirani ambao sasa walikuwa wengi wamejikusanya ilipotokea ajali na nyumbani kwao mzee Komba, wengi wakiulizia maendeleo ya majeruhi.
Baada ya kumaliza shughuli hiyo, wakawasha gari wakiwa na Baptist na kuondoka kuelekea hospitali alikolazwa majeruhi. Wakaomba kukutana na daktari aliyempokea mgonjwa na kutaka kujua hali yake.
“Ana hali mbaya sana afande, sidhani kama atapona,” daktari aliyempokea na kumshughulikia Santo aliwaambia askari wale alipowakaribisha ofisini kwake na wao kujitambulisha.
“Ameumia kwa kiasi gani,?” askari kiongozi wa msafara aliuliza. Kabla daktari huyo hajajibu chochote, simu yake ya mezani ikaita. Akatoa ishara ya kumtaka radhi, akainua mkonga wa kuongelea na kuuweka sikioni, alisikiliza kwa sekunde chache kabla ya kuurudisha mahali pale.
“He is dead (amefariki),” alisema huku akitoa miwani yake na kuifuta kwa kitambaa chake cheupe!
***
Vilio viliripuka nyumbani kwa mzee Komba mara tu taarifa za kifo hicho zilipopelekwa. Alikuwa ni mzee huyo aliyempigia simu mtoto wake mkubwa wa kiume, akimfahamisha tukio hilo la kusikitisha. Mama yake Tonny alipoteza fahamu mara tu alipofuatwa na mtoto wake na kumweleza kuwa kule hospitalini, Santo amefariki dunia!
Taarifa za kifo hicho zilisambaa kwa kasi kubwa, ndugu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi waliarifiwa na zilipomfikia Asfat, ambaye sasa alikuwa ameshamaliza masomo na akijiandaa kwa safari ya kurejea nyumbani Tanzania, hakuamini.
“What?” aliuliza wakati alipopokea simu ya kaka yake, Amani, aliyemtaarifu juu ya msiba huo.
“Ndiyo hivyo sista, bahati mbaya,” Amani alisema kwa upole.
Asfat hakutaka kuamini kirahisi kama kifo kile kilikuwa bahati mbaya, akilini mwake aliona huenda kilikuwa ni kisasi, hivyo akataka maelezo ya kutosha kutoka kwa kaka yake.
“Kaka Amani, slowly please (taratibu tafadhali), hebu niambie vizuri, una uhakika kaka Baptist kamgonga Santo kwa bahati mbaya? Sitaki kuamini, naona kama kisasi fulani hivi, wewe unaonaje?” Asfat aliongea huku akiwa ameuma meno.
“Hapana dada Asfat, ni ajali. Santo alikuwa na mama uani, wanataniana, si unawajua walivyo, sijui ilikuwaje wakaanza kufukuzana, Santo akakimbilia nje, sasa ile anatokeza tu mlangoni na Baptist anapita, si unajua anavyoendeshaga, hakujua, hakumuona, hakuna hata mtu mmoja anayemlaumu Bap, ni ajali dada, amini ninachokuambia, ambacho najua hata mama atakuambia hicho hicho,” Amani alijaribu kumtuliza dada yake.
Asfat akakubali, lakini hakuridhika!!!!…
...Baptist akaondoka na askari wale kurejea kituoni Wazo, ambako aliwekwa mahabusu na baadaye kufunguliwa jalada la ajali iliyosababisha kifo.
Pale hospitalini, mzee Komba na mzee Linus wakaanza taratibu za kuutoa mwili ili uende kuhifadhiwa hospitali yenye majokofu ya kuhifadhia maiti. Majirani wengine kadhaa nao walikuwa wameshawasili hospitalini hapo kwa msaada wowote unaoweza kuhitajika.
Mzee Komba akashauriwa kurejea nyumbani ili aweze kupumzisha akili sambamba na kupokea wageni, kazi ile ya kushughulika na mwili wa marehemu ikaachwa mikononi mwa mzee Linus, akishirikiana na vijana wa familia zote mbili.

No comments:
Post a Comment