Monday, 19 January 2015
POLISI WATEMBEZA MKONG'OTO KWA RAIA
▼
Monday, January 19, 2015
LIGI DARAJA LA KWANZA: POLISI WAJERUHI MASHABIKI, YUPO ALIYEKATWA SIKIO, ALIYECHANWA TAKO NI UKATILI WA KUTISHA
Na Andrew Mhaiki, Songea
MASHABIKI wa Majimaji ya Songea juzi walijikuta katika wakati mgumu pale waliposhambuliwa na askari Polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia na baadhi yao wakilazwa hospitali ya mkoa wa Ruvuma(HOMSO) wodi ya majeruhi wakitibiwa baada ya majeraha ya kipigo kutoka kwa askari.
Askari hao ambao walionekana kutumia nguvu zaidi kuliko mashabiki ambao waliokuwepo kiwanjani hapo, baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi Daraja la kwanza (FDL) kati ya Majimaji na Kurugenzi ya Mufindi, mchezo ambao ulimalizika kwa timu hizo kufungana bao 1-1, mchezo huo ulifanyika kwenye uwanja wa Majimaji mjini hapa.
Katika mchezo huo Majimaji ndio walikuwa wakwanza kujipatia bao la kuongoza katika dakika ya 12 na Ditram Nchimbi kwa mpira wa kichwa, kabla ya Kurugenzi kusawazisha bao hilo katika 54 Asili Mkondya aliyeingia kuchukua nafasi ya Stanley Msangila, na Majimaji walikuwa wakicheza mbele ya Mkufunzi wao wa kiufundi na Mkurugenzi wa kituo cha michezo cha Symbion cha jijini Dar es Salaam, Stuward Hall.
Pamoja na mashabiki wa Majimaji kulalamika kuwa mashabiki wa Kurugenzi wamekuwa na tabia ya kuzishambulia timu pinzani zinapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani kwa kushirikiana na askari polisi wa wilaya hiyo, kitu ambacho askari wa kikosi hicho wakahisi huenda mashabiki hao wakalipiza kisasi wanachokifanya mashabiki wenzao wa timu pinzani.
Polisi walianza kurusha mabomu baada ya mashabiki wa Majimaji kumzomea Mbunge wao, Emmanuel Nchimbi wakati akitoka uwanjani kushuhudia mchezo huo, baada ya Mbunge huyo kuwapungia mkono mashabiki hao akiwataka watulie,huku mashabiki wao walijibu hatukutaki tuachie tuwafunze adabu hao Kurugenzi , kauli ambayo ilionekana iliwaudhi Polisi na kuanza kutumia nguvu kupiga mabomo na kutembeza kipigo pasipo sababu ya kimsingi kama kwa binadamu mwenye akili mwenye utashi wa kutambua baya na zuri.
wachezaji wa kurugenzi wakitolewa uwanjani kwa gari la polisi
Pamoja na Polisi kuwaondosha uwanjani wachezaji wa Kurugenzi na viongozi wao salama bado waliendelea kutengeneza chuki kwa wananchi kwa kuendelea kuwashambulia, kwani askari hao walihama ndani ya uwanja wa Majimaji na kuhamia mitaani kupiga wananchi wasiokuwa na makosa kama soko la Manzese ambapo waliingia na kuanza kuwashambulia wafanyabiashara pamoja na wanunuzi ambao waliingia katika soko hilo kutafuta mahitaji yao.
Baadhi ya mashuhuda wetu ambao walikuwa wakifuatilia unyama wa askari hao alidai hasira za askari hao zilimalizika maeneo ya Bombambili umbali wa kilometa mbili kutoka ulipo uwanja wa Majimaji ambapo walipiga mabomo na kuwashambulia wananchi wasiokuwa na hatia na kurejea kambini kwao, huku wakiwaacha wananchi wa Songea katika mshangao mkubwa juu ya hatima ya chombo chao kilichopewa dhamana ya kulinda usalama wa maisha ya raia na mali zao.
Mmoja wa wahanga hao pamoja na mwandishi wa mtandao wa www.jamvila habari.com alijikuta katika wakati mgumu pale alipolazimishwa kulala chini kifudifudi huku askari mmoja akimlinda kwa kumwekea bunduki ya aina ya SMG kisogoni wakimzuhia asipige picha za tukio hilo jinsi linavyoendelea pamoja na kumpa vitisho wangeweza kuondosha uhai wake mara moja, alidai alitii amri hiyo kwa lengo la kuokoa uhai wa maisha yake.
Mwandishi wa gazeti pia aliweza kupata bahati na kuzungumza na baadhi ya majeruhi ambao wamelazwa katika hospitali ya mkoa(HOMSO) wakipatiwa matibabu akiwemo mtangazaji wa kituo cha Radio cha mjini hapo (Jogoo Fm) ambaye amelazwa wodi namba mbili kitanda namba tatu, Hossam Ulaya alidai alishambuliwa na askari saba wa kikosi hicho wakati akijaribu kuwasalimisha wachezaji wa timu ya mkoa ya wanawake, baada ya Polisi kuwatembezea kichapo kisichokuwa na sababu, huku mmoja ya kati ya hao wachezaji amelazwa wodi namba tano ambaye amejitambulisha kwa jina la Arasha Chande
Mtangazi huyo alisema kichapo hicho kilimkuta baada ya kuona wachezaji hao wa timu ya mkoa ya wanawake wakichalazwa bakora na askari ambao wakiongozwa na mkuu wa kituo cha Polisi cha wilaya ya Songea, ambaye alimtaja kwa jina moja la Mashimbi ambaye alikwenda kwa ajili ya kuwasalimisha wachezaji hao, wakati huo anakwenda kuwasalimisha akiwa amefuatana na mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la mpira wa miguu nchini(TFF), James Mhagama.
Alisema pamoja na kichapo hicho bado aliweza kumshuhudia mjamzito wakimshambulia kwa marungu katika maeneo mbalimbali ya mwili wake huku akilia kwa maumivu na kumtaja askari mmoja wa kike ambaye na alikuwa akishiriki unyama huo alidai aliweza kunukuru jina moja la Jojina, na baadaye askari huo alikwenda na kuanza kumfariji kwa kumpa pole wakati wamemuumiza.
Alisema askari hao pamoja na vitendo vya vya kinyama kubwa zaidi alidai waliweza kumvamia mtoto wa jinsia ya kiume ambaye alidai anaweza kuwa na umri wa miaka saba kwa kumshambulia kwa marungu, mateke na kupelekea kumsababishia maumivu , alidai licha ya mtoto huo kuangua kilio askari hao waliendelea kumpa kichapo aliokolewa na kikundi cha vijana ambao walijitoa muhanga kwa kuwavamia askari hao kwa kuwarushia mawe na kuamua kumuacha na kukimbia huku mtoto huyo akiwa tayari amepoteza fahamu
Hata hivyo habari za kitelejensia ambazo zimenaswa na gazeti hili huenda vita hiyo ikaendelea Januari 24 mwaka huu, wakati Mlale JKT watakapokutana na Kurugenzi ya Mufindi katika mchezo wa ligi hiyo ya FDL ambao utakuwa wa kulipiza kisasi kati ya wananchi na jeshi la Polisi ambapo wananchi wanajipanga kwa mashambulizi, gazeti hili litaendelea kuwapatia nini kinachojili juu ya tukio hilo ambalo linahisiwa huenda likapelekea kutokea kwa mauaji.
Na baadhi ya wadau wa soka wa Songea walizungumza na gazeti hili wengi wao wamelitupia lawama jeshi la Polisi wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kulikoni akili na maharifa, huku wakidai hata nchi ikiingia kwenye machafuko yatakuwa yanasababisha na askari wa jeshi la Polisi na si jeshi la wananchi, kwani michezo ujenga umoja mshikamano wa kindugu na pia inaendeleza kudumisha amani na utulivu wetu tulionao Watanzania kwa sasa huku wakidai Serikali wanatakiwa walione hilo.
Hata hivyo Katibu mkuu wa chama cha soka mkoa wa Ruvuma (FARU) Ahamed Challe amesikitishwa na maamuzi ya jeshi la Polisi la kutumia nguvu kuliko akili, alidai ilikuwa haina sababu ya kuwashambulia wananchi na kuwajeruhi wakati wachezaji wa kurugenzi walikuwa wamewaondoa uwanja wakiwa chini ya ulinzi wao kwa amani na utulivu, baada ya hapo nao wangeondoka na wangeendelea na majukumu yao mengine ya kiusalama badala ya kuingia mitaani na kuanza kuwashambulia wananchi bila ya sababu.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikheli hakuweza kupatikana kuelezea tukio hilo lakini ameweza kunukuliwa wakati akiingia hospitali ya mkoa, kumtakia hali huyo mtangazaji wa kituo cha Jogoo Fm, Hossam Ulaya kuwa taarifa alizozipata kutoka kwa maofisa wake walidai wananchi walikuwa na lengo la kuwafungia milango askari wake ndani ya uwanja wa Majimaji kwa lengo la kuwashambulia, kitu ambacho si kweli huo ni uongo mtupu wanania ya kujitetea mbele ya Kamanda wao.
Jamvi la Habari Tanzania at 3:23 PM
Share
›
Home
View web version
Powered by Blogger.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment