Kijana huyo alikuwa na kituo maalum ambacho gari la shule yao lilikuwa likiwashusha. Kuanzia hapo kulikuwa na mwendo kiasi hadi kufika nyumbani kwao. Kabla ya kufika kwao, kulikuwa na vichochoro viwili ambavyo Stone angeweza kumfanyizia, lakini mara zote hakufanikiwa kwa sababu kijana huyo alikuwa na wenzake.
Endelea..
Kutoka pale alipokuwa, Stone alimuona Tonny akishuka na kuanza kutembea. Kwa hatua za haraka haraka, naye akaanza kujivuta kuufuata uchochoro ule alioingilia. Alipoufikia, tayari windo lake lilishavuka uchochoro wa kwanza, akawa katika uwazi, tayari kuufuata unaofuatia.
Naye akakaza mwendo na giza lilishampa fursa ya kufanya anavyotaka. Mtaa ulikuwa kimya, mapigo ya moyo wake yalikuwa makubwa, kiasi cha kuweza hata yeye mwenyewe kuyasikia, akaongeza mwendo na sasa alikuwa hatua chache tu kumfikia.
Tonny hakuwa na hofu yoyote, kichwani mwake alifikiria kuhusu homework aliyopewa shuleni, siku zote hakupenda kulala na kazi ya shule bila kuifanyia kazi. Alitamani afike haraka nyumbani ili amalizie kiporo chake.
Stone alimnyatia na kujiweka sawa kumrukia. Ghafla, taa kali ya gari ikamulika kutoka mwanzo wa uchochoro kwa nyuma yao, wote wawili wakageuka haraka kutazama, ndipo Tonny alipostaajabu kumuona mtu akiwa karibu yake mno, lakini ambaye hakupata kumsikia kabla taa hazijawaka.
Akapatwa na hofu kubwa, kwa vyovyote hakuwa na nia njema naye. Akageuka na kuanza kutembea kwa haraka kuumaliza uchochoro ule. Alipomaliza, akageuka tena kumuangalia mtu yule ambaye naye alikuwa anakuja taratibu. Mwanga wa gari ulimfanya amtambue aliyekuwa nyuma yake, akazidi kupatwa na hofu kubwa, Stone?
Stone alifadhaika sana, alililaani lile gari na kwa jumla, alijisikia mkosefu mno kwa kilichotokea, alijua wazi kuwa Tonny hawezi kumwelewa.
Chapuchapu akapata wazo, gari lilipopita, akamwita Tonny na kumtaka asimame. Akiwa ameshajenga hofu naye, Tonny akaongeza mwendo, hakumjibu lolote hadi alipofika nyumbani kwao, akaingia moja kwa moja chumbani kwake na kujitupa kitandani, hofu imetawala kichwa chake.
“Alitaka kunifanya nini?” Tonny alijiuliza bila kupata jibu, akaanza kufikiria nyenendo za Stone za siku za hivi karibuni, akaona wazi kuwa alikuwa na nia mbaya dhidi yake!
“Hapana, lazima nimwambie baba, siwezi kukaa kimya,” alijisemea na kuinuka akiwa bado hajabadilisha nguo za shule. Sebuleni, wazazi wake wote walikuwa wamekaa wakinywa kahawa. Akawasalimia na baadaye akawapa mkanda mzima!
“Hebu eleza vizuri maana usije sababisha matatizo bure, mtu hata hajakugusa unasema alitaka kukuua, tukueleweje?” baba yake, mzee Linus alimwuliza, moyoni mwake naye akihisi hatari kutokana na maelezo ya mwanaye.
“Sasa baba, mtu kama anakuja nyuma yako anatembea si unamsikia? Ninaamini kabisa kama siyo zile taa kumulika, kaka Stone alitaka kunidhuru, haiwezekani nimuone hatua moja nyuma yangu bila kumsikia halafu uchochoroni, tena na yeye alishtuka sana kwa zile taa, aligeuka nyuma na kuduwaa,” Tonny aliwaambia wazazi wake.
Mama yake aliyekuwa akisikiliza kwa makini bila kusema neno, akakohoa, ishara kwamba alikuwa anataka kusema, wote wawili wakamwangalia na kusubiri alichotaka kusema.
“Ninahisi harufu ya damu,” alisema na wote wakamkazia macho.
“Kivipi mke wangu,” mumewe alimwuliza.
“Katika siku za hivi karibuni Stone amebadilika sana, mimi nashangaa siku hizi hata hanisalimii, wakati ni kijana ambaye alikuwa rafiki yangu sana, huyu ana jambo anataka kufanya, tujihadhari,” alisema mama mtu.
“Twende kwa wazazi wake tukayazungumze,” alisema mzee Linus, kauli ambayo ilipingwa haraka na mkewe, kwa madai kuwa kitendo hicho kitaanzisha upya chuki baina ya familia zao.
“Hapana, ni lazima twende, halafu lazima akatoe taarifa polisi, nimepata mashaka makubwa sana na simulizi hii, hata mimi naanza kuona hatari, maisha hayako salama kabisa,” alisisitiza mumewe, ambaye baada ya kusema maneno hayo akainuka kuelekea nje ya nyumba yake.
Alipotokeza tu nje ya geti la nyumba yake akiwa na Tonny, macho yake yakatua kwa Stone, aliyekuwa amesimama upande wa pili wa barabara, taa kutoka kwenye nyumba zilizokuwepo mtaani, zilimfanya aonekane bila kikwazo.
Je, nini kilitokea? Usikose kufuatilia mkasa huu katika toleo lijalo.
Chanzo: Globalpublishers
No comments:
Post a Comment