Pamoja na kuwa alikuwa na akili nzuri darasani, lakini nje alikuwa kwenye makundi ya vijana, wakipora watu usiku na kuwabaka wasichana. Mara tatu alishawahi kukamatwa na Polisi kwa kutajwa na wenzake kwenye matukio, lakini mara zote baba yake mkubwa, aliyekuwa mfanyabiashara aliyefanikiwa, alitoa kitu kidogo na yeye kuachiwa..!
Sasa endelea...
Mzee Linus alishashiriki katika matukio mengi makubwa, ya kupora kwa kujeruhi na hatimaye majeruhi hao kufariki. Hakuweza kukumbuka vizuri watu wangapi walikufa baada ya kundi lao kuwashambulia kwa mapanga.
Kilichomfanya kuachana na tabia hiyo ya uhuni wa kupitiliza, ni siku alipombaka bila kujua, dada yake, mtoto wa baba yake mkubwa. Siku hiyo dada mtu aliondoka nyumbani usiku bila baba yao kujua na kwenda disco. akiwa huko, pamoja na marafiki zake, wakaondoka na wavulana wao kuelekea gesti. Njiani wakakutana na kundi la akina Linus.
Wanaume wakapigwa mapanga na kufanikiwa kukimbia, wasichana wakawekwa chini ya ulinzi. Linus alikuwa wa kwanza kumbaka dada yake ambaye ingawa alimtambua, aliamua kunyamaza ili kujiokoa maana hakujua nini angefanya kama angejitambulisha. Walipomaliza vitendo vile, wakawamulika kwa tochi wale wasichana usoni ili kuwatambua.
Hakuamini macho yake alipomuona dada yake. Akamuomba samahani sana. Dada yake aliamua kumsamehe kwa sababu hakujua angemuambiaje baba yake. Tokea siku ile, Linus akaacha maisha ya mjini, akarejea kanisani..
**
“Huyu dogo nataka nimshughulikie mimi mwenyewe, kama anadhani ule mwili wake unaweza kunishinda mimi, basi ataisoma namba,” mzee Linus alijisemea mwenyewe akiwa amelala kitandani kwake.Alijiwa na mawazo mengi sana kichwani mwake juu ya nini cha kumfanya Stone. Baada ya kufikiri sana, hatimaye akamkumbuka Dayani, mmoja kati ya marafiki zake wa utotoni Singida, ambaye aliendelea na tabia hiyo, hadi akawa jambazi wa kutisha kabla ya kutajirika na kuamua kuachana na kazi hiyo!
Dayani alikuwa anaishi Bunju, nje kidogo ya jiji na Dar es Salaam ambako alijenga nyumba moja nzuri sana na alikuwa na miradi kadhaa ya kumuingizia fedha, ikiwemo baa ya Zanzi ambako alipenda kutembelea mara kwa mara.
Asubuhi na mapema, mzee Linus alichukua simu yake na kumpigia Dayani, kwani ingawa yeye alishaacha mambo hayo, waliendelea kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara, alifahamu nyendo zake na wala hawakufichana.
“Haloo,” Dayani aliita mara baada ya kuona simu ya rafiki yake ikiita.
“Chuga, nahitaji kukuona,” alisema mzee Linus simuni bila hata kumsalimia. Aliposikia neno Chuga, mwili wa Dayani ulisisimka, kwa sababu lilikuwa ni jina waliloitana enzi zile za ukabaji, kwani wakiwa kazini hawakutakiwa kabisa kuitaja majina yao halisi hata kwa bahati mbaya. Akajua kuna kazi!
“Njoo tunywe supu Zanzi, utanikuta,” alisema Dayani na kukata simu!
Saa mbili kamili asubuhi, mzee Linus aliingiza gari lake katika eneo la maegesho la baa kubwa ya Zanzi. Ilikuwa ni moja ya baa zilizokuwa zikijaza watu sana na kwa kipindi hiki cha fainali za kombe la dunia, skrini kubwa nne zilifungwa kila upande.
Alimuona Dayani akiwa amekaa akisoma magazeti kwenye kibanda kimoja cha peke yake, akamfuata na kuvuta kiti na kukaa kabla ya kumpa mkono kumsalimia.
Mwenyeji wake akamuita mhudumu ambaye alifika na kuagizwa kuleta mchemsho wa samaki kwa ajili ya mgeni. Mzee Linus aliushambulia haraka haraka mchemsho huo ulipoletwa na alipomaliza, akakohoa kidogo kusafisha koo!
“Lete habari Chuga,” Dayani alimwambia mzee Linus. Wote wawili walionekana umri kuanza kuwatupa mkono. Aliposikia kauli hiyo, mzee Linus akajikuta akicheka kwa sauti!
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.
Chanzo: Globalpublishers
No comments:
Post a Comment