Mapigano yamepamba moto mashariki mwa Ukraine, kuelekea mkutano wa Belarus, unaowaleta pamoja viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Ukraine. Rais Barack Obama alizungumza na Vladimir Putin kuelekea mkutano huo.
Kansela Angela Merkel, marais Francois Hollande, Vladimir Putin na Petro Poroshenko wanatarajiwa mjini Minsk baadae siku ya Jumatano, kwa mazunugumzo muhimu juu ya mgogoro nchini Ukraine. Ikiwa mazungumzo hayo yatashindwa kuleta muafaka, vikwazo zaidi vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi vinatarajiwa. Marekani pia inatafakari kulipatia silaha jeshi la Ukraine ikiwa hakutakuwa na hatua zozote katika mazungumzo.
Kabla ya mkutano huo ikulu za White House na Kremlin ziliripoti juu ya mazungumzo kwa njia ya simu kati ya marais Obama na Putin. Kwa mujibu wa Whote House, Obama alisisitiza umuhimu kwa rais Putin kutumia fursa ya mazungumzo ya Minsk kufikia suluhu ya amani. Kremlin ilisema viongozi hao wawili wlikubaliana juu ya haja ya kuwa na suluhu ya kisiasa kwa mgogoro wa ndani wa Ukraine.
Ni mapema mno kwa usitishaji mapigano
Wajumbe wa upatanishi kutoka Ukraine, waasi wanaowania kujitenga, Urusi na shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE, waliweka msingi wa mazungumzo ya leo katika majadiliano ya karibu masaa mawili mjini Minsk jana. Licha ya taarifa za usitishaji mapiagano, ilibainika baadae ni hatua kidogo sana zilizopigwa.
"Ni mapema mno kuzungumzia usitishaji mapigano,"alisema Denis Pushilin, mjumbe wa ujumbe wa wanaotaka kujitenga. Aliongeza kuwa waasi wamewasilisha pendekezo juu ya namna ya kusonga mbele na kwamba walikuwa wanasubiri majibu, bila kubainisha undani wa mapendekezo hayo.
Na taarifa zinazotoka Ukraine zinasema mashambulizi ya waasi yamewauwa wanajeshi 19 wa Ukraine na kuwajeruhi wengine 78 katika mji wa Dibalseve. Mapigano mengine makali jana Jumanne yaliripotiwa kuuwa zaidi ya raia 10 na wanajeshi katika mji wa Kramatasorsk. Wakati mapigano yakiendelea, waziri wa mambo ya nje ya Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliwatolewa mwito wanaohusika kujizuwia wakati wanadiplomasia wakifanya kazi.
"Ukweli kwamba mkutano huo unafanyika siyo uthibitisho wa mafanikio. Ndiyo maana nazisihi, na nazitaraji Moscow na Kiev kuyachukulia kwa uzito, na kutumia nafasi hii, kwa kuzingatia kitisho kilichoko mbele yetu cha mgogoro wa kijeshi," alisema waziri Steinmeier.
Mpasuko barani Ulaya
Mgogoro huo umesababisha mpasuko miongoni mwa mataifa ya Ulaya, na kuitikisa dhana ya mshikamano usiyoyumbishwa wa mataifa ya Atlantic. Ufaransa na Ujerumani zimeweka chini matarajio ya juhudi zao mpya za amani. Rais wa Ufaransa Francois Hollande alisema viongozi hao walikuwa wanaongoza mazungumzo hayo kwa dhamira ya kufanikiwa, lakini bila ya kuwa na uhakika wa iwapo wataweza kutimiza lengo hilo.
Vita hivyo na miaka kadhaa ya rushwa iliyokithiri vimeipeleka nchi hiyo kwenye kingo za kufilisika, ambapo sarafu yake iliporomoka wiki iliyopita. Ukraine inajadiliana mkopo wa uokozi na shirika la fedha la kimataifa IMF, na duru zilisema mkopo huo huenda ukapanuliwa kwa kiasi kikubwa na kuipatia nchi hiyo kiasi cha dola bilioni 40 za msaada.
Chanzo: Dw.de
No comments:
Post a Comment