Harare, Zimbabwe. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amewasimamisha kazi walinzi wake 27 ikiwa ni siku chache baada ya kuanguka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Harare wakati akirejea nyumbani akitokea Addis Ababa, Ethiopia.
Kati ya waliokumbwa na adhabu hiyo ni pamoja na walinzi wake wa karibu ambao wanadaiwa kutojishughulisha kwa lolote wakati kiongozi huyo alipoteleza na baadaye kuanguka chini.
Likiwanukuu maofisa wa serikali, gazeti la The Standard lilisema kuwa walinzi hao wamewajibishwa kwa kushindwa kuchukua hatua za dharura kushughulikia tukio hilo lililosambaa katika mitandao ya kijamii.
Rais Mugabe ambaye alikutwa na mkasa huo muda mfupi baada ya kuzungumza na wafuasi wake waliokuja kumpongeza baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wiki ijayo atasherehekea siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 91.
Vyanzo vya habari vinasema kuwa, Ikulu haikufurahishwa na namna walinzi wake walivyoshindwa kuchukua hatua za haraka kudhibiti kuenea kwa taarifa za kuanguka kwake.
Taarifa zimesema kuwa kwa ujumla walinzi wa rais walibweteka kwani kanuni zinawataka kusimama angalau hatua chache kutoka kiongozi alipo.
“Hili suala ni kubwa tena lilipaswa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa na hawa walinzi walizembea kwani kanuni namba tatu inayohusu ulinzi kwa rais inaeleza ni umbali gani wanapaswa kusimama. Ninachoweza kusema ni kwamba kuna idara nyingi zinaendelea kuchunguzwa, kuanzia Shirika la Ndege la Zimbabwe lenyewe hadi timu nzima ya walinzi wake.
Sina uhakika katika hawa waliosimamishwa kama kuna mmoja wao atarejea kazini,” kilisema chanzo kimoja cha habari kikikariri taarifa kutoka mtandao wa www.bulawayo24.com. Hata hivyo mtandao huo baadaye ulisema kuwa taarifa ofisi ya Ikulu imekanusha vikali taarifa hizo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa walinzi hao walikabidhiwa barua za kusimamishwa kazi mwishoni mwa wiki na kwamba kurejea kwao kutategemea uchunguzi unaoendelea kufanywa.
Taarifa za kuwa walinzi hao walikuwa wamesimamishwa kazi zilipata nguvu mpya wakati wa ziara ya Rais Edgar Lungu wa Zambia aliyekuwa nchini Zimbabwe na kukutana na mwenyeji wake Rais Mugabe.
Wale waliokuwepo Ikulu walisema kuwa walishuhudia sura mpya za walinzi wakiwa kando ya Rais Mugabe. Hata wakati Rais Lungu akiondoka Ikulu, Rais Mugabe hakuambatana naye kumsindikiza uwanja wa ndege badala yake alisimama mita chache na baada ya mgeni wake kuondoka alirejea tena ofisini.
Msemaji wa Ikulu George Charamba hata hivyo alipuuza taarifa hizo akisema kuwa ni uzushi unaoenezwa na watu wasiokuwa na tija.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment