Imelda alivipanga vizuri vitu vyake, akatoa bastola na bunduki moja vilivyokuwemo chumbani, akaingia chini ya uvungu wa kitanda, akafunua mfuniko wa kuingia ndani ya handaki, akaurudishia vizuri, akaanza kuteremka na kutambaa kuelekea nje!
Sasa endelea...
GARI dogo la rangi ya kahawia lilifunga breki nje ya nyumba ya mzee Komba, watu wawili wakatoka nje na kugonga geti. Mama Juddy alikuwa karibu, akachungulia katika tundu la ufunguo ili kuwatambua wagongaji, lakini hakufanikiwa, hata hivyo, kwa kuwa ilikuwa ni mchana wa jua kali, akafungua mlango na kuwakaribisha.
Wakauliza kama pale ni nyumbani kwa mzee Komba, mama huyo akakubali kwa kutingisha kichwa. Akawakaribisha sebuleni kisha akamfuata mumewe chumbani kumweleza juu ya ugeni huo ambao ulikuwa bado haujajitambulisha. Alipofika na kuwasalimia, mazungumzo yakaanza.
“Sisi ni Polisi, mimi naitwa Noel,” alisema askari mmoja huku akimpatia mzee Komba kitambulisho chake. Na yule mwingine naye akampa na baada ya kuviangalia na kujiridhisha, akatingisha kichwa na kuwataka waendelee na kilichowaleta.
“Huyu anaitwa Yona. Tumekuja hapa kwako ili utusaidie mambo machache unayoyajua kuhusu Linus Kingwande,” Noel alimweleza mzee Komba.“Mambo ninayoyajua? Kama yapi,” naye alijibu kwa kuuliza.
“Tuna taarifa kuwa ni rafiki yako wa muda mrefu, lakini uhusiano wenu katika siku za hivi karibuni ulidorora sana, ni kweli?”
“Ni kweli, sielewi hasa tatizo lilianzia wapi, lakini nafikiri ni mambo ya watoto yamesababisha hadi ikawa hivi.”“Kivipi labda, ungejaribu kutufafanulia kidogo,” Noel alisema.Mzee Komba akasimulia kila kitu alichokijua kuhusu uhusiano wao, urafiki wao na mwanzo wa mzozo na hadi walipofikia. Wale polisi wakatazamana huku wakionekana kuwa kwenye tafakuri nzito.
Baada ya kuuliza uliza tena maswali mawili matatu, waliaga na kuondoka huku wakiwaachia maswali mengi yaliyokosa majibu wanandoa hao wawili. Walipobaki peke yao, wakajadiliana tena na kwa mbali, wakaanza kuhisi huenda jirani yao alikuwa katika matatizo makubwa.
***
Imelda alitambaa kwenye mtaro huo polepole huku akiwa na ujasiri wa ajabu. Tokea alipotambua kuwa mume wake ni jambazi, akajikuta amejivika roho ngumu, isiyojali wala kuogopa na mara mbili alishajaribu bila mafanikio kumshawishi Dayani waende wote eneo la tukio.
Kitendo hicho kilimfanya Dayani ampende sana na alimweleza kila jambo alilolifanya, tofauti na majambazi wengine ambao huwaficha wake zao kazi wanazofanya. Alipofika kwenye nyumba ndogo ambayo mtaro huo unatokea, alisimama kwa muda kusikilizia kabla ya kuufunua mfuniko.
Akachungulia kupitia dirishani na kujiridhisha kuwa hakukuwa na mtu karibu, akachukua ufunguo mmoja kati ya mitatu iliyokuwepo kwenye msumari, akafungua mlango na kutoka nje akiwa katika muonekano wa hijab. Bunduki aliiacha ndani ya handaki, lakini bastola ilikuwa pamoja naye.
Akaanza kutembea kuelekea barabarani, simu yake ya mkononi ikiwa sikioni, aliwasiliana na mume wake kumwelezea kinachoendelea, habari ambazo zilianza kumtia presha Dayani. Katika siku zote za uhalifu wake, polisi hawakuwahi kufika nyumbani kwake!
Alipofika barabarani, akasogea kituo cha daladala ili apande basi aelekee Kitunda kwa shemeji yake, akakae huko hadi mumewe arudi. Akiwa kituoni hapo, akamuona mjumbe wa mtaa wao, akiwa kwenye gari na watu waliofika nyumbani kwake.
Akabonyeza tena namba za mumewe, akasogea pembeni mbali na watu kisha akamfahamisha juu ya jambo hilo. Mumewe akamweleza kuwa kwa vyovyote wanakwenda kuvunja mlango ili waingie ndani.
“Umeziondoa zile bunduki?” Dayani aliuliza akiwa na hofu kubwa.
“Ndiyo, ile shotgun nimeiacha kwenye mtaro ila ile ndogo ninayo naondoka nayo,” mkewe alimjibu akiwa anatazama huku na huko kuona kama watu wanaweza kumtambua!
Chanzo: globalpublishers
No comments:
Post a Comment