KWA UFUPI
Azam ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 38, ikifuatiwa na Simba iliyo katika nafasi ya tatu na pointi 35, huku Yanga ikiongoza ligi kwa pointi 46, baada ya juzi kuichapa Mbeya City kwa mabao 3-1.
Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Azam wameanza kukata tamaa ya kutetea ubingwa wao msimu huu, baada ya kuweka bayana kwamba malengo yao ni kuhakikisha Simba haiwaondoi katika nafasi ya pili.
Azam ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 38, ikifuatiwa na Simba iliyo katika nafasi ya tatu na pointi 35, huku Yanga ikiongoza ligi kwa pointi 46, baada ya juzi kuichapa Mbeya City kwa mabao 3-1.
Meneja wa Azam, Jemedari Said alisema wanatambua Yanga imewaacha kwa pointi nane na hilo ni pengo kubwa, lakini wataendelea kupambana hadi mwisho kuhakikisha wanashiriki katika mashindano ya kimataifa mwakani.
“Kazi kubwa ni kuwakimbia Simba, tunatafuta utofauti wa pointi hivyo tunataka kwanza tuongeze pointi tatu na kuwa na tofauti ya pointi sita baada ya mchezo wetu na Mgambo JKT, kwani hata tukikosa ubingwa basi tuwe kwenye nafasi ya pili,” alisema Jemedari.
Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe amefuta uwezekano wa Azam FC kutetea ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Mrundi huyo tayari ameshafunga mabao tisa hadi sasa katika ligi na alisema kwa sasa hakuna timu inayoweza kuizuia Yanga kuchukua ubingwa kutokana na kiwango cha juu kinachoonyeshwa na timu hiyo. “Sitaki niongee maneno mengi kwani ukweli unajionyesha uwanjani. Kwa sasa akili yetu ipo kwenye ubingwa ambao ni lazima tuupate. Tuna kikosi bora kuliko timu yoyote ile kwenye ligi,” alisema Tambwe.
Tambwe alisema iwapo Yanga itatwaa ubingwa huo, itakuwa jambo la furaha kuvaa medali ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wakati huo huo, Suzy Butondo anaripoti kutoka Shinyanga; Kagera Sugar imeichapa Ruvu Shooting kwa mabao 2-0 jana kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Chanzo: Mwananchi

No comments:
Post a Comment