Umoja wa Mataifa wataka kusitishwa mapigano Yemen
Umoja wa Mataifa umetaka kusitishwa mara moja kwa mapigano nchini Yemen ili kuruhusu kufikishwa msaada wa dharura kwa maelfu ya watu wenye uhitaji. Shirika la Msalaba Mwekundu na lile la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, lilipatiwa fursa ya kuingia kwenye taifa hilo lililogawanyika katika Bara Arabu. Ndege mbili zilizojaa msaada wa madawa zilitua hapo jana kwenye uwanja wa ndege wa Sanaa, unaoshikiliwa na waasi wa Kihouthi. Ilikuwa ni shehena ya kwanza ya msaada kwenye mji huo, tangu Saudi Arabia kuongoza muungano wa mataifa ya Kiarabu kuwashambulia waasi hao mwezi Machi. Mapigano kwenye mji wa kusini wa Aden katika wiki za hivi karibuni, yalimlazimisha Rais Abd Rabbo Mansour Hadi kukimbilia mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.
India yaikosoa Pakistan kumuachia mshukiwa wa Mumbai
India imeukosoa vikali uamuzi wa Pakistan kumuachia mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya kigaidi ya Mumbai. Zakir-ur-Rehman Lakhvi alituhumiwa kuhusika na mashambulizi ya siku tatu kwenye mji wa kibiashara wa India, mwezi Novemba 2008. Zaidi ya watu 160 waliuawa kwenye mfululizo wa mashambulizi ya mabomu na ufyatuaji risasi. Lakhvi na washukiwa wengine sita wameshitakiwa nchini Pakistan kutokana na mashambulizi hayo, lakini kesi zao zimekuwa zikiendeshwa kwa kasi ndogo. Pakistan imekanusha kwamba vyombo rasmi vya dola vilihusika na mashambulizi hayo, kama inavyodaiwa na India.
Mmarekani ashukiwa kutaka kushambulia kambi ya kijeshi
Raia mmoja wa Marekani amekamatwa akituhimiwa kupanga mashambulizi ya kujitoa muhanga kwenye kituo cha kijeshi cha Marekani kilichopo Kansas. Maafisa wa mji huo wanasema mshukiwa huyo alikuwa yuko kwenye matayarisho ya mwisho mwisho ya mashambulizi hayo katika kambi za Fort Riley. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 20 anakabiliwa na mashitaka matatu, yaliwemo ya kujaribu kutoa vifaa kulisaidia kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.
Waandamanaji CAR wawashambulia wanajeshi wa Umoja wa Mataifa
Mtu mmoja aliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati wa mashambulizi yaliyofanyika katika kambi ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Risasi za tahadhari zilirushwa kuelekea kwa waandamanaji 400 waliojaribu kuweka kizuizi na kuichoma moto kambi hiyo. Wanajeshi kadhaa pia walijeruhiwa kwenye ghasia hizo. Hii ni mara ya pili ndani ya wiki moja kwa wapiganaji wa kulinda amani kushambuliwa katika kambi ya Kaga-Bandoro. Kikosi hicho cha wanajeshi 9,000 wa Umoja wa Mataifa kilichukuwa nafasi ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika mwezi Septemba. Watu wapatao 5,000 wameuawa kwenye mgogoro huo uliochukuwa sura ya kidini, tangu ulipoanza kufuatia mapinduzi ya mwaka 2013.
Chanzo: dw.de

No comments:
Post a Comment