Social Icons

Friday, 10 April 2015

Mahakama ya Kadhi na Siasa kali



SINEMA ya Mahakama ya Kadhi ilianza muda mrefu lakini mjadala wa sasa wa Mahakama hiyo ulianza baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutangaza kuwa muswada wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi ungewasilishwa katika kikao cha Bunge kilichomalizika hivi karibuni.

Hata hivyo, huo ulinoga pale Baraza la Maaskofu lilipoibuka siku moja baadae na kuwataka waumini wa dini ya Ukristo kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya “hapana”.

Tamko hilo lililotolewa chini ya mwavuli wa Jukwaa la Wakristo limetaja sababu mbili za uamuzi wake kuwa ni muswada wa Mahakama ya Kadhi kukiuka misingi ya taifa kuwa na serikali isiyo na dini, na Kura ya Maoni kusababisha mgawanyiko.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alichangamsha zaidi mjadala huu alipojitokeza kukosoa tamko la maaskofu la kuwataka waumini wa kikristo kupiga kura ya hapana kwa Katiba Pendekezwa, jambo lililosababisha Askofu Josephat Gwajima kumkemea na kujikuta matatani akituhumiwa kumkashifu Pengo.

Matukio kadhaa yaliyofuatia yaliisukuma serikali kufuta uamuzi wake wa kuwasilisha muswada wa Mahakama ya Kadhi. Bila shaka, serikali ilipima upepo na kugundua kuwa muswada wa Mahakama ya Kadhi ungeleta msuguano mkali bungeni.

Dalili za hali hiyo zilikuwa dhahiri katika semina iliyoandaliwa kwa ajili ya wabunge kujadili muswada huo, ambapo baadhi ya wabunge waliitaka serikali iuondoe muswada huo, huku wengine wakiutetea.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali wabunge walitukanana, walikejeliana, walizomeana na hata kutishiana. Kwa ujumla ubabe ulitawala.

Ikumbukwe kuwa muswada wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi uliondolewa kwenye mkutano wa Bunge uliopita kabla ya huu wa Machi kwa kilichoelezwa kuwa ulihitaji ‘mashauriano zaidi’. Lakini hata baada ya mashauriano zaidi, kwa mara nyingine serikali imebidi kuundoa.

Miongoni mwa watu ambao mjadala huu umewaweka katika wakati mgumu ni Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye naye amekwishatia shatia nia ya kuwania urais kumrithi bosi wake, baadaye mwaka huu.

Akiwa Muislamu, Rais Jakaya Kikwete, amejikuta katika wakati mgumu. Viongozi wa dini ya Kikristo wameonyesha kutokubali kusikiliza au kumuamini katika utetezi wake wa muswada wa Mahakama ya Kadhi.

Hali hii bila shaka imejitokeza kwa sababu tayari Wakristo wengi wamekuwa wakiamini kuwa utawala wa Kikwete umekuwa ukipendelea Waislamu.

Kwa sababu hii, pamoja na Kikwete kufafanua kuwa serikali haitoanzisha wala kugharimia Mahakama ya Kadhi, bali inakusudia kutunga sheria kuitambua na kudhibiti shughuli zake, Baraza la Maaskofu limeshikilia msimamo wake wa kupinga muswada huo.

Ikumbukwe kuwa, madai ya awali ya Waislamu ilikuwa serikali ianzishe na kugharaimia Mahakama ya Kadhi. Baada ya majadiliano serikalini ikaonekana si sahihi kwa serikali kuanzisha, kuiendesha wala kuigharimia Mahakama hiyo. Waislamu wakaambiwa kama wanataka waanzishe na kuigharimia wao wenyewe.

Kwa upande wake, Mizengo Pinda amekuwa akishutumiwa kwa kutoa rushwa ya ahadi ya Mahakama ya Kadhi wakati wa kupitisha Katiba Pendekezwa katika Bunge Maalumu la Katiba na kwamba kushupalia muswada huo kuna malengo ya kisiasa ya kutaka kuungwa mkono katika harakati zake za kugombea urais.

Wakati hayo yakiendelea, Waislamu nao wanaona Mahakama ya Kadhi ni haki yao. Waislamu wanadai Mahakama ya Kadhi haiwahusu Wakristo na kuhoji vipi pilipili wasoila iwawashe, ukizingatia kuwa hata miongoni mwa Waislamu hawalazimishwi kupeleka masuala yao huko.

Waislamu wa Tanzania ambao ni wengi ukilingnisha na idadi ya Waislamu walioko Kenya, Uganda na Rwanda wamekuwa wakihuzunika kuona kuwa nchi hizo zimekuwa na Makakama ya Kadhi bila kuleta usumbufu wowote kwa serikali na Wakristo wa nchi hizo na kujiuliza kwa nini sio Tanzania?
Hata hivyo, harakati za Waislamu za kudai Mahakama ya Kadhi zimekosa nguvu kutokana na migawanyiko ya Waislam wenyewe. 

Kosa kubwa walilolifanya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ni kujikasimisha madaraka ya kuendesha Mahakama ya Kadhi bila kushirikisha taasisi nyingine.

Bakwata walidhani wangeipata Mahakama ya Kadhi kirahisi, wakitarajia ‘nia njema’ ya serikali. Sasa, ambapo nguvu ya pamoja ya kushawishi inatakiwa, Bakwata wanagundua kuwa yenyewe pekee haiwezi.

Yote kwa yote, mambo muhimu niliyojifunza kutokana na mvutano huu ni, mosi, suala la Mahakama ya Kadhi kama halitoshughulikiwa kwa busara litazalisha siasa kali nyingi kutoka dini zote Waislamu na Wakristo.

Wazo la kuwapo Mahakama ya Kadhi limezalisha Wakristo wengi wenye misimamo mikali ambao hawataki kuona hata kidogo, Mahakama ya Kadhi inatajwa katika majalada ya serikali.

Msimamo huu wa Wakristo na labda kutokana pia na namna ulivyowasilishwa na kujadiliwa umezalisha Waislamu wengi wenye misimamo mikali, nao wakidai Mahakama ya Kadhi ni haki yao na ni lazima iwepo.

Ukisikiliza viongozi wa kiislamu, wamekuwa wakidai kuwa Wakristo wanatumia wingi wao serikalini na ushawishi wao mkubwa katika vyombo vya habari, kuzuia sheria ya kuitambua Mahakama ya Kadhi. Masheikh wanadai hakuna madhara yoyote ambayo Wakristo watakumbana nayo kwa Waislamu kuwa na Mahakama ya Kadhi.

Hali ya uhusiano wa dini hizi mbili, Waislamu na Wakristo, kwa sasa ni tete. Hii ndio hali halisi, tukubali tukatae. Pamoja na kuwa Waislamu na Wakristo wanaishi, wanafanya kazi na kushiriki mambo mengi kwa pamoja, ukweli ni kwamba waumini wa pande hizi mbili wamebeba ‘wasiwasi’ dhidi ya wenzao wa upande wa pili. Katika hali hii, ushawishi na chokochoko ndogo inaweza kuleta maafa na kuharibu amani na utulivu wa nchi yetu.

Tatizo la msingi ambalo mimi ninaliona ni kwamba tumeshindwa kusikilizana, na badala yake jazba na mihemko imetawala. Naaamini Serikali, na viongozi wakuu wa pande hizi mbili wakikaa na kujadiliana bila jazba wala chuki na kwa nia njema tutafikia muafaka na kuilinda nchi isiingie katika majanga ya vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Swali la msingi ambalo linapaswa kuongoza mjadala wa Mahakama ya Kadhi ni je, inawezaje kuanzishwa (na Waislamu wenyewe) bila kukera watu wa dini nyingine? Ili swali hii lijibiwe vema ni muhimu Wakristo wakaweka bayana kabisa wasiwasi wao juu ya Mahakama hii na mipaka ambayo wanadhani ikivukwa wao (kama Wakristo) au taifa litaathirika.

Mwisho, napenda kuonya kuwa mivutano hii na hususan inapohusisha viongozi wakuu si mizuri na huweza kuwafanya kushindwa kutoa uamuzi sahihi kwa hofu ya kuudhi watu. Kama ambavyo Kikwete Muislam, amejikuta katika wakati mgumu katika suala hili akihofu kutoonekana mbaya na watu wa dini isiyokuwa yake, atakuja rais mkristo ambaye naye Waislamu watamuandama na kumuweka katika jakamoyo la kushindwa kutoa uamuzi akihofia kuonekana anawachukia Waislamu. Huu sio mwelekeo mzuri kwa taifa. - 

Chanzo: Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates