Social Icons

Wednesday, 15 April 2015

Yanga kumbakumba


Dar es Salaam. Yanga imeendeleza harakati zake za kuivua Azam ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa Mbeya City iliyomaliza pungufu, kwa mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga ambayo inaiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika ilipata mabao yake kupitia Kpah Sherman, Salum Telela na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, huku Themi Felix akifunga bao la kufutia machozi kwa Mbeya City kabla ya kutolewa kwa kupewa kadi nyekundu.

Kwa matokeo hayo Yanga imejikita kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 46, baada ya kucheza mechi 21, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 38, huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake 35.

Ushindi huo umeiongezea morali Yanga inayojiandaa kuvunja mwiko Aprili 18, kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam itakapoikabiri  Etoile du Sahel ya Tunisia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha alisema tayari wamepokea taarifa za ujio wa Etoile du Sahel ambayo itawasili nchini Alhamisi hii.

Kwenye Uwanja wa Taifa jana, Yanga ilianza mchezo kwa kulisakama lango la Mbeya City katika dakika ya tano, ambapo nahodha wa Haroub ‘Cannavaro’ alikosa bao baada ya shuti lake kuokolewa na kipa  Hanington Kalyesubula.

Pia mwamuzi Mathew Akrama alikataa bao la Yanga katika dakika ya nane kwa madai mfungaji Amissi Tambwe alikuwa ameotea kabla ya kuunganisha krosi ya Simon Msuva.

Mshambuliaji Sherman alisawazisha makosa ya wenzake kwa kuifungia Yanga bao la kwanza katika dakika ya 17, baada ya kupokea mpira uliopigwa fyongo na Tambwe na kumkuta Mliberia huyo aliyemlalia Juma Nyoso kabla ya kugeuka na kupiga shuti lililompita kipa wa Mbeya City, Kalyesubula na kujaa wavuni.

Bao hilo lilikuwa la pili kwa Sherman katika Ligi Kuu kwani bao lake la kwanza alifunga wiki iliyopita wakati Yanga ilipoichakaza Coastal Union kwa mabao 8-0 kwenye Uwanja wa Taifa. 

Yanga ilitawala mchezo huo baada ya bao hilo kwa wachezaji wake kugongeana pasi nyingi katikati ya uwanja na kuwafanya Mbeya City kupata wakati mgumu kupanga mashambulizi yao, pia wachezaji wa Mbeya City walishindwa kuwakaba vema wachezaji wa Yanga hivyo kuwapa nafasi ya kuanzisha mashambulizi.

Yanga ilipata bao la pili dakika ya 38 kupitia kwa Salum Telela aliyeunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna Niyonzima baada ya Sherman kufanyiwa faulo na Christian Sembuli. Mpira huo uliopigwa na Telela uliwababatiza mabeki wa Mbeya City kabla ya kutinga wavuni.

Haya hivyo, mshambuliaji Themi Felix alitumia vizuri uzembe wa mabeki wa Yanga na kipa wao Mustapha ‘Barthez’ kuipatia Mbeya City bao katika dakika 40 ya mchezo na timu hizo kwenda mapumziko matokeo yakiwa 2-1.

Kinara wa Ligi Kuu, Yanga iliingia kwa kasi katika kipindi cha pili na kupata bao la tatu lililofungwa na Haroub ‘Cannavaro’ akiunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Niyonzima.

Mbeya City ilipata pigo dakika ya 57, wakati Themi Felix alipopewa kadi nyekundu na mwamuzi Akrama kutokana na kumchezea vibaya kiungo wa Yanga, Telela.

Baada ya kadi hiyo kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi aliwapumzisha Raphael Alpha, Deus Kaseke na Paul Nonga nafasi zao kuchuliwa na Abdallah Seif, Peter Mapunda na Mwigane Yeya.

Wakati kocha wa Yanga, Hans van Pluijm alimtoa majeruhi Telela na  Sherman na nafasi zao kuchukuliwa na Hassan Dilunga na Mrisho Ngassa.

Mabadiliko hayo yalionekana kuifaidisha zaidi Mbeya City kwani ilijipanga kuizuia Yanga ili isifungwe mabao mengi zaidi kama ilivyokuwa kwa Coastal Union.

Yanga itashuka uwanjani tena Jumatano kucheza dhidi ya Polisi Morogoro kumalizia viporo vyake vya Ligi Kuu.

Wakati huo huo, Stand United imeutumia vizuri uwanja wake baada ya kuichapa Polisi Morogoro kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage.Mshambuliaji Abaslim Chidiebele alifunga bao pekee kwa Stand katika dakika 60 na kuhakikishi pointi tatu.

Vikosi

Yanga: Ally Mustapha, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Salum Telela, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Kpah Sherman na Simon Msuva.

Mbeya City: Hanington Kalyesubula, Richard Peter, Hassan Mwasapili, Juma Nyoso, Christian Sembuli, Kenny Ally, Paul Nonga, Raphael Alpha, Themi Felix, Peter Mwalyanzi na Deus Kaseke.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates