HATIMAYE imetokea. Baada ya jina lake kukatwa katika kinyang’anyiro cha kutafuta mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi –na baada ya minong’ono iliyodumu kwa muda mrefu kuhusu iwapo Edward Lowassa atabaki au kuhama kutoka chama hicho, sasa ni rasmi kuwa amejiunga na Chama cha Demkrasia na Maendeleo (Chadema).
Lowassa sasa ndiye mgombea wa nafasi ya urais kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya NCCR Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF), Chadema na National League for Democracy (NLD).
Kutokana na hatua yake ya kuhama kutoka CCM, Lowassa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, ameweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu kutoka chama hicho kujiunga na upinzani tangu Tanzania ilipoanza siasa za vyama vingi zaidi ya miaka 20 iliyopita. Wakati akiwania nafasi hiyo kupitia CCM, Lowassa alikuwa akionekana kama mgombea kinara na tafiti nyingi zilizofanyika zilimuonyesha kama mgombea aliyekuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda.
Kuondoka kwake CCM kumekitikisa chama hicho kuanzia juu mpaka chini. Lowassa ni mwanasiasa mwenye taswira mbili tofauti. Kwa wengine, anaonekana kama mfano wa viongozi wa kuigwa kwa utendaji na si maneno matupu lakini kwa wengine anaonekana kama ndiye “ Baba wa Ufisadi” hapa nchini. Vyote hivi viwili anakwenda navyo Ukawa.
Hata kwa mambo ambayo Ukawa imekuwa ikiyasimamia kwa muda mrefu, Lowassa si aina ya mtu anayekwenda na sera hizo. Ukawa imejijengea sifa kutokana na mambo makubwa mawili; mosi msimamo wa kuunga mkono mapendekezo ya Tume ya Jaji Joseph Warioba kuhusu Katiba Mpya na Pili ni kupinga ufisadi.
Mmoja wa waungaji mkono wakuu wa Katiba Inayopendekezwa inayopinga na Ukawa alikuwa ni Andrew Chenge ambaye ni mmoja wa maswahiba wakubwa wa kisiasa wa Lowassa. Lowassa pia amekuwa akituhumiwa na Ukawa kama Baba wa Ufisadi na Chadema kwa muda mrefu na sasa watapata taabu kuwaeleza wananchi vinginevyo.
Ndiyo maana, wapo wanaoamini kuwa uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka hautatawaliwa na masuala ya kisera au kiitikadi kwa sababu hii ya mkanganyiko wa Ukawa. Chadema na vyama vingine vinavyounda Ukawa wamekubali kumeza matapishi yao kwa kumkubali mwanasiasa ambaye wametumia muda mrefu kumshambulia kwa kumwita majina yote mabaya.
Wanachama wa Chadema waliokuwa na matamanio ya kuwania urais kama aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, sasa wamebaki kuwa watazamaji. Viongozi wa Ukawa wameamua kucheza kamari hiyo wakiamini kuwa inaweza kulipa kwenye uchaguzi. Inawezekana ushindi ukapatikana kwa njia hii. Hii ni kamari.
Lowassa pia amecheza kamari ya aina yake kwa sababu kila mtu alitaraji kuwa baada ya kilichotokea CCM, angeamua tu kuwa mstaafu. Kwa namna zaidi ya moja, kilichofanyika kwa Ukawa kumpitisha Lowassa kinaonekana kama ni uamuzi uliofanywa kwa haraka. Imeonyesha kuwa Ukawa haikuwa na imani kuwa Dk. Slaa angeweza kumshinda mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli. Inamuonyesha Lowassa kama mtu aliyefikia maamuzi kutokana na kukosa namna nyingine.
Inaionyesha Chadema kama chama kilichoamua kuweka pembeni misingi yake kwa sababu ya kupata madaraka. Inamuonyesha Lowassa kama mtu aliyeamua kuweka maslahi yake binafsi juu ya maslahi mapana ya chama chake. Kwa mtazamaji wa pembeni, swali kubwa la kujiuliza ni moja; Je, mambo haya yote yana athari gani kwa uchaguzi wenyewe? Kwa sasa, hili ni swali ambalo busara inahitaji kuliepuka.
Kuna mambo yasiyofahamika yanayofanya ubashiri uwe kazi ngumu kufanyika. Maswali yafuatayo ni muhimu kupata majibu yake kabla ya kufanya ubashiri wowote.
1. Lowassa ataondoka na wangapi?
Kwa sasa habari za maelfu ya wanachama wa CCM, wa kawaida na wengine vigogo kama mawaziri, wabunge na viongozi wa chama hicho katika ngazi mbalimbali, kukihama chama hicho na kuhamia Chadema zimepamba moto.
Kama maneno ya wafuasi wake kuhusu nguvu ya kisiasa aliyonayo Lowassa ndani ya CCM ni ya kweli, maana yake kuna uwezekano wa chama hicho kupasuka katikati. Huu ndiyo wakati ambapo itafahamika kama kweli Lowassa alikuwa na wafuasi wanaopenda kwa thati au walikuwa wakivutiwa na mambo mengine.
Watu wengi sasa wanafanya maamuzi kuhusu mustakabali wao wa kisiasa. Kwa vile huu pia ndiyo wakati ambao vyama viko katika mchakato wa kutafuta wagombea wa nafasi za ubunge, maamuzi hayo yanatakiwa kufanyika kwa haraka.
2. Fedha zitakwenda wapi?
Si siri kwamba Lowassa alikuwa na watu wengi nyuma yake wanaomsaidia kifedha.
Watu hawa waliokuwa wakimchangia Lowassa fedha bila shaka sasa watakuwa na uamuzi wa ama kuendelea naye akiwa upinzani au kubaki CCM. Si rahisi kuwa Lowassa alifanya uamuzi wa kuhama pasipo kujua kuwa fedha hizo za wafadhili wake zitamfuata popote alipo.
Lakini, wafadhili hao pia wanajua kuwa ni jambo la hatari kujiruhusu kumfadhili mgombea mmoja wakati huna uhakika kama atashinda. Kuunga mkono wagombea wote wawili ni gharama kubwa lakini ndiyo namna pekee ya kumfanya mchangiaji ashinde kwa vyovyote itakavyotokea. Swali ni kwamba, kati ya Lowassa na Magufuli, nani atapata zaidi?
3. Dk. Slaa atakwenda wapi?
Dalili zinaonyesha kwamba Dk. Slaa hajakubaliana na uamuzi wa wenzake kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wa Ukawa.
Taarifa zilizopo ni kwamba si Slaa pekee ambaye hajaunga mkono bali kuna wengine wanaomuunga mkono. Kuna uwezekano wa kuanza kuona wanachama (akiwamo Slaa?) pia wakihama kutoka Chadema na kwenda kujiunga na chama kipya cha ACT-Wazalendo kinachoongozwa na mwana Chadema wa zamani, Zitto Kabwe.
Wengine pia wanaweza kwenda kujiunga na CCM. Zitto ni mdogo kiumri kuweza kuruhusiwa kuwania urais kwa mujibu wa Katiba. Lakini ni jambo la wazi kuwa chama chake kinahitaji kuwa na mgombea urais mwaka huu. Kama Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na Lowassa wameweka pembeni tofauti zao na kukubaliana kufanya kazi pamoja; kwanini isiwe kwa Zitto na Dk. Slaa kwenye ACT?
4. Wafuasi wa Chadema wanakubaliana na hili?
Wengi wa wafuasi wa Chadema walikipenda chama hicho kutokana na msimamo wake kwenye masuala ya ufisadi. Je, wanachama wa kawaida wa Chadema wamepokeaje jambo hili kwamba yule mtu ambaye waliaminishwa kuwa ndiye fisadi namba moja hapa nchini, sasa ndiye kinara wao? Swali ni hili; Je, Ukawa itapoteza watu wangapi kwa sababu tu ya kumfanya Lowassa kuwa mgombea wake?
5. Nini kinaweza kutokea?
Lowassa anaweza kuanguka au kuzimia kwenye mojawapo ya mikutano ya kisiasa. Anaweza kutumia ufahamu wake wa masuala ya ndani ya serikali kumbomoa Kikwete na serikali yake. CCM inaweza kupata ushahidi wa moja kwa moja kumhusisha Lowassa na rushwa ambao utasababisha atumie muda mrefu kwenye mapambano ya kisheria badala ya siasa. Kuna wanaosema pia kuwa Lowassa si mzuri kwa kujieleza kwa maana ya sera na ufafanuzi wake. Itakuwaje atakapotakiwa kushindana na Magufuli kwenye mdahalo? Hayo ni mambo ambayo hayajatokea lakini yatakapotokea yanaweza kubadilisha ubashiri wowote uliotolewa kabla. Mwandishi wa makala haya,
Chanzo:Raia mwema

No comments:
Post a Comment