Social Icons

Wednesday, 19 August 2015

Ni wakati wa CCM kujisahihisha


JUZI hapa kwenye mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, mbali ya wazungumzaji wengine, nilimwona na kumsikiliza Mzee Joseph Butiku. Naamini Watanzania wengi wamepata fursa ya kumsikiliza na kumuelewa.

Nilimwona Mzee Butiku akinyanyua vitabu viwili vilivyoandikwa na Mwalimu; ' TANU na Raia' na ' Tujisahihishe'. Nina bahati ya kuvisoma vitabu vyote hivyo. Kwenye TANU na Raia Mwalimu aliona umuhimu wa kujiuzulu na kumwachia madaraka ya Uwaziri Mkuu Rashid Kawawa na yeye Mwalimu kuzunguka nchi nzima kuwasikikiliza wananchi. Mwalimu aliona mapema, kuwa TANU ilianza kupoteza ukaribu na umma. Kwamba kukawa na tabaka la viongozi walio mbali na wanaowaongoza.

Na ndipo akaja na kijitabu kile muhimu cha ' TUJISAHIHISHE'. Na hakika, CCM ya sasa, kwa yote iliyoyapitia hadi kufikia hatua hii, na kwa kusoma alama za nyakati, ina lazima ya kuiona hali iliyopo kama fursa ya kipekee na ya kihistoria, ya chama hicho kujivua magamba kwa ukweli na kuanza na ' CCM Mpya' itakayoanza kuifuata kwa matendo; misingi, malengo na madhumuni ya kuwepo kwake. Ni fursa ya chama hicho kuutafuta moyo wa chama hicho- Searching for party's soul.

CCM wana lazima ya kuujua ukweli wao na wakati unaowazunguka. Na hili lilipata kusemwa na hata Mwenyekiti wa chama hicho. Jakaya Kikwete, alipata kuusema ukweli wake juu ya Chama chake, tena ni kwenye vikao vya Chama hicho kule Dodoma. Kwa ufupi tu, Kikwete aliwatamkia Wana-CCM wenzake, kuwa wakati umebadilika. Kwamba chama hicho kina lazima ya kusoma alama za nyakati. Kikwete alikisaidia chama chake kuuelewa ukweli unaoishi nao, sasa.

Nimepata kuliandika hili, kuwa kuna namna mbili kwa mtu kusafisha chumba chake; unaweza kufagia chumba, ukazoa takataka na kuzitupa. Lakini waweza pia kuzifagilia takataka chini ya jamvi.

Ukifanya hilo la mwisho bado atakayeingia chumbani kwako ataona chumba kimesafishwa. Huko ni kujidanganya kwa mwenye chumba. Akiendelea na tabia hiyo, iko siku uchafu ule utaanza kuvunda na kunuka. Asipoinua jamvi kuondoa uchafu unaovunda iko siku ataambiwa na wengine; kuwa chumba chako kinanuka.

Ni vema na busara kabisa tukawa na taratibu na nidhamu ya kuzifuata taratibu. Na nidhamu ya kufuata taratibu inatokana na sheria na adhabu zinazoendana na kukiukwa kwa taratibu hizo.

Na hapa mpira uko ndani ya chama tawala, CCM. Chama Cha Mapinduzi ni chama tawala, hivyo kina wajibu wa kwanza wa kuandaa taratibu zitakazofuatwa ndani ya chama hicho inapohusiana na uongozi wa kisiasa. CCM hakipaswi kuwa ni chama kinachopambana ili kiishi. Tayari kiko madarakani, hiki si chama cha upinzani.

Ndani ya CCM ilianza kuboboka misingi iliyosababisha kuanzishwa kwa chama hicho tukianzia na vyama mama vya TANU na Afro- Shiraz. Hili ni jambo la hatari sana. Ikumbukwe, Vyama mama kwa CCM, TANU na Afro- Shiraz, vilikuwa ni kimbilio la makabwela, kimbilio la wanyonge.

Lakini, CCM ya sasa imeonekana ikikimbiliwa zaidi na wafanyabiashara, wasomi na wajanja wengine. Wasomi hapa kwa maana ya hata wale wenye taaluma zao, wako tayari kuzikimbia taaluma zao na kuingia kwenye siasa za vyama, hususan Chama cha Mapinduzi. Baadhi yao wanasukumwa huko kwa ajili ya kutafuta maslahi zaidi. Maslahi binafsi. Na kuna waliokuwa wakiambiwa; "Mkitaka mambo yenu yawanyokee, njooni CCM". Si mambo ya wananchi, ni mambo yao binafsi!

CCM ya sasa imekuwa ikikimbiliwa hata na baadhi ya viongozi wa taasisi za kidini. CCM ya sasa ni taasisi kubwa. Ndani yake imekuwa na watu wa kila namna. Kuna makundi. Kuna majungu na fitna. Kuna kupakaziana, kuchafuana na kusafishana.

Naam. Kuna waliokuwa wakikimbilia ndani ya CCM kwa kuamini katika malengo na madhubuni ya kuanzishwa kwa chama hicho. Lakini kuna wanaokimbilia ndani ya CCM wakiwa na malengo na madhumuni yao binafsi yasiyohusiana kabisa na ya CCM. Kwao wao, CCM ni sawa na daraja la miti la kuwasaidia kuvuka na kufika wanakotaka kwenda.

Baadhi wako tayari kutumia mamilioni ya shilingi kukimbilia uongozi ndani ya chama hicho. Wanakimbilia ndani ya chama kujificha, kuficha maovu yao, kulinda na kutetea maslahi yao binafsi na ya makundi yao.

CCM ina nafasi ya kujisahihisha na kuuvunja ili iweze kuongoza kwa miaka mingi mingine. Si udhaifu kwa kiongozi au wanachama wa chama cha siasa kukiri udhaifu na kujisahihisha. Mwl. Nyerere katika kijitabu chake cha " Tujisahihishe" anaandika; "Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi huzuia Umoja wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumuni yake. Ukiondoa matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige, kiangazi, nk, matatizo yao mengi hutokana na ubinafsi"

"Swali ambalo twalisikia mara kwa mara; "Hali yetu ya baadaye itakuwaje? Mtu anayeuliza anafikiri kuwa TANU iliundwa kwa faida yake yeye binafsi. Ni kama kwamba TANU ilipoundwa ilimwahidi kwamba ikiwa atakubali kuwa mwanachama, au kiongozi, basi, TANU itamfanyia yeye jambo fulani kama tuzo! Anasahau kabisa, kuwa TANU inajishughulisha na haja za jumuiya kwa ujumla.

Lakini, kwa mtu wa aina hiyo, hata kama TANU inatimiza madhumuni yake ya Jumuia, ataona kuwa ni umoja ambao hauna maana kwa sababu haumtimizii haja zote za nafsi yake! Huu ni ubinafsi. Kama wanachama wa TANU, na hasa viongozi, hawatakiuhukumu chama chetu kwa mahitaji ya jamii yao, bali watakihukumu kwa mahitaji ya nafsi zao wenyewe, chama hakitadumu. Wanachama wa aina hiyo ni ugonjwa katika chama"

Mwalimu Nyerere anaendelea; " Dalili nyingine ya ubinafsi, na ambayo ni ugonjwa mbaya sana, ni fitina. Kanuni moja ya TANU inasema; "Nitasema kweli daima. Fitina kwangu ni mwiko." Lakini bado tunao wanachama ambao ni wafitini wakubwa bila kujitambua." (J.K Nyerere "Tujisahihishe",1962).

Hakika, uongozi wa Chama Cha Mapinduzi ungefikiria kukichapa tena kitabu hiki cha Mwalimu na kukigawa kwa viongozi na wanachama wake. Ni kitabu ambacho kinapaswa kusomwa pia na kila mzalendo wa nchi hii. Maana, aliyoyaandika Mwalimu Nyerere mwaka 1962 ndio yaanayotokea sasa ndani ya CCM. Hakika Mwalimu alikuwa na uwezo wa kuona .

Chanzo: Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates