Social Icons

Sunday, 13 September 2015

Askofu Gwajima alivyopenya kwa mke wa Dr. Slaa


ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, ambaye ndiye kiungo (mshenga) wa kufanikisha ujio wa Edward Lowassa, na kisha kuwania urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alijipenyeza kwa mke wa Dk. Wilbrod Slaa, Josephine Mushumbushi, kuhakikisha Slaa haondoki kwenye chama hicho, Raia Mwema, limeelezwa.

Gwajima alifanya hivyo ikiwa ni juhudi zake za kuhakikisha Dk. Slaa haondoki Chadema ili kumwongezea nguvu za kisiasa Lowassa na hatimaye kufanikisha ushindi wake wa urais, Oktoba 25, mwaka huu.

Ilikuwa asubuhi ya Julai 28, mwaka huu, Gwajima alifanya kazi ya ziada kumshawishi Josephine, akifanya hivyo baada ya kushindwa kuelewana na Dk. Slaa mwenyewe ambaye alikataa ushauri wake.
Dk. Slaa ndiye anayefichua hali hiyo inayoeleza namna juhudi mbalimbali zilizofanyika na viongozi kadhaa wa Chadema kupitia kwa Gwajima bila mafanikio. Mahojiano kwa kirefu na Dk. Slaa yamechapishwa katika gazeti hili.

“Kama hana hofu ya Mungu atapinga, na mimi ndiyo maana nikahoji hata uaskofu wa Gwajima kutokana na hilo. 
Kama Askofu anapokanusha vitu alivyosema sasa unategemea waumini watafanya nini? Gwajima amembembeleza mke wangu asubuhi ya tarehe 28, Julai, alipotoka nyumbani kwangu tumegombana, alikwenda kumtafuta mke wangu amemkuta Kibo Complex (Tegeta) wamekaa kwenye gari, mke wangu akaweka msimamo wa kutaka kutubembeleza anatushawishi tumkubali Lowassa, na ndiyo maana nikasema alipozungumza hoja ya maaskofu kuhongwa alikuwa anajenga hoja ya kwamba nimuunge mkono kwa sababu huyu mtu anaungwa mkono na watu wengine wengi.

“Bahati mbaya anatumia hoja kwamba amewanunua, mimi hasira yangu siyo kwa hela kutolewa kwa maaskofu, lakini askofu inafikaje mahali hatambui madhara ya rushwa, askofu ni mtu anayepaswa kupiga kelele dhidi ya rushwa, lakini yeye anaona huyu tumuunge tu mkono, sikushangaa baadaye kwa sababu kuna kauli imesemwa hata kama ni kufunga mkataba na shetani, ilitolewa na Tundu Lissu, tufanye tu mkataba huo ili kuiondoa CCM, mimi nimesema siwezi kukubali kufanya mkataba na shetani kwa ajili ya lengo lolote lile.

“Kuna mahali katika theolojia, kuna kitu kinaitwa ‘the end justifies the means, naomba hawa wote wanaoutumia huu msemo waende shule wasome Theoloji ya Thomas wa Aquino, waelewe huo mfano unatumika katika mazingira gani, sababu ni hasara ya watu au kuwa wasomi nusu wanachukua misemo hawajui hata misingi yake, nimesoma theoloji najua maana ya Mtakatifu Thamos wa Aquino anaposema the end justices the means, siyo katika mazigira haya na kama watu ahwajui basi waache kutoa nukuu amabzo hawajazifanyia utafiti,” alisema

Slaa na urais wa Lowassa
Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chadema, Dk. Slaa, katika hatua nyingine amezidi kuhatarisha mbio za mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa.

Katika kuhatarisha huko, safari hii, katika mahojiano maalumu na Gazeti hili la Raia Mwema, Dk. Slaa amefichua utajiri wenye shaka wa Lowassa.

Kwa mujibu wa mahojiano hayo hayo yaliyochapishwa kwa kirefu katika kurasa za 14 na 19 za gazeti hili, anasema; “Lowassa, watu wengi hawajui anahusika na utajiri wa aina gani, ndiyo maana swali analotakiwa kujibu ni uhalali wa utajiri wake, asiendelee kuwapumbaza Watanzania kwamba anachukia umasikini, tunajua utajiri siyo kosa, si dhambi, si ufisadi, ufisadi ni namna ulivyopata utajiri wako.”

Akisimulia zaidi, anasema; “Tarehe 07, April, 1997 (Lowassa) alianzisha yeye na mke wake Regina kampuni inayoitwa Barare Ltd, katika kampuni hiyo Lowassa ana hisa 500 na Regina ana hisa 500, na hii ni 1997, akiwa mbunge tu, hisa 500 zilikuwa na thamani ya shilingi milioni 50, niambie hizo milioni 50 kila mmoja walizipata wapi? Kumbuka Frederick Sumaye akiwa Waziri Mkuu, alituhumiwa kwa kukopa NSSF milioni 50, huyu hakukopa alizipata wapi?”

Alisema Lowassa ana mali nyingi ambazo hajaziorodhesha kwenye Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma, jambo ambalo ni kosa, akiongeza kwamba baada ya Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu, Juni 30,2010, kampuni hiyo ikanunua hisa 7,500 kwa shilingi 60,000.

“Hiyo ni jumla ya shilingi milioni 450, jiulize wakati huo Lowassa amemaliza miaka miwili ya uwaziri mkuu, akabaki mbunge wa kawaida, hivi milioni 450 huyu Lowassa alizitoa wapi? 

Lakini Lowassa ni mbunge wa kawaida posho za mbunge wa kawaida zinajulikana, na mshahara unajulikana milioni 450 zilitoka wapi, ingekopwa tungeona kwenye fomu yake ya maadili kule kwenye Sekretariati ya Maadili na kosa kubwa zaidi hata kule hakueleza kwamba ana hisa zimenunnuliwa kutoka kwenye kampuni inaitwa Integrated property Limited, kutokutaja hisa zako kwenye Sekretariati ya Maadili ni kosa linalofanya mbunge afutwe ubunge bila hata kwenda mahakamani,” alisema.
Katika hatua nyingine Dk. Slaa alionya kuhusu pupa ya mabadiliko wanayoyataka Watanzania, akisema yanaweza kuleta majuto badala ya neema wanayoitarajia.

“Watanzania wajiulize mabadiliko daima yana sura mbili kuna mabadiliko mema na kuna mabadiliko mabaya, hata Hitler kwa wakati wake alileta mabadiliko yakaishia kuua mamilioni ya watu, kwa hiyo sisi tunaojua kwenye dhamiri zetu hatuwezi kukaa kimya,” alisema. 

Chanzo. Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates