Social Icons

Friday, 2 October 2015

Mpambano kati ya Shitambala na Mbilinyi Jijini Mbeya.


ZIKIWA zimebaki siku takribani 35 kupiga kura, ushindani katika Jimbo la Mbeya Mjini umebaki kati ya mbunge aliyemaliza muda wake, Joseph Mbilinyi na Sambwee Shitambala.


Wagombea hao wawili wanatoka kwenye vyama viwili vikuu na vyenye ushindani mkubwa tangu Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2010. Vyama hivyo ni Chadema kinachowakilishwa na Mbilinyi na CCM kinachowakilishwa na Shitambala.


Mbali ya ushindani wa vyama vyao, wagombea hao pia wana ushindani wao wenyewe, ikizingatiwa kuwa katika chaguzi zilizopita, Shitambala aliwania ubunge Jimbo la Mbeya Vijijini ambapo baada ya kushindwa alijiengua na kuhamia CCM.


Shitambala anakifahamu vema chama chake hicho cha zamani na ananukuliwa akisema anazifahamu mbinu zilizotumika na chama hicho kushinda katika uchaguzi uliopita. Hata hivyo mazingira ya uchaguzi wa mwaka huu kwa jimbo hilo yamebadilika, uhasama uliokuwepo ndani ya Chama cha Mapinduzi, haupo tena.


Wachambuzi wa siasa za jimbo hilo wanabainisha kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu ushindani ni mkubwa na hakuna mteremko kwa vyama vyote kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita. Ni uchaguzi unaoelezwa kutengemea zaidi namna kila chama kitakavyochanga karata zake.


Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Mbilinyi hakupewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini alinufaika na mgogoro ulioibuka ndani ya CCM jimboni humo, ambapo kambi ya Thom Mwang'onda inadaiwa kutoridhishwa na matokeo ya kura za maoni hivyo kuamua kukiadhibu chama chao kwa kuungana Chadema, hatua iliyomwezesha Mbilinyi kuibuka mshindi.


Pamoja na mgogoro huo kukinufaisha Chadema, nguvu ya mgombea wake wa nafasi ya urais katika uchaguzi huo, Dk Wilbrod Slaa nayo inaelezwa kuchangia kwa kiwango kikubwa kukijenga chama hicho jimboni humo na Mkoa wa Mbeya.


"Watu walimwamini Dk Slaa, ana uwezo mkubwa wa kushawishi, alikuwa na nguvu kubwa, angeweza amuru watu wafanye chochote na wangefanya," anasema kiongozi mmoja wa Chadema mkoani Mbeya, lakini akiomba kuhifadhiwa jina lake.


Mazingira hayo mwaka huu hayapo, chama hicho kitalazimika kufanya kazi ya ziada kufanikiwa kuendelea kulishikilia jimbo hilo, ambalo ni kati ya majimbo muhimu katika siasa za nchi. Migawanyiko iliyokuwepo CCM na ambayo iliwarahisishia Chadema kulitwaa jimbo hilo haipo tena na Dk. Slaa hayupo tena na chama hicho.


Migogoro itokanayo na kura za maoni inavikabili vyama vyote viwili, na kwa Chadema unakuwa mtihani wao wa kwanza, hawakuizoea, mtu alijiunga na kupewa nafasi ya kugombea nafasi za ubunge bila kusababisha migawanyiko. Safari hii wameingia kwenye kampeni wakiwa sio wamoja tena baada ya kura za maoni, walioshindwa wakilalamikia mchezo mchafu ikiwemo matumizi makubwa ya fedha.


Wakati Chadema wakionja adha ya migogoro itokanayo na kura za maoni, mahasimu wao wamepumua, hali ya uhasama ni tofauti sana na ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita. Katika hatua ambayo hata viongozi wa chama hicho hawakuitegemea, makundi hayakujitokeza baada ya kura za maoni, na hivi sasa wameungana kwenye kampeni.


Hatua ya wanachama kupinga wazi wazi ujio wa baadhi ya wanasiasa toka CCM kwa lengo la kupewa nafasi za kuwania nafasi za uongozi, udiwani hadi urais, ni ujumbe tosha kwamba mwaka huu mambo sio rahisi kama ilivyokuwa huko nyuma.


Mwanjelwa yaumiza vichwa vya wagombea

Miongoni mwa maeneo yanayoumiza vichwa vya wagombea na vyama vyao ni eneo la kibiashara la Mwanjelwa, ni eneo la kimkakati zaidi, likiwa na ushawishi kwa maeneo mengine ya Jiji la Mbeya. Ni eneo linalowakutanisha wakazi wote wa Jiji hilo, wakitumia muda wao mwingi wa mchana.


Mmoja wa wanachama wa CCM aliyewania kuteuliwa na chama hicho katika nafasi ya ubunge, Ulimboka Mwakilili anasema ukikamata Mwanjelwa unakuwa umekamata pia sehemu ya kata ya Iyela, miongoni mwa kata kubwa jimboni humo na yenye wapiga kura wengi zaidi.


Pamoja na Iyela, pia unakuwa na ushawishi mkubwa kwenye kata za Luanda Nzovwe, Isanga na Ilemi, kata zenye wapiga kura wengi pia. Pamoja na wingi wa wapiga kura, ni maeneo ambayo wakazi wake sio watu wenye mahaba na vyama bali huamua kulingana na ushawishi wa wagombea, kihaiba na uwezo wake wa kumkabili changamoto. Ni wapiga kura wasiotabirika.


Mwanjelwa, hususani, eneo la Kabwe imekuwa ngome kuu ya Mbilinyi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ambapo mgombea huyo wa Chadema aliweza kutoa agizo lolote likatekelezwa, na kufikia hatua ya serikali kuliogopa eneo hilo.


Hata hivyo, hali imebadilika, hususani mitazamo ya wafanyabiashara ambao awali wanaelezwa kufadhili harakati za mbunge huyo aliyemaliza muda wake. Safari hii wamekuwa watazamaji zaidi kuliko wanaharakati, huku ilielezwa kuwa wamejiweka pembeni kutokana na kutoridhishwa na mwenendo mzima wa siasa za eneo hilo la Mwanjelwa kwa kipindi kilichomalizika.


Taarifa ambazo bado kuthibitishwa na Mamlaka ya ya Jiji hilo, zinaeleza kuwa, wafanyabiashara hao wamejikuta njia panda wakihofia biashara zao, sababu kuuikibainishwa kuwa ni kubainika kwao kuhusu kufadhili harakati mbalimbali zilizoisumbua serikali eneo hilo.


Harakati zilizofanyika baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita jijini humo, zimeacha makovu ikiwemo vilema vya viungo kwa baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la Soweto, wakiwemo majeruhi wa risasi.


Inaelezwa zaidi kwamba wafanyabiashara hao hawaoni uwezekano wa Chadema kushinda nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka huu kutokana na kile wanachokieleza kuwa ni kubeba tope la CCM na kuachana na ajenda ya ufisadi, iliyowajenga na kuwavutia wananchi wengi wa Jiji hilo.


Ni mazingira hayo, ya kuwepo migawanyiko inayotokana na kura za maoni na hatua ya kuwakaribisha waliowatuhumu kwa ufisadi na kuwapa nafasi ya kugombea nafasi za juu za uongozi, tena kwa kuishi na demokrasia, ndiyo yenye kuliweka Jimbo hilo katika nafasi sawa kwa kila chama.


Mbinu kuu inayotumika na chama hicho Kikuu cha upinzani nchini, ni kusimamia hoja ya mabadiliko kwa kuiondoa CCM madarakani. Hata katika mijadala maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo, Chadema husimamia hoja ya mabadiliko kwa kuiondoa CCM madarakani, na sio sera au kuzungumzia ufisadi.
Pamoja na mvutano huo, Mbilinyi ananufaika na hatua ya Shitambala kuhama vyama, wapiga kura jijini humo wanamuona kuwa kiongozi asiyeaminika.


"Sugu hamna kitu, lakini kwa Shitambala, anapita, alitukwaza sana huyu, haaminiki," anasema mfanyabiashara mmoja wa Ilomba aliyejitambulisha kwa jina mmoja tu la Mariam.


Vurugu mikutanoni
Zimekuwapo taarifa za kutokea kwa vurugu kwenye baadhi ya mikutano ya kampeni ya vyama hivyo hasimu wa kisiasa. Hata hivyo kila chama kinamlaumu mwenzie kuwa chanzo cha vurugu.
Tukio lililotolewa taarifa Polisi ni lile la msafarawa mgombea wa Chadema, Mbilinyi kushambuliwa na wafuasi ya CCM katika kile kilichoelezwa kuingilia mkutano wao.


Hata hivyo, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Jimbo la Mbeya Mjini, Musa Zungiza alisema ofisi yake haijapokea taarifa rasmi za tukio hilo kama sheria ya uchaguzi inavyoelekeza.
"Tulitegemea kama limetokea, wangeleta lakini hadi leo (20/09/2015) hatujaletewa taarifa," alisema Zungiza.


Kwa mujibu wa msimamizi huyo, taarifa inatakiwa kutolewa ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio.
Kampeni za ubunge ndizo zenye kufuatiliwa zaidi na wakazi wa Jiji hilo ikilinganishwa na zile za udiwani, jambo ambalo linahofiwa kuchangia Baraza la Madiwani lisilo na nguvu.


Chanzo. Raia mwema 

No comments:

 
 
Blogger Templates